NA BASHIR YAKUB-
Kuongezeko kwa makampuni na taasisi mbalimbali kumeleteleza wingi wa ajira maeneo mbambali ya nchi. Mbali na kuongezeka kwa ajira hizi kumekuwepo na tatizo kubwa la waajiriwa kutojua haki zao mbalimbali wawapo maeneo ya kazi. Niseme jambo moja tu kuwa hakuna suala la msingi kama muajiriwa kujua haki zake. Hii ni kwasababu kupitia kujua haki zake ndipo anapoweza kupata ujira stahiki, posho stahiki, masurufu stahiki, mafao stahiki, malipo stahiki ya kuachishwa kazi ikiwa ni pamoja na ujumla wa kufanya kazi kwa misingi ya kazi.
Ni muhimu kila mfanyakazi kupitia pitia haki zake mara kwa mara ili kujua nini anapata na nini hapati. Uwe kazini au umeachishwa bado ipo nafasi ya kudai haki hizi ili upate kilicho chako. Ukitegemea mwajiri ndio akwambie haki zako utakuwa unajidanganya kwasababu yawezekana kabisa faida kubwa ya mwajiri ipo katika wewe kutokujua haki zako. Ni hasara kubwa kufanya kazi bila kujua haki zako . Kutokana na hilo leo nitaeleza baadhi ya haki za mfanyakazi.
1. HAKI YA KUJUA SEHEMU YA KUFANYIA KAZI.
Isiwe uliambiwa eneo la kazi ni Dar es salaam halafu ujikute kila siku una safari za mikoani halafu uambiwe eti hiyo ndiyo kazi yenyewe, hapana. Lazima eneo la kufanyia kazi lijulikane kwa mfanyakazi. Ijulikane kuwa umeajiriwa na eneo lako la kazi ni Dar es salam , au Mwanza au Kagera. Hii ina maana kubwa kwakuwa mfanyakazi asipojua eneo lake la kazi hataweza kudai malipo yatokanayo na kufanya kazi nje ya ofisi . Lakini iwapo unajua eneo lako la kazi basi utakapokuwa nje ya eneo la kazi yakupasa kudai malipo ya ziada. Kwa hiyo hakikisha mwajiri wako unakuainishia kwa uwazi kabisa eneo lako la kazi na ulijue. Nje ya hilo eneo ni malipo mengine ambayo ni nje ya mshahara wa kawaida.
2. HAKI YA KUJUA MAHALI/SEHEMU MWAJIRI ALIPOKUTOA.
Waweza kuwa unakaa Mwanza lakini mwajiri amekuitia kazi Dar es salaam . Au makazi yako ni Arusha lakini kazi iko Mbeya. Mazingira kama haya yanazaa haki ya msingi unapokuwa unaajiriwa. Umuhimu wake ni kuwa wakati wa kustaafu au kumaliza mkataba au ikitokea umeachishwa kazi basi ni wajibu wa mwajiri kuhakikisha anakusafirisha kutoka eneo la kazi mpaka alipokutoa. Anatakiwa kukusafirisha kwa kutoa usafiri au kutoa gharama za usafiri ukasafiri mwenyewe. Hautoweza kupata haki hii iwapo hujui kitu kama hiki.
3. HAKI YA KUJUA AINA YA KAZI UNAYOTAKIWA KUFANYA.
Lazima kazi unayotakiwa kufanya ijulikane vyema. Isiwe unafanya kila kazi inayokuja mbele yako. Mchanganuo wa kazi uwe wazi. Kama ni sekretari ijulikane kazi ni zipi na zipi. Kama ni meneja ijulikane kazi ni zipi na zipi kwa mchanganuo wenye kueleweka kabisa. Hii husaidia kutofanya kazi ambazo si zako au kufanya kazi nje ya makubaliano. Kwa kujua haki hii kazi yoyote utakayopewa iliyo nje ya mchanganuo wa kazi zako, utapatana upya na malipo yake yatatakiwa kuwa nje ya mshahara.
4.HAKI YA KUJUA MCHANGANUO WA MSHAHARA.
Mshahara ni jambo moja lakini mchanganuo wa mshahara huo ni kitu kingine. Mwajiri anaweza kukwambia mshahara ni laki saba . Swali ni je laki hiyo saba inagawika vipi. Ili uendane vizuri na haki hii mara nyingi usiiangalie ile laki saba isipokuwa angalia mchanganuo wa laki saba. Lazima mwajiri aoneshe kati ya hiyo laki saba mshahara kamili( basic salary) ni upi, kodi itakuwa kiasi gani, posho ya usafiri itakuwa kiasi gani, posho ya chakula itakuwa kiasi gani, posho ya pango la nyumba ya mfanyakazi itakuwa kiasi gani, fedha za mfuko wa hifadhi ya jamii kiasi gani, na makato mengine yote ambayo hutokana na makubaliano kati ya mwajiri na mwajiriwa yajulikane vyema. Hii husaidia hata kudai malimbikizo kwa usahihi baada ya kazi kuisha. Huwezi kupata stahiki zako kwa kiwango unachotakiwa kulipwa hasa baada ya kazi kuisha kama huyajui haya.
5.HAKI YA KUJUA AINA YA MKATABA WA KAZI.
Wapo watu ambao wako makazini na hela wanapata na maisha yanakwenda lakini hawajui wanafanya kazi kwa mkataba wa aina gani. Ni hatari kutojua aina yako ya mkataba kwakuwa utalazimika kukosa baadhi ya haki zinazotokana na mkataba wako yakiwemo malipo na posho nyinginezo. Lazima ujue kama mkataba wako ni wa muda au wa kudumu. Mkataba wa muda unao masurufu yake na wa kudumu unao masurufu yake. Usipolijua hilo utayakosa hayo masurufu. Mkataba wa muda wa ajira ni ule ambao ni wa kipindi fulani kwa mfano mwaka mmoja lakini waweza kuongeza au miaka miwili n.k. Kwa hiyo ni vyema upitie mkataba wako wa ajira ili ujue ni wa aina ipi.
6. HAKI YA KUJUA KAMA KUNA KIPINDI CHA MPITO.
Kipindi cha mpito hujulikana kama probation period. Hiki ni kipindi ambacho unakuwa umeajiriwa lakini ukiwa chini ya uangalizi maalum wa kupima ufanisi wako katika kazi. Ni muhimu kuwekwa wazi kipindi hiki kitaanza lini na kuisha lini na ni haki zipi ulizonazo ndani ya kipindi hicho. Nasema hivyo kwakuwa wapo watu ambao wamewekwa katika kipindi hiki kwa miaka mingi tu huku wakikosa stahiki kamili za ajira na pia wakikosa hata stahiki za hicho kipindi. Hii si sawa na hulenga kumminya mfanyakazi na kumfaidisha mwajiri. Hivyo ni muhimu uambiwe kipindi hiki kinaanza lini na kinaisha lini na una haki gani ndani ya kipindi hicho
0 comments :
Post a Comment