Na Luqman Maloto
Angel in disguise ni msemo wa Kiingereza wenye maana kuwa Malaika anaweza kukujia
katika sura ya Shetani. Maana nyingine ni Shetani kukutokea kwa umbo la Malaika. Akili
ikae kichwani.
Kwamba rafiki mzuri anaweza kukujia kwa mazingira ya uadui. Yupo ambaye
aliharibikiwa na gari njiani, katika kutafuta msaada, akakutana na mwanamke ambaye
baadaye alikuwa mke wake mwema kabisa.
Au yule aliyeumwa kwa muda mrefu, mke wake akashindwa kumjali, akawa anateseka
wodini, lakini akatokea nesi akampa huduma bora kabisa na baadaye walifunga ndoa,
wakaishi kwa upendo, amani na furaha tele.
Kumbe basi ile hali ya kuharibikiwa na gari ni tukio baya lenye neema ndani yake, kama
ilivyo kwa yule aliyeugua na kutelekezwa wodini, matokeo yake alimpata mke bora
asiyeweza kumfananisha na chochote. Hiyo ndiyo tafsiri ya Angel in disguise!
Mwanamke aliporwa na vibaka, akakosa mpaka nauli ya kurudi nyumbani. Alipokuwa
anatapatapa kutafuta msaada, ndipo akakutana na mwanaume aliyemsaidia nauli. Na
mwanaume huyo leo hii ndiye mume wake. Wanaishi raha mustarehe.
Hii ina maana kuwa Malaika wa heri alimshukia katikati ya tendo la kuporwa na vibaka.
Kwamba vibaka walimsaidia kumkutanisha na mume wake anayemfanya ayafurahie
maisha leo.
Yupo aliyefukuzwa kazi, akawa anatapatapa mitaani, ndipo akagundua kipaji chake na
uwezo mkubwa alionao. Hivi sasa ni bilionea wa mfano. Asingefukuzwa kazi, pengine
angezeeka kwenye ofisi za watu. Leo hii asingeitwa bilionea shujaa.
Mwingine kero za nyumba za kupanga na manyanyaso ya nyumba za ndugu, ndiyo
yalimtia hasira, akafanya kazi kwa bidii na akawekeza fedha zake kwenye ujenzi. Leo
hii anamiliki nyumba saba. Sita amepangisha, moja anaishi na familia yake.
Yupo ambaye alitoka kujisaidia, nyuma yake basi lilimwacha. Alisonya na kuumia kupita
kiasi. Muda mfupi baadaye akapokea taarifa kuwa gari lililomwacha, lilipata ajali na
watu wengi walifariki dunia na waliosalia, wengi wao walijeruhiwa vibaya.
Mwingine alibanwa na shida kubwa ya fedha, ndugu wenye uwezo walikataa hata
kumkopesha. Akaenda taasisi za mikopo akanyimwa. Akakata tamaa, machozi
yakamtoka. Akahisi dunia inamuelemea. Siku iliyofuata alipokea hundi yake ya malipo
kwa fedha alizokuwa anadai ambazo hakutegemea kama angelipwa haraka kiasi hicho.
Ina maana Mungu alimuokoa na mkopo ambao angerejesha na riba. Alimzuia ili apate
fedha zake za bila amsharti. Na ziliweza kutatua matatizo yake yote. Vilevile alipata
kujua undugu wake na ndugu zake upoje. Kwamba kumbe siyo wa kutegemea. Lazima
awe imara kukabili changamoto zake bila kuwazia uwepo wa ndugu.
Ikufundishe kutambua kuwa Malaika wa heri kutoka kwa Mungu, huwa wapo karibu na
wewe mno. Hukulinda dhidi ya changamoto nyingi. Hukukinga dhidi ya majaribu na
mitihani mingi. Huruhusu mengine yakupate kwa sababu maalum.
Amini kuwa zipo neema nyingi katikati ya kila shari. Upo mpango mzuri kwa ajili yako.
Na wakati mwingine mpango huo siyo rahisi kuufikia bila kupitia majaribu na mitihani.
Yale majaribu na mitihani, Mungu huruhusu yakufike kama sababu ya kukuelekeza
kwenye mpango mzuri ulioandaliwa kwa ajili yako.
Binadamu asili yake ni kubweteka. Hali inapotulia, husahau kuchangamkia fursa
nyingine. Mungu anaposhusha mtihani, anakuwa na maana yake.
Hivyo basi, pokea kila hasi inayokufikia leo kama chanya. Tambua kuwa zipo fedha
nyingi baada ya mitihani. Yapo mapenzi matamu baada ya kuvuka majaribu. Ipo kazi
nzuri baada ya mataabiko. Upo ufalme baada ya utumwa, upo ubwana baada ya
utwana!
Jiwekee utaratibu huu kuanzia leo; Ukipatwa na baya, usivunjike moyo, usinung’unike,
usiwaze visasi, usiweke kinyongo, usiwe mwekundu kwa hasira na kadhalika, badala
yake mshukuru Mungu, maana hujui ni neema gani amekuandalia kupitia hilo baya
lililokufika.
Tambua kuwa baya na jema, yote hayakufikii bila ridhaa yake. Ukijikuta ndani ya jaribio
la maisha, elewa kuwa Mungu ametaka iwe kwa sababu anakupenda na anakuamini
sana. Kwamba baada ya hapo atatakuvusha kwenda mahali bora zaidi.
Mungu humpenda sana yule anayetambua uwepo wake. Kuonesha umeumia na kutoa
matamshi ya kufuru humchukiza Mungu. Ukiweza kushukuru na kutabasamu katikati ya
majaribu, wewe ni mpendwa hasa wa Mungu. Naye atakuonesha miujiza.
Soma Kitabu cha Nne, Zaburi 91:14-16: “Kwa kuwa amenipenda kwa msisitizo,
nitamwokoa na kumweka juu. Kwa kuwa amenijua jina langu, ataniita nami nitamwitikia,
nitakuwa pamoja naye taabuni, nitamwokoa na kumtukuza. Kwa siku nyingi
nitamshibisha. Nami nitamwonesha uokovu wangu.”
Neno hili la Mungu katika Kuran, likuongezee hali ya kujiamini na tabasamu. Anasema
katika Sura ya Banii Israail (Wana wa Israel), 17:29-30: “Wala usifanye mkono wako
kama uliofungwa shingoni mwako (kujikunyata), wala usiukunjue mkunjuo kabisa, usije
ukakaa hali ya kujilaumu na kuhisi kufilisika.
“Hakika Mola wako humkunjulia riziki amtakaye na kumtia katika dhiki mtu amtakaye.
Hakika yeye kwa waja wake ni mwenye habari zote na anaona kila kitu.”
Tuwe na imani hai, tumkumbuke Mungu muda wote kwa mazuri yetu na mabaya
yanayotufika. Tuheshimu uwepo wa Mungu na miujiza yake.
Nakutakia Jumapili njema.
-
Blogger Comment
-
Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments :
Post a Comment