-->

ACT WAZALENDO TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Wananchi wanaumizwa na mgogoro Zanzibar

CHAMA cha ACT-Wazalendo kinasikitishwa na hali ngumu ya maisha inayowakumba wananchi wa Zanzibar kutokana na mkwamo wa kisiasa unaoendelea visiwani humo.

Wakati wa mkutano wa tathmini ya hali ya kisiasa ya Zanzibar uliofanyika Unguja kati ya Desemba 19 na 20 mwaka huu, Kamati ya Uongozi ya Chama cha ACT-Wazalendo imefanya tathmini ya kina kuhusu hali ya kisiasa viswani Zanzibar, ikiwemo kuongea na wananchi wa kawaida kuhusu nini hasa kinaendelea. Athari za mkwamo wa kisiasa Zanzibar zimeshaanza kujitokeza katika maisha ya wananchi.

Bei za vyakula na huduma nyingine zimepanda kwa kiwango cha kutisha. Sekta ya utalii ambayo ni muhimu kwa uchumi wa Zanzibar imeathirika kiasi kwamba ziko hoteli ambazo zimepokea nusu tu ya idadi ya watalii zilizotarajiwa kuwapata kipindi hiki cha mwishoni mwa mwaka.

Athari hii ya kutokuja kwa watalii haiwagusi wamiliki wa hoteli pekee, kwani ujio wa wageni husaidia kuchagiza biashara nyingine mbalimbali za wenyeji zikiwamo za waongoza watalii, wauza bidhaa pendwa, wasafirishaji na kada nyingine katika mnyororo wa biashara ya utalii. Idadi ya watu wasio na kazi imeongezeka kwa kasi kubwa katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita kwa sababu ya kudorora kwa utalii Zanzibar.

Ili kupata picha halisi ya nini kinaendelea Zanzibar, ni vema tukawapa takwimu kwa mujibu wa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Zanzibar. Mfumuko wa bei wa Zanzibar, hivi sasa umefikia kiwango cha asilimia 11 ambacho hakijawahi kufikiwa katika miaka ya karibuni.

Bei za bidhaa hususani vyakula zimepanda kwa kiwango cha asilimia 16.4, huku vyakula vya baharini, kwa mfano samaki, mfumuko wake wa bei umefikia kiwango cha takribani asilimia 30. Bidhaa kama Viazi, Mchele na Sukari vimepanda bei kwa kasi na kuumiza wananchi wa hali ya chini.

Kwa kulinganisha, mfumuko wa bei kwa Tanzania ni asilimia 6.6 kwa mujibu wa taarifa ya mwezi uliopita ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS). Huu ni ushahidi wa wazi kwamba mkwamo huu wa kisiasa umeanza kuwaumiza wananchi wasio na hatia.

ACT-Wazalendo inasema kwamba hali hii ya kuumiza wananchi wa kawaida haikubaliki na ni LAZIMA ifikie ukomo haraka iwezekanavyo. Hatuwezi kuumiza wananchi wetu kwa sababu zisizo na maana.

Ili kuwaokoa wananchi na maumivu haya, Kamati ya Uongozi ya ACT-Wazalendo imekaa na kutafakari suala hili la Zanzibar na hivyo inapendekeza yafuatayo;

Mosi, Mshindi wa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25 mwaka huu atangazwe haraka ili hali ya utulivu wa kawaida irejee. Mshindi ale kiapo, aunde Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kuwaunganisha Wazanzibari.

Pili, ACT-Wazalendo imebaini kuwapo kwa idadi kubwa isivyo kawaida ya wanajeshi wanaolinda Bandari, Uwanja wa Ndege, Vituo vya Redio na maeneo mengine muhimu. Chama chetu kinataka askari hao warejee makambini kwao kwani uwepo wao katika maeneo ya kiraia unasababisha hali ya shaka na hofu miongoni mwa wananchi.

Tatu, kwa ajili ya mustakabali mwema wa Zanzibar, ACT-Wazalendo kinataka mazungumzo yoyote kuhusu uchaguzi uliofutwa yahusishe wadau wa vyama vyote na taasisi nyingine walioshiriki kwenye uchaguzi.

Hii si mara ya kwanza kwa viongozi wa vyama vya CCM na CUF kukutana na kufanya mazungumzo baada ya kutokea matatizo. Lakini uzoefu unaonyesha kwamba suluhisho huwa si la kudumu na badala yake matatizo yaleyale hujirudia baada ya muda.

Suluhisho la hali hii ni vyama vingine vyote, kujumuishwa katika aina hii ya mazungumzo ili kupata mawazo jumuishi na yatakayowakilisha sehemu kubwa zaidi ya Wazanzibari ambao wengi wao, hasa kizazi kipya, hawana uhusiano wowote na vyama hivyo viwili.

Kwa ujumla hali ya kisiasa Zanzibar ni mbaya sana na inatisha kwani wananchi wanaishi kwa hofu kubwa na hawaelewi kinachoendelea, ukimya uliotamalaki hauashirii hatima njema ya siasa za Zanzibar.

ACT-Wazalendo kinapenda kutumia nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru wananchi wa Zanzibar kwa subira na uvumilivu wa kiwango cha juu waliouonyesha katika kipindi hiki cha hali ya sintofahamu.

Imetolewa leo, Desemba 20, 2015.

Mji Mkongwe, Zanzibar

Kabwe Z Ruyagwa Zitto,Mb
Kiongozi wa Chama

Share on Google Plus

About Omari Makoo

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment