Kwa miaka takribani kumi na mitano (2000 – 2015) Tanzania imekuwa na uchumi unaokua kwa kasi ya wastani wa 7% kwa mwaka. Hata hivyo kasi hii ya kukua kwa uchumi imeshindwa kuondoa umasikini wa wananchi kwani kwa kiasi kikubwa kasi hii imesukumwa na mitaji kutoka nje ambayo imewekezwa kwenye sekta ambazo haziwanufaishi wananchi moja kwa moja kama vile Madini, Mafuta na Gesi, Mawasiliano ya Simu na Uchuuzi. Ni muhimu kasi ya ukuaji wa uchumi iendane na kiwango cha uwekaji akiba cha Taifa (National savings rates).
Wakati uwekaji akiba Tanzania upo katika kiwango cha 16%, nadharia za uchumi zinaelekeza kuwa “Nchi zenye malengo ya kukua kwa 7% kwa mwaka inabidi ziwe na uwekaji wa akiba wa 35% ya pato la Taifa” (Pinto, 2014).
Kwa uwekaji akiba nchini ni wa chini na duni, uhuru wa nchi unahatarishwa kwa kutegemea sana mitaji kutoka nje. Ili kuondokana na mrija huu wa mitaji ya nje, Chama cha Wazalendo kinataka kuhimiza uwekaji akiba kupitia mfumo wa hifadhi ya jamii ( Social Security Systems).
Licha ya Hifadhi ya Jamii kuwa ni kwa ajili ya pensheni, ACT-Wazalendo itatumia hifadhi ya jamii kama nyenzo (instrument) ya kukuza uwekaji akiba nchini ili kuweza kuwa na vyanzo vya mitaji ya uwekezaji wa ndani.
Moja ya sababu kubwa ya kuwa na mporomoko wa thamani ya sarafu ya Tanzania ni nakisi ya uwekaji akiba maana ‘nchi yenye nakisi ya akiba, sarafu yake hushuka thamani mpaka pale mali zake zinapokuwa rahisi sana kiwango cha kuvutia akiba za nje kuingizwa nchini’.
Bila ya kuwa na uwekaji akiba mkubwa nchini, nchi yetu itakuwa kwenye mnyororo wa mitaji kutoka nje ambayo inahatarisha uhuru wa nchi yetu katika kuamua namna ya kuwekeza na maeneo gani ya kuwekeza.
Uwekezaji wa miradi mikubwa yenye faida kwa nchi kama miundombinu ya umwagiliaji, viwanda vya kusindika mazao ya kilimo, barabara kuu, reli, bandari, viwanja vya ndege, vyuo vikuu na vyuo vya ufundi utafanywa na akiba kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kwani kwa uasili wake madai dhidi ya mifuko (liabilities) ni ya muda mrefu. Iwapo Watanzania milioni tano tu kati ya Watanzania milioni ishirini na mbili waliopo kwenye nguvu kazi wakiweka akiba ya shilingi thelathini elfu tu kwa mwezi (shilingi 20,000 itachangiwa na mwananchi na shilingi 10,000 na Serikali kwa kila mwananchi mchangiaji), akiba itakayowekwa itakuwa ni shilingi 1.8 trilioni kwa mwaka, sawa na 2.5% ya Pato la Taifa. Fedha hizi ni sawa na jumla ya Fedha zote Tanzania imeingiza kama Foreign Direct Investments kutoka nje mwaka 2013. Fedha hizi ni mtaji tosha kwa uwekezaji kwenye miradi ya muda mrefu na yenye kuweza kulipa vizuri na kufaidisha wanachama wa hifadhi ya jamii.
Kuna ugumu kwa watu masikini kujiwekea akiba kwa sababu ama ya kipato kiduchu au kutokuwa na nidhamu ya kuweka akiba. Hata hivyo, watu masikini wengi katika nchi yetu ni wanachama wa vyama vya kuweka na kukopa (SACCOS) ili kuweza kufikia akiba yao wanapokuwa na mahitaji kama vile matibabu, elimu ya watoto wao na kupata mikopo ya gharama nafuu ili kuanzisha biashara ndogondogo. Mfumo wa Hifadhi ya Jamii utamwezesha masikini kuweka akiba kupitia vyama vyao vya hiari vya SACCOS na kupata mikopo nafuu ili kuongeza kipato chao. Muhimu kuliko yote mwanachama atapata Bima ya Afya na hivyo kuweza kupata matibabu bure bila ya kuathiri michango yake katika mfuko wa hifadhi ya Jamii. Hifadhi ya Jamii kwa wote itakuwa nguzo muhimu katika Sera za Chama cha ACT-Wazalendo na nyongeza muhimu sana katika kuhuisha Azimio la Arusha.
Katika kutekeleza Azimio la Arusha, Serikali ya wakati huo ilianza kampeni ya wananchi kuhamia kwenye vijiji vya ujamaa. Msukumo mkubwa pamoja na mambo mengine ulikuwa ni kuiwezesha Serikali kutoa huduma za kijamii kwa urahisi. Vilevile wananchi walilima kwenye mashamba ya ujamaa kwa kutumia kauli mbiu nyingi ikiwemo kilimo cha bega kwa bega. Chama cha ACT- Wazalendo kitaka nataka Serikali kuwafuata wananchi huko walipo vijijini na kuwawezesha kulima mashamba yao binafsi wenyewe kwa tija kwa kupitia ushirika wa msingi ili kuongeza uzalishaji, kufungua viwanda vidogo vidogo vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo vijijini na kuunganisha uchumi wa vijijini na uchumi wa Taifa.
Ujamaa wa kidemokrasia unaosimamiwa na ACTWazalendo ni ujamaa wa kuzalisha na sio ujamaa wa kugawana tu…
#AzimioLaTabora la #ACTwazalendo
0 comments :
Post a Comment