Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr. Jakaya Kikwete akihutubia Wazee wa Dar es Salaam.
Rais Kikwete anamfahamu fika Harbinder Singh Sethi wa IPTL kwa kuwa singasinga huyo alitokea ikulu kabla ya kukwapua mabilioni ya shilingi kutoka akaunti ya Escrow katika Benki Kuu. Saed Kubenea anaandika.
Ni vigumu kwa Rais Jakaya Kikwete kufanikiwa kujitenga na kashfa ya ukwapuaji wa zaidi ya Sh. 321 bilioni zilizochotwa katika akaunti ya Tegeta Escrow, MwanaHALISI Online, limeelezwa.
“Mimi sina tatizo na maelezo ya rais,” anaeleza waziri na kuongeza, “umma unasubiri kujua huyo ‘mmoja wa wanafimilia wa Kikwete’ aliyempeleka singasinga ikulu, ni nani.
Taarifa zinasema , anayejiita na kuitwa na serikali kuwa ni “mmiliki mpya wa IPTL/PAP,” Harbinder Singh Sethi, aliletwa nchini na mmoja wa wanafamilia wa Rais Kikwete.
Inaelezwa kuwa singasinga alikutana na rais, ikulu jijini Dar es Salaam; na kutoka hapo alikwenda kukwapua mabilioni ya shilingi BoT hata bila kumfahamisha Rugemalira – mbia mwenzake.
“Kikwete anajua kila kitu. Yule singasinga alitokea ikulu. Huenda ndiyo maana sasa anaonekana kumtetea kwa kila jambo, likiwamo hata suala la kodi ya serikali,” ameeleza waziri mmoja mwandamizi serikalini kwa sharti la kutotajwa jina.
“Nakuambia, Kikwete hatoki katika hili. Barua ya msaidizi wake akimwandikia katibu mkuu Hazina, inadhihirisha kuwa rais anajua kila kitu na hasa alibariki kila kitu. Rais mwenyewe hajakana hilo,” ameeleza waziri huyo.
Kupatikana kwa taarifa kuwa Rais Kikwete alifahamu kila hatua kuhusu uchotaji mabilioni ya shilingi kutoka Benki Kuu (BoT), na hata yule Harbinder Sethi alitokea ikulu, kumekuja siku tatu baada ya Kikwete kudai kuwa fedha katika akaunti ya Escrow, hazikuwa za umma.
Akihutubia wanaoitwa, “Wazee wa Dar es Salaam,” katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Jumatatu wiki hii, Rais Kikwete alisema, mabilioni ya shilingi katika akaunti ya Escrow yalilipwa kwa PAP baada ya Mahakama Kuu kutoa “amri” tarehe 5 Septemba 2013,” kauli ambayo imethibitika kutokuwa kweli na sahihi.
Taarifa zinasema, kinachoitwa amri ya mahakama, kilikuwa ni kumaliza mzozo wa wanahisa wa kampuni ya kufua umeme wa dharula ya IPTL (Independent Power Tanzania Limited).
Usahihi na ukweli unapotea pale rais anaposema fedha ni mali ya IPTL huku wanaoshughulikia “fedha binafsi” kuchukuliwa ni pamoja na wasaidizi wake ikulu, mawaziri, makatibu wakuu, wabunge na gavana wa BoT.
“Mimi sina tatizo na maelezo ya rais,” anaeleza waziri mwandamizi na kuongeza, “umma unasubiri kujua huyo ‘mmoja wa wanafimilia wa Kikwete’ aliyempeleka singasinga ikulu, ni nani.
Akaunti ya Escrow ilifunguliwa ili kusubiri kumalizika kwa mgogoro kati ya Tanesco na IPTL, uliohusu madai ya udanganyifu katika uwekezaji; na hata gharama za kuweka mitambo – Capacity Charge – ambavyo vilifanywa na kampuni hiyo ya kigeni.
Kampuni ya IPTL ni muungano wa kampuni mbili – VIP Engineering and Marketing Limited ya James Rugemalira, iliyokuwa ikimiliki asilimia 30 ya hisa na MECHMAR ya Malaysia iliyokuwa na asilimia 70 za hisa.
Katika mazingira haya, wachunguzi wa mambo wanasema ya IPTL yatakuwa kama ya Richmond/Dowans. Waziri mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa aliwahi kuambia kikao cha CCM mjini Dodoma kuwa “kila kitu” alichofanya katika uwekezaji huo wa kifisadi, kilikuwa kinajulikana kwa rais.
Hapa ndipo unakuja mshangao. Kama singasinga alitokea ikulu; wasaidizi wa rais ndio waliandika barua za kuruhusu kuchota fedha BoT; na rais anajua kila kitu kilichokuwa kinatendeka; serikali inaweza kusemaje kuwa “inatafuta” kampuni ya Machmar, ambayo ndiye singasinga, ili ilipe kodi ya VAT?
Kwa waliomwona Rais Kikwete akihutubia, watakuwa waligundua kuwa sura yake, mpangilio wa maneno yake na jinsi alivyokuwa akihangaika kitini; bila shaka alikuwa akijitahidi kuficha ukweli fulani kadri inavyowezekana,” ameeleza mtumishi mmoja wa ikulu.
Miongoni mwa waliotajwa kupewa fedha na Rugemalira, kama alivyopewa Profesa Anna Tibaijuka, ni mwandani wa rais kiofisi (mnikulu), Shabani Gurumo. Hajafukuzwa kazi.
Mtu mwingine ambaye ametajwa kunufaika na fedha za Escrow zilizopitia benki ya Stanbic, na ambaye jina lake lilitajwa bungeni na mmoja wa wabunge wa upinzani, ni Albert Marwa.
Wapo wengine waliochotewa mamilioni ya shilingi kupitia kwa Rugemalira na Stanbic akiwemo mtu mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Mashimba.
Kufikia hatua hii, Prof. Muhongo yumo katika mazingira kama yale ya Lowassa. Wandani wake wamesikika wakisema kuwa wamemnukuu akisema kwamba akichukuliwa hatua, basi “ataanika kila kitu.”
MwanaHALISI Onlile, liliripoti mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa, Rais Kikwete “…amepanga kulinda watuhumiwa,” na kwamba anayetarajiwa kutoswa katika sakata hili, ni Prof. Tibaijuka tu. Ndivyo ilivyotokea.
CHANZO :MWANAHALISI ONLINE
0 comments :
Post a Comment