-->

JWTZ KUSIMAMIA ZOEZI LA UBORESHAJI WA DAFTARI LA KUDUMU

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imetaka uboreshwaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura usimamiwe na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Imesema kila wilaya nchini itakuwa na askari sita wa JWTZ ambao watashirikiana na wataalamu wanne wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kutoka Nec na kampuni inayotengeneza vifaa vya uandikishaji.
Akizungumza katika mkutano baina ya tume hiyo na wadau wake juu ya hatua iliyofikiwa katika kuboresha daftari hilo, Mkurugenzi wa Nec, Julius Malaba alisema timu hiyo itasimamia uandikishaji na kufanya matengenezo madogomadogo ya vifaa wakati wa uandikishaji iwapo yatahitajika.”
Hata hivyo, mpango huo wa kutumia JWTZ umepingwa na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wakisema unaweza kuliingiza Taifa kwenye machafuko.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa alisema kwa mpango huo, Nec inaweza kuiingiza nchi kwenye machafuko kama yaliyotokea katika nchi nyingine.
Alisema kulitumia jeshi ni sawa na kuondoa demokrasia ambayo imezoeleka kwa Watanzania na kusisitiza kuwa tangu nchi imepata uhuru, hakuna siku ambayo jeshi lilitumika kwenye masuala ya uchaguzi wala uandikishaji wa daftari la wapigakura.
“Hii mitambo ya BVR kwani ni ya kijeshi mpaka mnasema jeshi litumike kusimamia daftari hili? Tumieni busara ili demokrasia iendelee kuwapo nchini,” alisema Dk Slaa.
Mkurugenzi wa Uchaguzi Chama cha Sauti ya Umma (Sau), Johnson Mwangosi alisema tangu mwaka 1995, vyama vya siasa vilikataa jeshi kuingizwa kwenye siasa, hivyo hakuna sababu kusimamia daftari hilo wala kujihusisha na uchaguzi.
Pia aliiomba Nec kutotumia Vitambulisho vya Taifa katika mchakato huo akisema ni Watanzania wachache wenye vitambulisho hivyo.
Mwenyekiti wa ADC, Said Miraji alisema: “Kutumia jeshi kwenye uandikishaji ni sawa na kutokomeza demokrasia iliyopo nchini.”
Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Sheweji Mketo alisema: “Ni kosa kulihusisha jeshi katika hili. Haya ni matokeo ya Nec kutovishirikisha vyama vya siasa katika kuandaa taratibu za maboresho haya.”
Kaimu Katibu Mkuu wa NCCR - Mageuzi, Faustine Sungura alisema: “Kulitumia jeshi ni sawa na kuwaambia wananchi wasijitokeze kabisa kujiandikisha. Wakiwaona watashindwa kujiandikisha, watakaopiga kura watakuwa wachache.”
SOURCE;CLANSMEDIA
Share on Google Plus

About Omari Makoo

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment