-->

CAMERON AIKOSEA KWA KUHUSIKA NA MATESO

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron ameungana na viongozi wengine kukemea vikali mbinu za mateso zilizotumiwa na Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA) kwa washukiwa wa ugaidi kufuatia kuchapishwa ripoti maalum.
Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron. Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron.
Cameron amesema mateso hayo yalioonekana kufanyiwa washukiwa hao wa kundi la kigaidi la Alqaida ni makubwa kuliko yalivyodhaniwa.
"Wacha tuwe wa wazi kabisa, mateso ni makosa, kutekeleza visa vya mateso ni makosa makubwa," alisema Cameron alipokutana na waandishi habari mjini Ankara, Uturuki, ambapo alikuwa ziarani kukutana na maafisa wa nchi hiyo kujadili ushirikiano wa usalama katika kupambana na vitisho vya ugaidi kutoka kwa wanamgambo wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu (IS).
Cameron amesema yalioyoangaziwa katika ripoti hiyo ya kurasa 500 iliyotolewa na wachunguzi wa baraza la Seneti la Marekani ni uvunjifu mkubwa wa haki za binaadamu katika kupambana na ugaidi.
Obama: Tumejifunza
Mkuu wa Kamati ya Uchunguzi ya Seneti ya Marekani, Dianne Feinstein. Mkuu wa Kamati ya Uchunguzi ya Seneti ya Marekani, Dianne Feinstein.
Aidha wakosoaji wa ripoti hiyo nchini Uingereza wameitaka serikali ya Marekani kujitokeza wazi na kusema jukumu lake katika kuwasaidia maafisa wa shirika hilo la ujasusi kukabiliana na ugaidi, ambapo magaidi walipelekwa katika maeneo ya siri na kuteswa na maafisa waliowahoji.
Ripoti hiyo iliyofichua mateso hayo imesema washukiwa wengi walinyanyaswa vibaya na kwamba magereza ya siri ya CIA yaligeuka kuwa vyumba vya mateso. Ripoti hiyo imeendelea kusema kwamba mbinu hizo za kikatili hazikuchangia kwa aina yoyote ile kuifanya Marekani kuwa nchi salama zaidi baada ya mashambulizi ya Septemba 11, 2001.
Hata hivyo, Rais Barrcak Obama amesema umuhimu wa kutolewa kwa ripoti hii ni nchi hiyo kujifunza kutokana na yaliyotokea na watu kuelewa ni kwa nini alipiga marufuku masuala kama haya kama hatua ya kwanza wakati akiingia madarakani.
Korea Kaskazini yaja juu
Kiongozi wa Korea ya Kaskazini, Kim Jong Un. Kiongozi wa Korea ya Kaskazini, Kim Jong Un.
Kwa upande mwengine, Korea ya Kaskazini ambayo imekuwa ikilaumiwa mara kwa mara na Marekani kufuatia uvunjifu wa haki za binaadamu, nayo imepaza sauti kuhusu ripoti hii kwa kulihimiza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kulaani mateso yaliyofanywa na Marekani kwa washukiwa wa ugaidi.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kaskazini amesema ripoti hii ni mtihani mkubwa sana wa kupima uaminifu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Msemaji huyo amesema, kwa kuzungumzia rikodi ya masuala ya haki za binaadamu ya Korea ya Kaskazini na kufumbia macho mambo yaliyobainika kufanywa na mwanachama wake wa kudumu ambaye ni Marekani, kutaonesha wazi kwamba Baraza hilo lipo tu na halina makali yoyote.
Huku hayo yakiarifiwa, China imeitaka Marekani kurekebisha mienendo yake baada ya baraza la Seneti kusema katika ripoti yake kwamba CIA iliipotosha ikulu ya Marekani pamoja na umma juu ya mateso kwa washukiwa wa ugaidi.
Hata hivyo, shirika hilo la kijasusi limekanusha madai ya ripoti hiyo.
Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters/AFP
Mhariri: Saumu Yusuf
SOURCE:DW SWAHILI
Share on Google Plus

About Omari Makoo

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment