-->

PROFESA MUHONGO BADO YU TAABUNI KWA SAKATA LA ESCROW


Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo 
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, anazidi kuandamwa na kashfa baada ya siri kufichuka kuwa katika uongozi wake hakuna kipya alichofanya zaidi ya kutekeleza miradi na mipango iliyobuniwa na watangulizi wake.

Taarifa za kiuchunguzi kutoka vyanzo mbalimbali na ndani ya Wizara hiyo, zimebaini kuwa sifa anazojipa katika kujinasua na sakata la Escrow, zimejaa propaganda kwa ajili ya kuwadangaya wananchi.

Taarifa za uhakika kutoka vyanzo hivyo, zinaeleza tangu aingie madarakani Mei 2012 baada ya Rais Jakaya Kikwete kufanya mabadiliko Baraza la Mawaziri, hajawahi kubuni kitu kipya kikubwa ambacho kinalenga kuwasaidia Watanzania.

Taarifa zinaonyesha kuwa miradi na mipango yote anayopigiwa debe ilianzishwa kabla ya kuingia madarakani na mingine ilikuwa imeanza kufanya kazi kwa ufanisi.

MGAWO WA UMEME
Moja ya eneo ambalo Profesa Muhongo, anatamba kufanikiwa ni kero ya mgawo wa umeme.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, katika kuhakikisha mgawo huo unadhibitiwa, Rais Jakaya Kikwete aliagiza zitolewe Sh. bilioni 2.4 kila siku kusaidia Shirika la Umeme nchini (Tanesco) kununulia mafuta mazito ya kuendeshea mitambo ya kufulia umeme nchini.

Utaratibu huo ulianza kutekelezwa miezi saba kabla ya kuingia madarakani, ambapo wakati huo William Ngeleja, Mbunge wa Sengerema alikuwa akiongoza wizara.

Chanzo cha habari kinaeleza pesa hizo zinatolewa nje ya bajeti ya serikali na kufanya wizara hiyo kupokea zaidi ya Sh. bilioni 70 kwa mwezi, kitu ambacho kimesababisha baadhi ya wizara kushindwa kufanya kazi kikamilifu kutokana na ukosefu wa pesa.

“Waziri Muhongo ni bingwa wa propaganda anaposema amedhibiti mgawo wa umeme siyo kweli, serikali iliamua kusaidia jambo hili kwa kutoa pesa nyingi, hata angekuwa nani angefanikisha labda aseme lingine,” kilisema chanzo hicho.

Kumbukumbu za wizara zinaonyesha utoaji wa fedha hizo pamoja na Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini.

“Sisi kama wabunge tumeziona fedha hizo, tumeamua kukaa kimya kutokana na kutumika katika jambo muhimu katika uchumi wa nchi, lakini inaleta athari kubwa kutokana na miradi mingi katika wizara mbalimbali kushindwa kuendelezwa baada ya pesa nyingi kupelekwa huko nje ya bajeti,” kilidai chanzo chetu.

UMEME VIJIJINI
Suala lingine ambalo Profesa Muhongo anadaiwa kudanganya ni kwamba amefanikiwa kusambaza umeme katika vijiji vingi pamoja na kupunguza malipo ya kuunganisha hadi kufikia Sh. 29,000.

Taarifa zinaonyesha mpango kabambe wa umeme vijijini unaosimamia na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) ulianza mwaka 2009 na kuimarika mwaka 2012 chini ya uongozi wa Ngeleja.

Fedha za kutekeleza miradi hiyo imetolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) na mfuko wa Marekani wa changamoto za Melenia (MCC) na serikali.

“Wakati REA inasambaza umeme tulikuwa na kigugumizi namna ya watu wa vijijini watakavyomudu kupata huduma hiyo, tukaamua kuanzisha majaribio ya kupunguza malipo ya kuunganisha kwa wilaya mbili,” alisema mtaalamu mmoja kutoka wizarani hapo.

Mpango huo ulifanyiwa majaribio mwaka 2010 na 2011 katika Wilaya za Kilombelo na Mbozi na kuonyesha mafanikio.

“Mpango ulipoonekana unawezekana kuutekeleza ulianza kusambazwa katika mikoa ya Kusini, hivyo hakuna ukweli kwamba yeye ameanzisha,” kilisema chanzo hicho.

MTAMBO WA KINYEREZI
Uchunguzi huo umebaini hata mkakati wa kuanzisha miradi mikubwa ya usafirishaji na kufua umeme ilianzishwa enzi ya Ngeleja, ukiwamo wa ujenzi wa mitambo ya kufua umeme kwa kutumia gesi eneo la Kinyerezi, uzalishaji umeme maporomoko ya Rusumo, usafirishaji wa umeme wa pamoja kati ya nchi za Kenya, Zambia, Burundi na Rwanda.

MFUKO WA MADINI
Katika hatua nyingine, imedaiwa Waziri Muhongo, hakuhusika katika kuubuni mfuko wa kusaidia wachimbaji wadogo kama inavyodaiwa.

Mfuko huo ulioanzishwa mwaka 2011 ulianza kufanyakazi kwa kusaidia wachimbaji wadogo kwa kuwakopesha mitaji na vifaa vya uchimbaji wa madini.

“Kwa kutumia uungwana, Waziri Muhongo wakati anajisifu kufanya mambo hayo angewataja kwa kuwashukuru waliomtangulia kwa kubuni mipango na miradi hiyo, kuliko kujigamba kwa kitu ambacho binafsi hajahusika nacho,” kilidai chanzo hicho. CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
Share on Google Plus

About Omari Makoo

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment