Chenge na Ngeleja |
Wenyeviti watatu wa
Kamati za Bunge waliopendekezwa kuwajibishwa na Bunge hilo katika sakata
la Akaunti ya Tegeta Escrow wataondolewa katika nyadhifa zao ndani ya
siku 21 zijazo, imeelezwa.
Naibu Spika wa Bunge,
Job Ndugai alisema jana kuwa utekelezaji wa maazimio ya Bunge kwa
upande wa mhimili huo wa dola utafanyiwa kazi mapema mwakani.
“Hilo litatekelezwa
wakati wa Kamati za Bunge ambazo zitaanza mwishoni mwa wiki ya pili ya
Januari mwakani kwa kamati husika kuchagua wenyeviti wapya.”
Wenyeviti hao ni wa
Kamati ya Nishati na Madini, Victor Mwambalaswa, William Ngeleja wa
Katiba, Sheria na Utawala na Andrew Chenge wa Kamati ya Bajeti.
Tuhuma zao
Chenge ambaye pia ni
Mbunge wa Bariadi (CCM) alitajwa katika ripoti ya Kamati ya Bunge ya
Hesabu za Serikali (PAC) kuwa aliwekewa Sh1.6 bilioni katika akaunti
yake binafsi kama ilivyokuwa kwa Ngejela (Sengerema -CCM) ambaye
aliingiziwa Sh40.4 milioni. Wote waliingiziwa fedha hizo na mmiliki wa
Kampuni ya VIP Engineering & Marketing, James Rugemalira.
Mwambalaswa, ambaye
pia ni Mbunge wa Lupa (CCM), ametajwa kwa kuwa alikuwa makamu mwenyekiti
wa Bodi ya Tanesco ambayo Bunge liliazimia kuwa wajumbe wake
wawajibishwe.
Katika azimio namba
tatu, Bunge lilielekeza kuwa kamati husika za kudumu za Bunge zichukue
hatua za haraka na kwa vyovyote vile kabla ya Mkutano wa 18 wa Bunge,
kuwavua nyadhifa zao wenyeviti tajwa wa kamati husika za kudumu za
Bunge.
Utekelezaji wa azimio hilo unakuja baada ya Serikali kuanza kuwawajibisha vigogo wake waliotajwa katika ripoti hiyo.
Jumatatu iliyopita,
Rais Jakaya Kikwete alimfukuza kazi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ambaye kama ilivyokuwa kwa
Chenge na Ngeleja, aliingiziwa Sh1.6 bilioni katika akaunti yake binafsi
kinyume na kanuni za maadili ya viongozi wa umma.
Pia, wakati Rais
Kikwete akimuweka kiporo Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo, juzi Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alimsimamisha
kazi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakimu Maswi kupisha
uchunguzi wa tuhuma dhidi yake.
Hao wote
walitanguliwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema
ambaye alijiuzulu kutokana na kashfa hiyo akisema ushauri wake
haukueleweka hivyo kuchafua hali ya hewa.
0 comments :
Post a Comment