-->

CCM NA CHADEMA WAWASHIANA MOTO BALAA KWENYE UCHAGUZI WA WENYEVITI WA MITAA


Zikiwa zimebaki siku tano kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa Serikali za mitaa nchini, Katibu wa Kata ya Kisutu, Dar es Salaam wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Sauda Addy na Mjumbe wa Kamati ya Udhamini ya Chama Cha Demekrasia na Maendeleo (Chadema), Muslim Hassan, wamepigana.


Sababu za kupigana kwao zinatokana na Hassan kuchana bango la mgombea wa CCM wa nafasi ya Uenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kisutu ambalo lilibandikwa katika ofisi yake ambayo ni jengo la Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).


Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, katika ofisi ya Makao Makuu ya Polisi mkoa, walisema tukio hilo lilitokea Desemba 6 wakati Sauda alipofika katika ofisi ya Hassan kumshutumu kutokana na kitendo cha kuchana bango hilo.


Hassan, alisema siku ya tukio Sauda alifika ofisini hapo na kuanza kumshambulia kwa maneno na kipigo, hivyo watu kuingilia kati ili kuamulia vurugu hizo hali iliyosababisha akapoteza vitu vyake ikiwamo, miwani, nyaraka za ofisi na kuharibu samani za ofisi.


Sauda alisema siku ya tukio alimfuata Hassan ili kuhoji sababu za kuchana bango walilokuwa wamebandika, lakini cha kushangaza alimkunja nguo yake ya juu na kukata kifungo hali iliyomlazimu kwenda kituo cha polisi kuripoti.


Wote waliripoti katika kituo kidogo cha Polisi Kisutu na kutakiwa kuripoti kituo kikubwa cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, kwa madai kuwa kituo hicho hakipokei kesi za siasa, jana walihojiwa na kutakiwa wasubiri upelelezi utakapokamilika ndipo wataitwa tena.


Akizungumza na Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Ilala, David Mnyambuga, alisema suala hilo halijafika kwake na kwamba ataanza kulishughulia mara baada ya kupata maelezo ya walalamikaji hao, ambao aliwaita ofisini kwake kwa mahojiano.
SOURCE:CHALIIZEE
Share on Google Plus

About Omari Makoo

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment