Dar es
Salaam. Kocha Marcio Maximo amesema hana kinyongo na uamuzi wa uongozi
wa Yanga kumuondoa, ingawa umefuta ghafla mkakati wa kutaka klabu hiyo
iendeshwa kwa weledi.
Maximo na
msaidizi wake Leonard Neiva walisitishiwa mikataba yao baada ya Yanga
kufungwa na Simba 2-0 katika mchezo wa Nani Mtani Jembe mwezi huu, ikiwa
ni takriban miezi mitano tangu aje nchini.
Akizungumza
muda mfupi kabla ya kupanda ndege kurudi kwao Brazil jana, Maximo
alisema hana kinyongo na uamuzi huo, lakini akaitaka klabu hiyo kongwe
kuendeleza soka la vijana na kutengeneza mindombinu kama inataka kupata
mafanikio makubwa katika soka.
Alisema
katika muda mfupi aliokuwa klabu hiyo, alijenga misingi ya utendaji kazi
wa kisasa ndani na nje ya uwanja kwa wachezaji ili waweze kujitambua
katika kazi yao, lakini jambo hilo limeishia njiani.
"Katika
miezi sita niliyokuwa na timu, nilijaribu kujenga weledi ndani na nje ya
uwanja, tulifanya kazi kubwa ya kujaribu kutengeneza miundombinu,
lakini tulishindwa kuwashawishi viongozi wote," alisema Maximo ambaye
timu yake ililazimika kuhama viwanja kwa ajili ya mazoezi kutokana na
Uwanja wa Kaunda kuwa katika hali mbaya.
Yanga
bado inapambana na mamlaka za jiji ikidai iongezewe eneo ili ijenge
uwanja wa kisasa, maombi ambayo yamekataliwa na hivyo timu kulazimika
kukodi viwanja tofauti kwa ajili ya mazoezi.
"Hii
inatokana na ukweli kuwa baadhi ya viongozi hawakupenda yale tuliyokuwa
tunayafanya. Labda sisi hatukuwa makocha wa aina yao ndio maana
walichukua uamuzi waliouchukua. Hatuna kinyongo hata kidogo. Tutakuwa
sehemu ya timu hiyo na pale watakapotaka ushauri wetu tutakuwa tayari
kutoa," alisema kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa.
Alisema uamuzi uliochukuliwa ni kawaida kwa kuwa ni sehemu ya changamoto katika maisha ya ukocha pamoja.
"Ili
kupata kazi ya ukocha, lazima kutakuwa na tukio la kufukuza kocha.
Kuondoka kwetu sisi kuna watu wengine wameingia. Maisha bado
yanaendelea. Si ajabu kwani kuna ushahidi kuwa baadhi ya makocha
walikatishiwa mikataba yao na kurejea tena katika timu hiyo hiyo, kama
ilivyotokea kwa Jose Mourinho, aliondoka Chelsea na kurejea tena
kutokana na uongozi kutambua kile alichokuwa anakifanya kabla
hajasitishiwa mkataba wake," alisema.
Maximo anaondoka akiwa ameiacha Yanga katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu.CHANZO.MWANANCHI
0 comments :
Post a Comment