VIJANA wajulikanao kama panya road wameendelea kukamatwa, ambapo Mkoa
wa Kipolisi wa Ilala umewakamata watu 114 kwa makosa mbalimbali ya
kihalifu, wakati wa operesheni kuwakamata vijana hao.
Akizungumza Dar es Salaam jana na Jambo Leo, Kamanda wa Polisi Mkoa
wa kipolisi Ilala, Mary Nzuki, alisema vijana hao walikamatwa na makosa
mbalimbali, wakati wa operesheni inayoendelea jijini Dar es Salaam, kwa
ajili ya kupambana na vijana wanaojihusisha na uhalifu.
Alisema kuanzia jana (juzi) hadi kufikia leo(jana), jeshi hilo
lilifanikiwa kukamata vijana hao kwenye maeneo mbalimbali ambayo ni
kwenye vijiwe ambavyo huvitumia kuvutia madawa ya kulevya (vichochezi
vya uhalifu), gongo, mirungi na kwenye vituo vya daladala.
Alisema vijana hao walikamatwa wakiwa na vitu mbalimbali ambavyo ni
bangi, gongo, mirungi na kubainisha kuwa, vijana walikamatwa katika
maeneo ya Posta Mpya, Mnazi Mmoja, Feri na maeneo mengine na hawakuwa na
aina yoyote ya silaha.
Aliongeza kuwa, kwa sasa jeshi hilo limejipanga kukabiliana na vijana
hao na kubainisha kuwa, ulinzi umeimarishwa maeneo yote katika mkoa
wake wa kipolisi.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa kipolisi Temeke, Kihenya wa
Kihenya alisema katika eneo lake ulinzi umeimarishwa na kwamba
oparesheni kali inafanyika mchana na usiku.
“Msako mkali utafanyika katika meneo yote, nyumba hadi nyumba ili
kuhakikisha tunawatia nguvuni vijana wanaojihusisha na mambo ya
kihalifu,” alisema.
Alisema ulinzi katika maeneo yote umaimarishwa na msako mkali unaendelea.
Naye, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura alisema
katika mkoa wake wa kipolisi, oparesheni hiyo itaendelea na kubainisha
kuwa, imekuwa na mafaniko makubwa katika kupambana na uhalifu.
Alisema wakati wa oparesheni hiyo katika mkoa wake, hakuna
aliyekamatwa na kwamba, jeshi hilo limejipanda kuimarisha ulinzi na hali
ya amani katika eneo hilo.
“Kwa kuwa, ni majukumu yetu ya kusimamia na kukabiliana na uhalifu, hivyo niwahakikishie ulinzi upo wa kutosha,” alisema.
Alisema kuwa, awali wakati wa operesheni ya kuwakamata vijana hao
jeshi hilo katika mkoa huo wa kipolisi, lilifanikiwa kukamata vijana 226
na kwamba, huo si mwisho bali oparesheni hiyo itakuwa endelevu.
=> Jambo Leo
0 comments :
Post a Comment