-->

WANASAYANSI WAGUNDUA NAMNA YA KUPATA MAJI SAFI YA KUNYWA KWA KUTUMIA KINYESI CHA BINAADAM

KINYESHI cha binadamu hutumika sana kama mbolea katika bustani na mashambani, lakini kwa teknolojia mpya sasa kitaweza kuchujwa na kutoa maji safi na salama ya kunywa. Teknolojia hiyo mpya inatarajiwa kuzisaidia nchi nyingi hasa zinazoendelea zenye matatizo makubwa ya upatikanaji wa maji safi na salama pamoja kutokana na na kuwa na vyanzo vichache vya maji vya kuweza kutosheleza mahitaji.
Bill Gates kupitia kampuni yake ya Bill and Melinda Gates Foundation ameliona hili na ameamua kutafuta ufumbuzi.
Kwa kuwatumia wanasayansi, Gates amefadhili mradi uliokuja na teknolojia kama  ufumbuzi wa tatizo hilo.
Teknolojia hii ni ya mashine inayochakata na kuchuja maji taka (machafu ya chooni) na kugeuza kuwa maji safi na salama. Mtambo unaochakacha kinyesi umepewa jina la OmniProcesssor na umetengenezwa na kampuni ya Uhandisi iliyopo Seattle, Marekani inayoitwa Janicki Bioenergy.
Mradi huo ulikamilika kwa mafanikio, na hivi karibuni Gates alizindua rasmi mtambo huo kwa kunywa yaliyotengenezwa kutokana na kinyesi cha binadamu.
Picha ikionyesha gramu 1000 za maji taka (Kinyesi cha binadamu, Mkojo na Majimaji) zikichakachwa zinaweza kutoa Maji gramu 800 na uchafu wa kinyesi gramu 200.
Picha ikionyesha gramu 1000 za maji taka (Kinyesi cha binadamu, Mkojo na Majimaji) zikichakachwa zinaweza kutoa Maji gramu 800 na uchafu wa kinyesi gramu 200.
“Maji yalikuwa mazuri kana kwamba nakunywa kutoka kwenye chupa za maji ya kawaida  tuliyoyazoea.  Baada ya kusoma ufundi unaotumika kuyaandaa maji hayo sikuwa na wasiwasi kuyanywa,” Gates alisema.
Teknolojia hii siyo tu itazalisha maji ya kunywa bali pia itaboresha mfumo wa maji taka kwenye nchi zinazoendelea. Mtambo huu utasaidia sana kudhibiti maji taka yanayochafua vyanzo vingine vya maji hasa katika nchi zinazoendelea na kusababisha magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu, kuhara na kuhara damu.
Licha ya faida hizo, mtambo huo unatarajiwa kuwa chanzo cha mapato kwa wajasiriamali watakaokuwa wanaleta maji taka yatakayoingizwa kwenye mashine hiyo, lakini pia mtambo huu utakuwa unazalisha umeme kwa matumizi mengine.
Gates alisema OmniProcessor ilivyobuniwa itakuwa ya gharama ndogo kuinunua na kuitunza na ni ndoto yake teknolojia hii itatumika dunia nzima na hivyo kusaidia kipato kwa wajasiriamali.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya la Dunia (WHO), watu 1.8 bilioni duniani wanatumia maji ya kunywa yaliyochafuliwa na kinyesi cha binadamu.
Utafiti uliofanyika Tanzania mwaka 2009 na mashirika ya SNV, Water AID na UNICEF katika wilaya 16 nchini, asilimi 46 ya Watanzania wanakosa maji safi na salama, huku asilimia 87 ya Watanzania hawatumii mifumo ya maji taka kwenye nyumba zao.
OmniProcessor itakuwa na nafasi kubwa kwa nchi za Afrika kutatua tatizo la ukosefu wa maji safi na salama, lakini pia itaboresha mifumo ya maji taka na hii itawezesha upatikanaji wa malighafi ya mashine hizo kuweza kuchakata maji taka ili kupata maji ya kunywa.
Kuna idadi ya kushtua ya watu bilioni mbili duniani inayotumia vyoo visivyo tapishwa kwa mujibu wa kanuni za afya. Wengine wanajisaidia haja kubwa ardhini, Watanzania wapatao asilimi 16 walibainika kujisaidia nje ya nyumba zao bila ya kutumia vyoo, kwa mujibu wa utafiti huo.
Nyumba nyingi hasa katika Mkoa wa Dar es Salaam watu wana tabia ya kutapisha vyoo vyao, msimu wa masika mvua zinaponyesha na hivyo kuwa chanzo cha kuchafua maji na mazingira.
Gates alisema kwamba hali ya uchafu kwenye nchi zinazoendelea inachangia vifo 700,000 vya watoto kwa mwaka. Maji yasiyokuwa salama yanazuia watoto walioepuka vifo kutokana na maji yasiyo salama  kushindwa kukua vizuri kiakili na kimwili.
“Kama tutaweza kuwa na miundombinu salama na ya bei rahisi, itakayowezesha  kutumia na kuhifadhi maji taka, tutaweza kuzuia vifo hivyo na kusaidia watoto kukua vizuri na kuwa na afya njema,…..mashine zitageuza uchafu kuwa hazina,” Gates aliandika kwenye blogu yake.
OminProcessor inavyofanya kazi
Mashine hii ni ya aina yake na ni tofauti na nyingine zinazotumika nchi za magharibi katika uchakataji wa maji taka ili yaweze kutumika kwa matumizi mengine.
Mashine zilizopo zina gharama kubwa ya uendeshaji na uchakataji unatumia muda mrefu. Tofauti na mashine hizo, OmniProcessor zikishatenganisha maji na kinyesi, maji hayo yanamwagwa ardhini ambako yanaweza kuchujwa zaidi kwa matumizi ya kilimo na kadhalika tofauti na OmniProcessor inayotenegenza maji safi na salama.
Urojo wa mavi huchukuliwa kwa mkanda mpaka juu ya eneo ambalo maji taka haya huchemshwa. Maji hutoka baada ya kuchemshwa na hutoka kwa njia ya mvuke na katika joto hili wadudu wote wanakuwa wameuliwa.
Mabaki ya kinyesi huchukuliwa mpaka sehemu ya tanuri ambako huchomwa na kutoa mvuke, na ni mvuke huu unaorudishwa kwenye mashine ili kuendesha jenereta litumialo mvuke ili kuzalisha  nguvu zinazoendesha mtambo na pia jenereta hii inazalisha umeme kwa ajili ya matumizi mengine.
Hapo mvuke unapelekwa kwenye mfumo wa uchujaji kwa kutumia chujio nyingi tofauti ili kuhakikisha maji safi baada ya kuondoa chembechembe zisizohitajika.
Baadaye maji haya yanapelekwa sehemu nyingine na kupimwa kama yana viwango vya alkali inayohitajika. Baada ya hapo maji yanakuwa tayari kwa kunywewa.
Kampuni ya Janicki Bioenerg inaendelea na utafiti wake wa kutengeneza mashine nyingine (Model S100) kama uthibitisho wa wazo la awali kwa kutengeneza mashine itakayopelekwa huko Senegal.
Hii itakuwa ndogo na itakuwa na uwezo wa kutengeneza lita 10,800 za maji na umeme wa Kilowati 150. Umeme unaozalishwa hapa ni mkubwa na unaweza kutumika kwenye nyumba zaidi ya 10.
Mashine ya kwanza  (Model S200) ina uwezo mkubwa zaidi wa kuchakata maji taka kutoka kwa watu 100,000 na itazalisha maji safi na salama lita 86,000 kwa siku na umeme wa kilowati 300.
Share on Google Plus

About Omari Makoo

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment