HATIMAYE yametimia. Alliance for Change and Transparency (ACT-Tanzania), chama kipya cha siasa nchini na ambacho kilitarajiwa kuongozwa na Zitto Zuberi Kabwe, mbunge wa Kigoma Kaskazini, kimemfungulia kesi Samson Mwigamba na genge lake. Anaandika Saed Kubenea.
Kesi hiyo imefunguliwa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam na Lucas Kadavi Limbu, mmoja wa waasisi na mwenyekiti wa taifa wa chama hicho na wenzake watano.
Viongozi wengine wa ACT walioungana na Limbu kumfungulia kesi Mwigamba, aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho na ambaye amefukuzwa uwanachama, ni Leopald Mahona, naibu katibu mkuu (Bara) na Grason Nyakarungu, katibu mwenezi na mwenyekiti wa vijana taifa.
Wengine walifungua kesi hiyo, ni Ramadhani Suleiman, makamu mwenyekiti (Zanzibar) na mwenyekiti wa ngome ya wanawake, Dotto Chacha Wangwe. Kesi hiyo ni Na. 1 ya mwaka 2015.
Katika hati ya kiapo kilichowasilishwa mahakamani, Limbu, Nyakarungu, Mahona, Ramadhani na Wangwe, wanadai kuwa Mwigamba na Prof. Kitila, mshauri mkuu wa chama hicho, wamefanya mapinduzi ndani ya chama kinyume na katiba ya ACT.
Prof. Kitila aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu (CC), ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alifukuzwa uanachama mwaka mmoja uliopita; ndipo akajiunga na ACT-Tanzania.
Alituhumiwa kushiriki njama za kuhujumu chama na kuandaa mipango isiyo halali ya kubadilisha uongozi Chadema. Alikiri kushiriki njama.
Katika ACT, Prof. Kitila anakabiliwa na tuhuma zilezile. Naye Mwigamba ambaye alikuwa mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Arusha, alifukuzwa kwa madai ya “kuhujumu chama, usaliti, kukashifu viongozi wakuu wa chama na uchonganishi.”
Katika chama kipya sasa, Mwigamba na Prof. Kitila wanatuhumiwa makosa yaleyale na hasa kile kinachoitwa “kutaka kuleta mapinduzi ili Zitto Kabwe, ambaye pia alifukuzwa Chadema, aweze kuwa mwenyekiti wa ACT-Tanzania.”
SOURCE:MWANAHALISIONLINE
0 comments :
Post a Comment