-->

MAKALA MAALUMU YA NELSON MANDELA KUHUSU MAISHA YA JELA NA MAFUNZO ALIYOYAPATA


Nelson Mandela (kulia) akiwa na Rais mstaafu wa Marekani, Bill Clinton alipotembelea kilichokuwa chumba chake katika jela ya Kisiwa cha Robben, Picha ya Mtandao.
 
JUNI 12, 1964, Nelson Mandela alihukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kufanya hujuma dhidi ya Serikali ya kibaguzi ya Makaburu.


Hata hivyo Mandela alitumikia kifungo hicho kwa miaka 27 na kutoka akiwa mtu aliyebadilika kitabia, akiwa mtulivu, akiwa na hekima, mwenye busara na mwenye kuheshimika katika jamii.

Mandela alianza kutumikia kifungo katika jela iliyopo kwenye kisiwa cha Robben kilichopo kwenye bahari ya Atlantic umbali wa kilometa 12 kutoka mji wa Cape Town, alimotumikia kifungo kwa miaka 18, na mwaka 1982 aliondolewa ndani ya kisiwa hicho na kuhamishiwa kwenye gereza pia lenye ulinzi mkali la Pollsmoor lililopo Cape Town na siku chache kabla ya kuachiwa huru alihamishiwa gereza lililopo mjini Cape Town la Victor Verster.

Kisiwa cha Robben kwa takriban miaka 400 iliyopita kimekuwa kikitumika kama eneo la kuadhibu watu, kuweka watu katika maisha ya kuwatenga na kuwafunga jela. Ni kisiwa kwa ajili ya watu wasumbufu wa kisiasa, wasumbufu katika jamii na watu wasiotakiwa katika jamii.

Kama ilivyo kwa viongozi na wanaharakati wengine wa ukombozi wa kiafrika waliopata changamoto za Serikali za kikoloni kwa kukamatwa, ambao baadaye walikuja kushika uongozi wa nchi zao, kama vile Kwame Nkrumah wa Ghana, Jomo Kenyatta wa Kenya na Robert Mugabe wa Zimbabwe, Mandela naye alipotoka jela alikuwa Rais wa kwanza mweusi nchini Afrika Kusini.

Gereza la Kisiwa cha Robben, lililofahamika kwa jina la gereza ndani ya gereza, lilikuwa ni gereza lenye zahama na ukiwa. 


Kufungwa ndani ya gereza hilo maana yake ni muda mwingi kufanya kazi za suluba, lakini kulikuwa na fursa kwa mfungwa kupata muda wa kujisomea, kufanya mijadala na kujipima. 


Miongoni mwa masharti ya kushikilia maadili ndani ya gereza hilo ni kwa wafungwa kujikita kwenye kusoma na kufanya mijadala. Tabia ya Mandela na uongozi wenye weledi ni matokeo ya maisha ya jela au ‘Chuo Kikuu cha Kisiwa cha Robben.’

“Hakuna zaidi ya kuelekeza akili zako kwa kuwa mtulivu zaidi kwa kukubali ukweli wa jamii yako,” alisema Mandela. 


Mwanzoni mwa mwaka 1972, alipewa ofa ya kutoka jela kwa sharti la kutangaza kukomesha vurugu dhidi ya Serikali ya Makaburu, ofa mabayo aliikataa akisema kuwa Serikali ndiyo imekifanya chama cha ANC kutumia njia ya uanaharakati.

Maisha ya jela ndiyo yaliyombadili Mandela na kuwa kiongozi mwenye ushawishi, ambapo akiwa gerezani alijifunza kuhusu hisia za binadamu na namna ya kuondoa hofu na mambo yasiyo ya usalama kwa wengine. 


Akiwa gerezani Mandela aliwavutia askari magereza kwa namna alivyokuwa mtetezi wa haki, mweye heshima na mwenye uelewa wa masuala ya kisheria, ambapo ndani ya gereza la Kisiwa cha Robben alikuwa kiongozi wa wafungwa wenzake.

Kwa mujibu wa taarifa askari magereza walikuwa chini ya uongozi wa wafungwa na wafungwa walikuwa chini ya uongozi wa Mandela.

Mwandishi wa habari Eddie Koch aliandika kwenye magazeti ya Mail na Guardian kuwa selo namba saba alimokuwa akiishi Mandela, lilikuwa eneo lenye harakati nyingi za ulinzi mkali ndani ya gereza hilo kwa kila Jumamosi ya wiki.

Wakati Mandela akiwa ndani ya gereza hilo kulikuwa na mikwaruzano ya wafungwa, kutoka kitengo cha kijeshi cha ANC, chama cha Pan Africanist Congress na wanaharakati wa Steve Biko’s Black. Vurugu ndani ya gereza hilo zilifanyika kwa misingi ya kupingana watu binafsi na tofauti ya itikadi, ambapo vurugu hizo zilikuwa kipimo cha mbinu za uongozi wa kidiplomasia wa Mandela na wenzake.

Taarifa zilisema wafungwa wengi wapya walipelekwa kwenye gereza hilo la Kisiwa cha Robben, kama vile viongozi wa wanafunzi wa Soweto, wawakilishi wa baraza waliochochea vijana hadi wakaazisha vurugu nchini humo mwaka 1976, hawakuwa na ufahamu kuhusu hali ya kisiasa ndani ya gereza hilo. MWANANCHI
Share on Google Plus

About Omari Makoo

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment