Mshambuliaji wa Simba SC, Emmanuel Okwi akiwatoka mabeki wa Yanga SC, Kevin Yondan aliyelala chini na Juma Abdul
Na BIN ZUBERY
SIMBA SC imeendeleza ubabe wake kwa mahasimu wao, Yanga SC katika
mechi za Nani Mtani Jembe, baada ya jioni hii kuichapa mabao 2-0 Uwanja
wa Taifa, Dar es Salaam.
Desemba mwaka jana, Simba iliichapa Yanga SC mabao 3-1 katika mechi
ya Mtani Jembe, inayoandaliwa na wadhamini wa timu hizo, Kampuni ya Bia
Tanzania (TBL) kupitia bia ya Kilimanjaro.
Katika mchezo wa leo, hadi mapumziko, Simba SC ilikuwa tayari
inaongoza kwa mabao hayo mawili, yaliyotiwa kimiani na kiungo Awadh Juma
na mshambuliaji Elias Maguri.
Elias Maguri aliifungia Simba SC bao la pili dakika ya 42 akimalizia
mpira uliorudi baada ya kugonga mwamba kufuatia shuti la Mganda, Simon
Sserunkuma.
Kiungo wa Yanga SC, Mnyarwanda Mbuyu Twite aliumia dakika ya 39 na
kutoka nje, nafasi yake ikichukuliwa na Hassan Dilunga. Mshambuliaji
mpya Yanga SC, Mliberia Kpah Sherman alionyesha ni machachari, lakini
hakupata ushirikiano mzuri pale mbele.
Refa Jonesia Rukyaa kutoka Bukoba mkoani Kagera, pamoja na kwamba ni
mwanamke, lakini alijitahidi kuumudu mchezo huo kadiri ya uwezo wake.
Mashabiki wa Yanga SC walianza kuondoka uwanjani mapema tu baada ya
bao pili, huku wengine wakivamia chumba cha kubadilishia nguo wachezaji.
Kipindi cha pili, kocha wa Simba SC, Mzambia Patrick Phiri alianza na
mabadiliko, akimuingiza Nahodha Joseph Owino kwenda kuchukua nafasi ya
Juuko Murushid, wakati kocha Mbrazil wa Yanga SC, alimuingiza Salum
Telela kwenda kuchukua nafasi ya Emerson na Danny Mrwanda kumrithi
Andrey Coutinho.
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Ivo Mapunda, Nassor Masoud ‘Chollo’,
Mohammed Hussein ‘Tshabalala’/Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ dk66, Hassan
Isihaka, Juuko Murushid/Joseph Owino dk47, Jonas Mkude, Ramadhani
Singano ‘Messi’/Said Ndemla dk74, Awadh Juma, Elias Maguri/Dan
Sserunkuma dk84, Simon Sserunkuma/Shaaban Kisiga ‘Malone’ dk84 na
Emmanuel Okwi.
Yanga SC; Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Abdul/Hussein Javu dk79,
Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Mbuyu Twite/Hassan
Dilunga dk39, Emerson Roque/Salum Telela dk55, Haruna Niyonzima, Kpah
Sherman/Mrisho Ngassa dk63, Simon Msuva na Andrey Coutinho/Danny Mrwanda
dk46.
13 Dec 2014
0 comments :
Post a Comment