Joshua Kuney (kushoto) na mpambe wake, Yona Lazaro, wakimwagiwa maziwa na wazee wa kimila (Malaigwanan), kama ishara ya kusimikwa kuwa kiongozi wa kijamii, muda mfupi baada ya wananchi kumtawaza kuwa Mwenyekiti wa kijiji cha Kambi ya Chokaa badala ya Mbuki Mollel aliyepitishwa na CCM na kupita bila kupingwa katika uchaguzi wa Serikali za mitaa uliyofanyika jana. Picha na Peter Saramba.
Dar/ mikoani. Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika jana nchini, ulitawaliwa na vituko katika sehemu nyingi, lakini kikubwa ni kile kilichotokea katika Kijiji cha Kambi ya Chokaa, Wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara baada ya wananchi kumweka madarakani na kumwingiza ofisini Joshua Kuney (CCM) kuwa mwenyekiti wa kijiji hicho, badala ya Mbuki Mollel aliyeteuliwa na chama hicho kuwania nafasi hiyo.
Pamoja na hatua hiyo, wananchi hao pia waliwapitisha kwa kauli moja bila kupiga kura wajumbe wote wa serikali ya kijiji kupitia CCM kutokana na kijiji hicho kutokuwa na wagombea kutoka vyama vya upinzani.
Kabla ya kumpeleka ofisi ya kijiji na kumsimika kuwa mwenyekiti, wananchi hao walimzungusha Kuney kwa maandamano ya amani wakiwa wamembeba juujuu na kuhitimisha kwa kumbariki kwa mila za Kimasai kwa kumwagia maziwa mwili mzima, ikiwa ni ishara ya baraka.
Tukio hilo linakwenda kinyume na uamuzi wa vikao vya CCM wilaya ya Simanjiro ambavyo vilimwengua Kuney ambaye alikuwa ameshinda kwa kura 335 dhidi ya 215 za Mollel wakati wa kura za maoni.
Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Letee Sailepu ambaye hakugombea tena nafasi hiyo, alisema wakazi wa kijiji hicho hawako tayari kuongozwa na mtu wasiyemtaka.
“Mwenyekiti wa kijiji ni kiongozi wa watu anayestahili kukubalika kwa wananchi anaowaongoza. Joshua ndiye mwenyekiti wetu na hatutabadili msimamo katika hili,” alisema Sailepu.
Akizungumza muda mfupi baada ya matukio hayo, Kuney aliahidi kuongoza kwa haki na kuwaunganisha wananchi wote wa kijiji hicho ili kujiletea maendeleo.
“Sauti ya watu ni sauti ya Mungu. Sina budi kuitikia wito wa wananchi wa kuwa kiongozi wao. Nitaongoza kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu kwa faida na masilahi ya wananchi wenyewe,” alisema Kuney.
Kwa upande, mgombea aliyepitishwa na CCM, lakini akakataliwa na wananchi, Mbuki Mollel alisisitiza kuwa yeye ndiye mwenyekiti halali kisheria na ataongoza kwa kutumia busara ili kuwaunganisha wananchi wote, wakiwamo wanaompinga.
Diwani wa kata ya Naisinyai, kilipo Kijiji cha Kambi ya Chokaa, Kilempu Ole Kinoka aliunga mkono uamuzi wa wananchi kumweka madarakani mtu wanayemtaka kuwa mwenyekiti wao kwa sababu ndiyo wenye uamuzi wa mwisho.
Katibu wa CCM Mkoa wa Manyara, Ndeng’aso Ndekubari alisema amepata taarifa ya msimamo wa wananchi na kuahidi kuwa chama hicho kitatoa uamuzi baadaye.
Katika tukio jingine, zaidi ya wapigakura 200 wa Kitongoji cha Nanja Madukani, Kata ya Lepurko, Monduli mkoani Arusha walishindwa kupiga kura baada ya kituo hicho kukutwa kimefungwa na kuwekwa tangazo la kutokuwapo kwa uchaguzi kwa maelezo kuwa mgombea wa CCM amepita bila kupingwa, huku kukiwa na madai kwamba haikuwa kweli.
Msimamizi wa msaidizi wa uchaguzi katika kijiji hicho, Isaya Laizer alisema uchaguzi wa kitongoji hicho, haukufanyika kwani wagombea wa Chadema walijitoa.
“Tuliletewa barua za kujitoa wagombea wa Chadema na zipo kwa mkurugenzi ndiyo sababu hakuna uchaguzi katika hiki kitongoji,” alisema Laizer ambaye pia ni ofisa mtendaji wa Kijiji cha Nanja.
Hata hivyo, mgombea uenyekiti kwa tiketi Chadema, Makoo Mateyi na mwenzake Shabani Naitetei aliyekuwa akigombea nafasi ya ujumbe wa serikali ya kijiji, walikanusha madai ya kujitoa katika kinyang’anyiro hicho.
“Hadi muda huu (saa sita) ofisi zimefungwa watu wanashindwa kupiga kura hatujui hatima yetu, ofisa mtendaji wa kijiji hayupo,” alisema Mateyi.
Mmoja wa wapigakura wa kituo hicho, Lomayani Ladaro alisema kinachofanyika ni hujuma dhidi ya wagombea wa upinzani.
Mwenyekiti wa Chadema wilayani Monduli, Japhet Sironga aliwatuhumu viongozi wa CCM wa Kata ya Lepurko kwamba walighushi barua na kuipeleka kwa msimamizi ikionyesha kuwa wagombea wao wamejitoa, jambo ambalo si sahihi. “Huu ni uhuni wa hali ya juu, lazima tupinge uchaguzi huu mahakamani,” alisema Sironga.
Uchaguzi katika Kijiji cha Qurus, Wilaya ya Karatu ulisimamishwa baada ya mgombea mmoja kuwania nafasi uenyekiti wa kitongoji hicho, kupitia Chama cha Sauti ya Umma (Sau) na ujumbe wa serikali ya kijiji kupitia Chadema.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Moses Mabula alisema jana kuwa uchaguzi huo utafanyika kesho ili kuondoa dosari hiyo.
Hata hivyo, mkazi wa kijiji hicho, Jeremia Bayo alisema kabla ya uchaguzi, mgombea huyo alikuwa mwenyekiti wa kitongoji kupitia Chadema lakini alishindwa katika kura za maoni.
“Baada ya kushindwa aliomba kugombea ujumbe na akapitishwa sasa tumeshangaa tena leo kuona jina lake anagombea kwa Sau tunaamini ni njama za kugawa kura,” alisema Bayo.
Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Karatu, Moshi Darabe alisema kutofanyika kwa uchaguzi huo kumetokana na njama za kukihujumu chama chake na kwamba kinalichunguza kujua chanzo ili kuchukua hatua.
Hata hivyo, alisema Chadema kina uhakika mkubwa wa ushindi katika wilaya hiyo, ambayo tangu mwaka 1995 inaongozwa na chama hicho.MWANANCHI.
0 comments :
Post a Comment