Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imetaka uboreshwaji wa Daftari
la Kudumu la Wapiga kura usimamiwe na Jeshi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ).
Imesema kila wilaya nchini itakuwa na askari sita
wa JWTZ ambao watashirikiana na wataalamu wanne wa Teknolojia ya Habari
na Mawasiliano (Tehama) kutoka Nec na kampuni inayotengeneza vifaa vya
uandikishaji.
Akizungumza katika mkutano baina ya tume hiyo na
wadau wake juu ya hatua iliyofikiwa katika kuboresha daftari hilo,
Mkurugenzi wa Nec, Julius Malaba alisema timu hiyo itasimamia
uandikishaji na kufanya matengenezo madogomadogo ya vifaa wakati wa
uandikishaji iwapo yatahitajika.”
Hata hivyo, mpango huo wa kutumia JWTZ umepingwa
na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wakisema unaweza kuliingiza
Taifa kwenye machafuko.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa alisema
kwa mpango huo, Nec inaweza kuiingiza nchi kwenye machafuko kama
yaliyotokea katika nchi nyingine.
Alisema kulitumia jeshi ni sawa na kuondoa
demokrasia ambayo imezoeleka kwa Watanzania na kusisitiza kuwa tangu
nchi imepata uhuru, hakuna siku ambayo jeshi lilitumika kwenye masuala
ya uchaguzi wala uandikishaji wa daftari la wapigakura.
“Hii mitambo ya BVR kwani ni ya kijeshi mpaka
mnasema jeshi litumike kusimamia daftari hili? Tumieni busara ili
demokrasia iendelee kuwapo nchini,” alisema Dk Slaa.
Mkurugenzi wa Uchaguzi Chama cha Sauti ya Umma
(Sau), Johnson Mwangosi alisema tangu mwaka 1995, vyama vya siasa
vilikataa jeshi kuingizwa kwenye siasa, hivyo hakuna sababu kusimamia
daftari hilo wala kujihusisha na uchaguzi.
Pia aliiomba Nec kutotumia Vitambulisho vya Taifa katika mchakato huo akisema ni Watanzania wachache wenye vitambulisho hivyo.
Mwenyekiti wa ADC, Said Miraji alisema: “Kutumia jeshi kwenye uandikishaji ni sawa na kutokomeza demokrasia iliyopo nchini.”
Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Sheweji
Mketo alisema: “Ni kosa kulihusisha jeshi katika hili. Haya ni matokeo
ya Nec kutovishirikisha vyama vya siasa katika kuandaa taratibu za
maboresho haya.”
Kaimu Katibu Mkuu wa NCCR - Mageuzi, Faustine
Sungura alisema: “Kulitumia jeshi ni sawa na kuwaambia wananchi
wasijitokeze kabisa kujiandikisha. Wakiwaona watashindwa kujiandikisha,
watakaopiga kura watakuwa wachache.”
SOURCE;CLANSMEDIA
SOURCE;CLANSMEDIA
0 comments :
Post a Comment