-->

NJIA NANE ZA KUJIONGEZEA MOTISHA AU HAMASA KATIKA UTAFUTAJI

Leo naomba nianze kwa shukrani kwa wote ambao mmeniandikia barua pepe,kuchangia kwa kupitia njia ya maoni aidha kupitia hapa hapa BC au kwenye ukurasa wa Facebook na hata wale ambao mmeweza kunipigia simu na kunitia moyo nisiache kuandika dondoo hizi za kusaidiana kwa kupeana maarifa mbalimbali. Inatia hamasa kuona kwamba unanisoma na zaidi unapata maarifa fulani fulani ya kuboresha maisha yako.Hiyo ndio nia yangu ya msingi.Tafadhali usisite kuniandikia.Ukiwa na swali pia usisite kuniuliza.Najibu asilimia 99.9% ya barua pepe zote zinazonijia.
Motisha au sababu ya kufanya jambo fulani(natumaini kwamba jambo hilo ni la manufaa) ndio msingi wa maendeleo ya kibinafsi na pia kijamii.Bila hamasa au motisha(motivation) ni hakika kwamba mambo mengi yangekuwa yamekwama.Dunia ya leo isingekuwa ilivyo endapo watendaji fulani fulani wasingekuwa na motisha ya kufanya mambo waliyoyafanya au wanayoyafanya.
Binadamu tunatofautiana.Kuna ambao wana motisha au hamasa zaidi kuliko wengine.Mara nyingi watu wa namna hiyo hufanikiwa maishani.Lipo kundi lingine ambalo kwa kawaida ni la watu ambao hawana motisha(not or less motivated).Hawaoni sababu yeyote ya kufanya kitu au jambo fulani.Wanahitaji kusukumwa sana,kubembelezwa,kupewa ahadi mbalimbali nk ndipo watashtuka waamke wakafanye jambo.Unaweza kuwaita wavivu ukipenda ingawa kuna tofauti kati ya mtu mvivu na yule ambaye amepoteza motisha.
Pamoja na hayo,sote hukamatwa na mtego wa kukosa au kupoteza motisha katika nyakati fulani.Unakuwa hujisikii kufanya chochote.Hutaki hata kufikiri kuhusu mbinu za kujiletea mabadiliko chanya.Unakuwa upo upo tu.Unatakiwa kwenda mazoezini lakini hujisikii.Unatakiwa kumaliza kusoma kitabu fulani lakini wapi.Unatakiwa kwenda kazini lakini motisha huna nk.Hiyo hunitokea hata mimi.Unaweza kufanya nini hali kama hiyo inapokutokea ili kurudisha motisha yako ya kawaida? Leo tutaangalia baadhi ya mambo ambayo unaweza kufanya;
  • Kuwa na Lengo Moja kwa wakati mmoja: Kupoteza au kutokuwa na motisha ya kufanya jambo fulani mara nyingi hutokana na kuwa na malengo mengi kichwani kwa wakati mmoja.Unataka kufanya mambo kumi kidogo.Matokeo yake ndio unapoteza muelekeo na hivyo motisha ya kufanya lolote.Unachotakiwa kufanya ni kuwa na lengo au dhumuni moja moja.Unapoipunguzia akili yako mambo ya kufikiri,itakusaidia kutimiza malengo uliyonayo.Kumbuka kufanya jambo moja kisha ndio urukie lingine.
  • Tafuta msukumo(insipiration): Ipo sababu inayokufanya utake kufanya unalotaka kulifanya.Kama wewe ni mwanafunzi basi bila shaka kuna mtu ambaye ungependa kuwa kama yeye katika siku za mbeleni.Kama wewe ni mwanamichezo basi sio ajabu kwamba yupo mwanamichezo fulani ambaye ungependa kufikia na hata kupita mafanikio yake.Kuna sababu katika kila kitu.Unachotakiwa kufanya ni;unapoona motisha inapotea,hamasa inapungua basi jipatie msukumo kwa kuangalia tena mafanikio ya mtu/watu au nchi unayoitamani.Unataka kujenga mwili kama aliokuwa nao Gavana wa sasa wa jimbo la California nchini Marekani (Arnold Schwaznegger) enzi alipokuwa Mr.Universe basi ni shurti ujitahidi na mazoezi.
  • Jitie Shauku: Hili linaweza kuonekana la kawaida kwako.Ukweli ni kwamba ili uwe na hamasa au nia ya kufanya jambo fulani au kutimiza lengo fulani,ni lazima uwe na shauku(excitement) juu ya jambo hilo. Yawezekana ukawa unapata shauku au hamasa baada ya kumweleza umpendaye juu ya jambo au lengo ulilonalo.Waweza pia kujitia hamasa kwa kusoma zaidi kuhusu jambo fulani. Vyovyote vile,jitie shauku.Jitie msisimko juu ya lengo lako.Ukifanya hivyo hutopoteza motisha kirahisi.
  • Andika lengo/malengo yako: Mali bila daftari hupotea bila habari.Umeshawahi kusikia msemo huo.Hali ni hiyo hiyo hata katika mambo mengine yakiwemo haya ya motisha na hamasa.Andika lengo lako mahali ambapo unapaona kila mara.Waweza bandika lengo lako pembeni mwa kitanda chako,kwenye kompyuta yako kazini au nyumbani.Waweza andika kwenye ukurasa wa kwanza wa simu yako nk.Hiyo itakusaidia kukumbuka na pia kuona “soni” fulani hivi unaposhindwa kutimiza lengo au kujikosesha hamasa ya kutimiza.
  • Mwambie mtu wako wa karibu kuhusu lengo lako: Kila mtu hupenda kuonekana chapa kazi na mtu ambaye anaheshimu ahadi zake mbele ya watu.Ninaposema nitakuandikia makala moja kila wiki ninakuwa nimeahidi.Sitopenda kukuangusha au kujiangusha mwenyewe.Kwa maana hiyo nitajitahidi kwa kila namna kutimiza lengo langu.Kama umedhamiria kwamba mwaka huu utakwenda mazoezini sio chini ya mara tatu kwa wiki,mwambie mtu.Utaona kwamba kila unapokosa mazoezini unaona kama yule mtu uliyemwambia kuhusu lengo lako anakuona na kukusuta vile.
  • Fikiria Faida Badala ya Ugumu: Mara nyingi huwa tunashindwa kufanya jambo fulani kwa sababu kabla ya hata kuanza kufanya tunafikiria jinsi ilivyo ngumu kufanya jambo hilo.Tunajipa mawazo hasi.Tunashindwa hata kabla hatujaanza.Unashauriwa kufikiria kwanza kuhusu faida kabla ya kuanza kujipa mawazo ya jinsi ilivyo vigumu kutimiza unachotaka kufanya.
  • Usikate Tamaa: Pamoja na juhudi zote,bado yawezekana kukawa na ukosefu wa motisha.Bado unaweza kuhisi kwamba lengo lako halina nguvu tena.Huoni faida yake wala unakokwenda.Unahisi unapoteza muda wako tu.Ikitokea hali kama hiyo usikate tamaa. Endelea kujitia motisha/hamasa.Usikubali kushindwa kirahisi.Jiambie moyoni kwamba unaweza na utatenda.
  • Omba Msaada: Wengi wetu huwa ni wagumu sana kukiri kwamba jambo fulani linakuwa gumu sana.Usiwe mtu wa namna hiyo.Duniani tupo pamoja ili kusaidiana.Ninaloliweza au kulijua mimi sio lazima na wewe ulijue.Usione haya kuomba msaada.Hautopungukiwa na chochote kwa kuomba msaada.
Share on Google Plus

About Omari Makoo

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment