DAR ES SALAAM.
WANACHAMA wa Simba wamemtaka Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage kujiuzulu hadi ifikapo Jumamosi la sivyo wataandamana kwenda bungeni mjini Dodoma.
WANACHAMA wa Simba wamemtaka Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage kujiuzulu hadi ifikapo Jumamosi la sivyo wataandamana kwenda bungeni mjini Dodoma.
Wanachama hao wakiwakilishwa na wenyeviti wao wa
matawi Mkoa wa Dar es Salaam walisema jana, lengo la maandamano hayo ni
kumshtaki Mwenyekiti huyo kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda kwa kitendo
chake cha kusigina katiba ya klabu hiyo ya Wekundu wa Msimbazi.
Masoud Hassan ‘Ustadhi’ mwenye kadi namba 536
ambaye ni Mwenyekiti wa Tawi la Mpira Pesa alisema: “Tunataka mkutano,
wanachama ndio wenye uamuzi wa mwisho, Rage ajiuzulu tunampa mpaka
Jumamosi la sivyo Jumatatu tunamzukia bungeni, jimbo lake la Tabora
Mjini analoliwakilisha si kubwa kama Klabu ya Simba.
“Kwanza amekiuka katiba yetu ibara ya 22
inayozungumzia mkutano wa dharura, unaotakiwa kuitishwa ndani ya majuma
mawili yani siku 14 licha ya TFF kumheshimu na kutangaza kumtambua na
wakamtaka aitishe mkutano pia amekaidi, sasa huko bungeni anakotunga
sheria, anatunga sheria gani ambazo anazivunja tena kwa makusudi.
“Amekiuka pia ibara ya 40 inayozungumzia chombo
cha haki, mpaka leo hajaunda chombo kitakachosimamia masuala mbalimbali
ya uamuzi ndani ya Simba, nafasi ya Makamu mwenyekiti Geofrey Nyange
ilitakiwa ijazwe ndani ya siku 90 lakini mpaka leo haijajazwa.
“Kibaya zaidi amekiuka ibara ya 2 (2) kwa kumteua
Michael Wambura kuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji wakati Wambura
alisimamishwa uanachama wa Simba Mei 5 mwaka 2010 yeye na Juma Ntema
baada ya kwenda mahakamani na hatma yao ilikuwa iamuliwe na mkutano mkuu
wa wanachama ama kusamehewa adhabu yao na kurudishwa kundini au
kuvuliwa uanachama,” alidai.
Kutokana na hali hiyo, Ustadhi alisema licha ya
kumtaka Rage ajiuzulu kwa hiyari pia hatma yake itajulikana kwenye
mkutano mkuu wa dharura wa wanachama kwa kumchukulia adhabu zaidi
Mwenyekiti huyo kwa kukiuka katiba yao.
Hata hivyo, Wambura alipoulizwa kuhusiana na suala
hilo alisema, “Walichoongea ni mawazo yao na hiyo barua ya mimi
kufungiwa Simba kama wanayo ni ya kwao hao mimi sijawahi kuiona.”
“Isitoshea kusuluhisha migogoro si lazima niwe
mwanachama wa Simba, Rais Mkapa alipoenda kusuluhisha mgogoro Kenya
kwani yeye ni Mkenya?” alihoji.
Simba imeingia kwenye mgogoro baada Kamati ya
Utendaji chini ya Joseph Itang’are ‘Kinesi’ kumsimamisha Rage kwa kile
walichodai ni kukiuka katiba.
Hata hivyo, Rage alipinga kwa kile alichodai kikao kilichomsimamisha ni sawa na kikao cha harusi.
Rais wa TFF, Jamal Malinzi alisema Kamati ya
Utendaji ya TFF itakaa Desemba 22 kujadili iwapo Rage ataitisha mkutano
wa wanachama alioagizwa na chombo hicho au hapana ambapo alipewa siku 14
hadi leo. MWANANCHI
Blogger Comment
Facebook Comment