-->

KILIMANJARO STARS WAMTANDIKA SOMALIA BAO MOJA BILA KATIKA KOMBE LA CHALENJI

KILIMANJARO Stars imeingiza mguu mmoja kwenye robo fainali ya Chalenji baada ya kuichapa Somalia 1-0 lakini Kim Poulsen amecharuka na kuwaita kikosini Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.
Poulsen ametangaza hali ya hatari kwenye mechi zijazo ikiwemo dhidi ya Burundi keshokutwa Jumatano mjini Nakuru na kusisitiza hakuna masihara tena kuanzia sasa kwavile mafowadi waliopo  wameshindwa kuonyesha makali.
Bao pekee la Kili Stars lilifungwa na Haruna Chanongo dakika 57 akipokea krosi ya Ramadhani Singano ‘Messi’.
Matokeo hayo ni tofauti na msimu uliopita ambao Stars ikicheza na Somalia tarehe kama ya jana Jumapili iliifunga mabao 7-0.
Kim alisema: “Katika mechi mbili tulizocheza dhidi ya Zambia na Somalia hakuna straika aliyefunga, ni kiungo na beki. Hii inamaanisha bado sisi si hatari kwenye ushambuliaji.”
“Nimewaita mastraika Samatta na Ulimwengu watatua leo (jana Jumapili) jioni na kuanzia mechi na Burundi tutakuwa hatari. Kwenye hizi mechi zilizopita fowadi yangu haikuwa na madhara jambo ambalo linafanya tufunge magoli machache na mepesi.
“Hatukuwa na madhara kwa mabeki, lakini ninaamini kwa ujio wa Samatta na Ulimwengu tutafanya mabadiliko makubwa kwavile wana uzoefu mkubwa na ni wachezaji ambao wamezoea mashindano, tutakuwa na madhara sana kuanzia mchezo ujao, hilo ndilo ninaloweza kuwathibitishia,” alisisitiza kocha huyo ambaye anaitumia michuano hiyo kuisuka timu kwa fainali za Afrika mwakani.
Katika mechi dhidi ya Somalia, Stars ilitengeneza nafasi nyingi lakini ikashindwa kumalizia huku wapinzani wao wakicheza kwa kukamia na kukaba kitimu tofauti na misimu iliyopita.
Stars ilichezesha kikosi chenye badiliko moja tu ya kile kilichotoka sare ya bao 1-1 na Zambia mjini Machakos. Katika kikosi cha jana Poulsen alimuweka benchi Hassan Dilunga na kumuanzisha Athuman Idd katikati akicheza na Frank Domayo.
Stars ilikuwa hivi; Ivo Mapunda, Himid Mao, Erasto Nyoni, Said Morad, Kelvin Yondani, Frank Domayo, Aboubakary Salum, Athuman Idd, Mrisho Ngassa/Mussa Shah, Elius Maguri/Chanongo na Amri Kiemba/Ramadhani Singano.
Kukamia kwa Somalia kuliwachanganya wachezaji wa Stars ambao walionekana kupaniki, ingawa kipindi cha pili Mussa Shah, Chanongo na Messi walibadili mchezo na kwenda sawa na vijana wa Somalia ambao fowadi yao ilikuwa butu.
Uwanja uliokuwa chepechepe ulikuwa kikwazo cha Stars kuonyesha mchezo mzuri ingawa pointi nne zimeipa faida ya kunusa robo fainali.
CHANZO:MWANASPOTI
Share on Google Plus

About Omari Makoo

    Blogger Comment
    Facebook Comment