UFAFANUZI KUHUSU TAARIFA YA NDUGU ALI O. CHITANDA
Kutokana
na kuwepo kwa taarifa ya Ndugu Ali Omari. Chitanda, huku pia waandishi
wa habari wakitaka kujua na kupata ukweli kutoka Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA, tunapenda kutoa ufafanuzi mfupi;
Kwanza
suala la maamuzi ya Kamati Kuu ya kuwavua uongozi ndani ya chama, Ndugu
Zitto Kabwe na Dkt. Kitila Mkumbo, chama kimeshafunga mjadala kwenye
vyombo vya habari kwa kuheshimu na kuzingatia taratibu za kikatiba za
ndani ya chama kuendelea.
Pili
kuhusu suala la restructuring ya Makao Makuu ya Chama. Chitanda ametoa
taarifa akiwataja wakurugenzi wafuatao, kuwa ni wapya;
1.Mkurugenzi wa Oganaizesheni Mhe. Singo Kigaila Benson.
2. Mkurugenzi wa Mawasiliano na Mahusiano ya ndani Mhe. John Mnyika
3. Mkurugenzi wa Fedha na Uwekezaji Mhe. Anthony Komu.
4. Mkurugenzi wa Bunge na Halmashuri Mhe. John Mrema.
5. Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama Mhe. Wilfred Lwakatale.
2. Mkurugenzi wa Mawasiliano na Mahusiano ya ndani Mhe. John Mnyika
3. Mkurugenzi wa Fedha na Uwekezaji Mhe. Anthony Komu.
4. Mkurugenzi wa Bunge na Halmashuri Mhe. John Mrema.
5. Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama Mhe. Wilfred Lwakatale.
Wakurugenzi
wote aliowataja si wapya. Mkurugenzi pekee ambaye uteuzi wake ni mpya
na umefanyika hivi karibuni na kuthibitishwa ni Mwanasheria Peter
Kibatala, atakayesimamia Kurugenzi ya Sheria na Haki za Binadamu.
Kama
ni suala la kuangalia mtu anatokea wapi (ambalo halijawahi wala
haliwezi kuwa moja ya vigezo), ili kuonesha ukweli na kubainisha uongo
wa watu wanaojaribu kufanya kazi ya CCM wakisema wao ni wanaCHADEMA, kwa
kutumia propaganda zile zile na kuzifanya kuwa ni kete zao za kisiasa
ndani ya chama, tunaweza kutaja maeneo ya wanakotoka au asili yao kama
ifuatavyo;
Mkurugenzi wa Fedha na Uwekezaji, Antony Komu- Kilimanjaro.
Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama, Wilfred Lwakatare- Kagera.
Mkurugenzi wa Mafunzo na Oganaizesheni, Benson Kigaila- Dodoma.
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, John John Mnyika- Mwanza
Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri, John Mrema- Kilimanjar.o
Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu, Peter Kibatala- Morogoro.
Hadi
sasa uteuzi wa kurugenzi za Makao Makuu ya CHADEMA haujakamilika. Bado
kuna nafasi zinazotakiwa kujazwa kwa kufuata taratibu za chama.
Hii
ni kwa sababu maboresho yanayofanyika ndani ya chama, hadi sasa
yanaendelea katika ngazi ya Makao Makuu na kanda, kisha itaendelea kwa
ngazi za mikoa, wilaya, majimbo, kata, kijiji na hatimaye kitongoji.
Katika
maboresho hayo, kwa nafasi za uteuzi, yanayoendelea sasa ambayo
yanakwenda hatua kwa hatua, hadi kuwa na makatibu wa kuajiriwa ngazi ya
chini ya chama, chama kinazingatia uwezo, uadilifu na utayari wa mtu
katika kutoa utumishi bora kwa wanaCHADEMA na Watanzania wote katika
nafasi husika.
Suala
la maslahi ya watumishi wa CHADEMA ni utaratibu wa chama ambao
unajadiliwa, kufikiwa uamuzi na kisha kuridhiwa kwenye vikao vya chama,
kama ilivyofanyika kwenye kikao cha Kamati Kuu kilichoketi karibuni.
Katika
suala hili la maslahi ya watumishi wanaojitolea Makao Makuu ya CHADEMA
ambayo si siri, Ndugu Chitanda amesema uongo mkubwa. Kusema kwamba Ofisa
Mwandamizi anaweza kulipwa posho kubwa kuliko Mkurugenzi wa kurugenzi
husika, ni uongo unaovuka mipaka.
Ndugu
huyo anadhihirisha uongo huo yeye mwenyewe kwa kuandika hivi;
"800,000/= za awali na sasa itakuwa ni kuanzia Tshs.
1,500,000-2,500,000/= kwa Mkurugenzi na kutoka Tshs.6,800,000/= kwa
Afisa Mwandamizi na sasa ni Tshs.1,000,000-1,500,000/=".
Pia
si kweli kuwa kila mtumishi anayejitolea Makao Makuu analipwa.
Mathalani, wakurugenzi wenye nafasi za ubunge, hawalipwi hata shilingi
moja kwa kazi zote wanazokitumikia chama na Watanzania kwa ujumla.
Kwa
maelezo hayo ya kutengeneza, ni kwamba hadi sasa Ofisa Mwandamizi
anapokea posho kubwa kuliko Mkurugenzi na hata baada ya maboresho
atapata posho kulingana na Mkurugenzi. Anapaswa kuwa mkweli. Mtu
anayetaka kuonekana muungwana, anapaswa kujiweka mbali na uongo pamoja,
maneno ya kutunga pamoja na upotoshaji wa makusudi.
Kama
ilivyoelezwa hapo juu, restructuring inaendelea. Ni hatua kwa hatua.
Itafika ngazi za chini kama Baraza Kuu lilivyoagiza. Kwa sababu hiyo
hadi sasa uteuzi wa Makatibu wa Mikoa na Wilaya haujafanyika.
Hata
hivyo ruzuku imekuwa ikipelekwa kila kanda, mkoa, wilaya na jimbo kama
ilivyoridhiwa na Kamati Kuu. Na hii ni zaidi ya pikipiki, kompyuta na
magari yaliyopelekwa kila kanda. Angelikuwa mkweli, nagelisema na hili
pia.
Ndugu
Chitanda anajichanganya sana katika taarifa yake yote. Hii ni moja ya
sifa ya kukosa hoja hivyo mtu anaamua kuibua viroja au kutunga maneno
kwa sababu ya kujaribu kuukana ukweli anaoujua moyoni. Tutatoa mfano
mmoja;
Kupitia
taarifa yake, anasema alikuwa mtu aliyeaminiwa hadi kuwa katika vikao
muhimu, lakini wakati huo huo anasema kuna ubaguzi! Tunapaswa kumhurumia
kwa kushindwa kuunganisha hata mawazo yake na kupata mtiririko wa hoja
zenye mantiki! Angelikuwa mkweli angesema katika vikao vya sekretarieti
na CC, aliingiaje kama kuna ubaguzi wa dini!
Kwa
sababu anazozijua yeye, Ndugu Chitanda ameamua kujipachika cheo ambacho
hajawahi kuwa nacho. Amejiita kuwa ni Katibu wa Sekretarieti ya Makao
Makuu.
Ndani
ya CHADEMA pamoja na kwamba nafasi hiyo imetajwa ndani ya Katiba ya
Chama, hakuna mtu ambaye ameteuliwa kutumikia nafasi hiyo. Kama anaweza
athibitishe kwa kutoa barua ya uteuzi kutoka kwa Katibu Mkuu.
Mahali
pengine amejitambulisha kuwa ni Katibu Ofisi ya Katibu Mkuu. Ofisi hiyo
ina Katibu Mtendaji mmoja ambaye ni Mzee Victor Kimesera, mmoja wa
waasisi wa CHADEMA.
Operesheni ya Chama inayoendelea nchi nzima kwenye majimbo 103, si suala la siri wala lengo bovu kama anavyotaka umma uamini.
Ni
mwendelezo wa mpango mkakati wa chama kupitia progamu za Vuguvugu la
Mabadiliko (M4C), unaotekelezwa kwa hatua mbalimbali na kwa mbinu
tofauti tofauti pamoja na dhana ya CHADEMA ni msingi.
Operesheni
hiyo ambayo ni mwendelezo wa nyingi za namna hiyo zinazokwenda ngazi za
chini kabisa za chama, zikilenga kuimarisha taasisi na mifumo, imeanza
wiki hii na ilitangazwa mbele ya waandishi wa habari.
Tungependa
kumalizia ufafanuzi huu mfupi kwa kutoa tahadhari kwa umma kuwa makini
na matamko ya watu wa namna hii. Maana tunajua kwa uhakika yako mengi ya
namna hii yataandaliwa na kutolewa kadri ambavyo Watanzania wanakaribia
kuona na kuishi matumaini ya mabadiliko ya kiutawala na mfumo ndani ya
nchi yao.
Mathalani
katika taarifa yake, Ndugu Ali Chitanda amedhihirisha na kuonesha kuwa
ni aina ya watu ambao wanaCHADEMA na Watanzania kwa ujumla wanapaswa
kuwaangalia kwa macho ya kuhoji na tahadhari ya hali ya juu, anasema
hivi;
"Kwa
kuwa siamini kwamba kuvuliwa nyadhifa kwa Zitto Kabwe na Dkt Kitila
Mkumbo ni kwa sababu ya waraka wa ushindi, bali ninaamini kuvuliwa kwao
ni kutokana na hofu ya uchaguzi, ubaguzi wa kikabila na kikanda."
Aya
hiyo pekee inayotumia lugha wanayotumia mahasimu wa CHADEMA,
wakiongozwa na viongozi waaandamizi wa CCM, wanaohangaika kutokana na
Watanzania kuwakataa, wakijiandaa kuwaondoa madarakani kwa sababu sera
zao zimeshindwa, inatosha kuonesha uhalisia wa yeye mwenyewe (mtoa
taarifa) alivyo.
Ni
kauli za namna hii (kuwatisha na kutaka kuwatenganisha Watanzania)
ambazo zimekuwa zikitumiwa na watawala kama njia pekee ya kutaka kuzuia
upepo wa mabadiliko unaovuma nchi nzima, zimekuwa zikiwaunganisha zaidi
Watanzania kuiunga mkono CHADEMA bega kwa bega, ili kupata haki na
matumaini ya wanyonge, katika mapambano ya awamu ya pili, kuelekea uhuru
wa kweli.
Imetolewa leo Novemba 30, 2013, Dar es Salaam na;
Tumaini Makene
Ofisa Mwandamizi wa Habari- CHADEMA
Blogger Comment
Facebook Comment