Imechapishwa Ijumaa, 29 Novemba 2013 07:02
Imeandikwa na Mwandishi Wetu
Imesomwa mara: 9954
BAADA ya Katibu Mkuu wa Chadema, Dk
Willibrod Slaa kufunga mjadala wa mgogoro unaoendelea ndani ya chama
hicho, agizo hilo limeonekana kufuatwa vema na wajumbe wa Kamati Kuu,
lakini limewafungua wajumbe wa Baraza Kuu, Mkutano Mkuu na taasisi za
chama hicho.
Tayari imeripotiwa kuwa uamuzi wa chama
hicho kumvua madaraka aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Kabwe Zitto na
aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo, umeipasua Kamati hiyo
katika vipande vya wafuasi wa wagombea uenyekiti wa chama hicho katika
uchaguzi ujao, Mwenyekiti wa sasa Taifa, Freeman Mbowe na Zitto.
Miongoni mwa wajumbe wa Kamati Kuu
wanaotajwa kumwunga mkono Mbowe ni Dk Slaa, Mwanasheria Mkuu wa Chama
hicho, Tundu Lissu, Msemaji wa Chama hicho, John Mnyika na Mbunge wa
Arusha Mjini, Godbless Lema.
Waliojitokeza waziwazi kumwunga mkono
Zitto ni Dk Mkumbo, aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha, Samson
Mwigamba ambao kwa hatua hiyo wamevuliwa nyadhifa zao na aliyekuwa
Mwanasheria wa Mbowe, Albert Msando ambaye sasa ni Mwanasheria wa akina
Zitto.
Wengine wanaotajwa kumwunga mkono Zitto
ni aliyekuwa Makamu Mwenyekiti , Said Arfi ambaye uamuzi wa kumvua Zitto
madaraka, ulisababisha ajiuzulu nafasi hiyo.
Hata hivyo, Profesa Mwesiga Baregu,
ameripotiwa kukionya chama kwa hatua hiyo, akisisitiza kuwa baada ya
uamuzi huo wa Kamati Kuu dhidi ya Zitto, chama kilitakiwa kisubiri
baraka za Baraza Kuu, ndipo uamuzi huo utangazwe.
Wafuasi Baraza Kuu Jana Mwenyekiti wa
Chadema wa Wilaya ya Temeke na mjumbe wa Baraza Kuu, Patrick Joseph,
alitoa kauli iliyodhihirisha kuwa yeye ni mmoja wa wanaomwunga mkono
Zitto.
Joseph katika kauli yake, alionekana
kuungana na Katibu wa Chadema wa Mkoa wa Geita, Abdalah Hamis, ambaye
hakumung’unya maneno, kwani aliweka wazi kuwa yeye atamwunga mkono
Zitto. Mwenyekiti huyo wa Temeke, aliitisha mkutano na waandishi wa
habari akimtaka Mbowe, kuitisha mkutano wa dharura wa Baraza Kuu, ili
litoe uamuzi sahihi kuhusu Zitto na wenzake.
Pamoja na kuwa yeye si mjumbe wa
Sekretarieti ya chama, inayopanga ajenda za Baraza Kuu, Joseph alisema
ajenda ya kikao cha Baraza hilo, ni kutaka viongozi wawaeleze wajumbe
kwa nini wamesambaza waraka wanaodhani unawadhalilisha Zitto, Dk Mkumbo
na Mwigamba, wakati waraka huo umekidhalilisha chama kwa kuonesha
udhaifu wa Mwenyekiti na Katibu Mkuu.
Akionekana kuwasemea wajumbe wenzake wa
Baraza hilo, Joseph alisema katika mkutano huo, wajumbe watataka
waelezwe kwa nini wasiamini kwamba uamuzi huo umeathiriwa na hofu ya
uchaguzi wa ndani wa chama.
Pia watataka sababu zilizoifanya
Sekretarieti ya Kamati Kuu, itangaze ratiba ya uchaguzi mkuu wa ndani,
baada ya kuwachafua miongoni mwa watu waliotarajiwa kugombea nafasi,
mpaka kuwavua uanachama.
Mjumbe huyo bila kuonesha hofu ya
kuvuliwa madaraka kama wenzake walivyofanyiwa, alisema umefika wakati wa
kuijenga Chadema bila kufuata masuala ya ubaguzi wa kidini, kikabila
ama kikanda kama ambavyo inajulikana nje. Akifafanua hoja hiyo ya
ubaguzi, alisema kuwapo kwa Zitto na Arfi katika nafasi za viongozi wa
kitaifa, ilikuwa ni ishara ya kutokuwa na udini ndani ya chama.
"Sasa inawezaje kuwatimua na kuwaita wasaliti watu ambao mmekuwa mkijivunia kuwa ni ishara kwamba hakuna udini?"
Alihoji Mwenyekiti huyo wa Chadema
Temeke, na kusisitiza kuwa hayuko tayari kuburuzwa wala kuruhusu baadhi
ya viongozi waendelee kuibomoa demokrasia wanayoitangaza kila kukicha.
Joseph alisema chama chao kimekuwa na
tabia ya kuingia kwenye migogoro kila kinapokaribia kwenye uchaguzi wa
ndani hali inayosababisha kuchafuana na kutukanana miongoni mwa viongozi
kwa kuitana wahaini na wasaliti.
Alisema amefadhaishwa na uamuzi wa
Kamati Kuu dhidi ya Zitto na Dk Mkumbo, kwani haikuwa na mamlaka ya
kikanuni wala kikatiba kufanya hivyo na kuutangaza kwa umma.
Kauli hiyo ya Joseph, ilitolewa pia na
Dk Mkumbo, Msando ambaye pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu na Profesa
Baregu. Hata hivyo, imekuwa ikipingwa na Lissu kwa kutumia Katiba hiyo
hiyo ya Chadema, kwamba kuna kipengele kiliongezwa katika Katiba ya
sasa, kinachoruhusu Kamati Kuu kuchukua uamuzi kama huo inapoona inafaa.
Joseph alisisitiza kuwa haingii akilini
chama kinachopanga mikakati ya kushika Dola, kifukuze na kuogopa watu
wanaopanga mikakati ya wao kushinda uchaguzi ndani ya chama.
"Kama ni kweli kupanga mikakati ya
uchaguzi ndani ya chama ni uhaini na usaliti, basi operesheni zetu za
chama ikiwemo ya M4C zenyewe zinapaswa kuwa uhaini uliopitiliza kwa kuwa
nayo ni mikakati ya chama kushika Dola," alisema Patrick. Mikoani Juzi
Katibu wa Mkoa wa Geita, Hamis alitamka:
“Nikiwa Katibu wa Chadema, Mkoa wa Geita
nasema mimi na wenzangu pia wote ndani ya mkoa wetu tutakuwa nyuma ya
Zitto. Nyakati za uonevu, manung'uniko na kubaguliwa sababu tu za eneo,
ukanda, udini na kuchaguliana marafiki zimekwisha.”
Katibu wa Chadema wa Wilaya ya Tanga,
Harid Rashid, ambaye alifuatana na mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa, Hussein
Baruti na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Wilaya ya Tanga, Mohamed
Aufi, aliripotiwa kusema hakubaliani na uamuzi wa Kamati Kuu.
Rashid alisema Kamati Kuu ilikuwa na
njia nyingi za kulipatia ufumbuzi jambo hilo badala ya kuwavua uongozi.
Alisema wameamua kuwa wazi kuhusu tukio hilo kutokana na ukweli kuwa
Zitto ni mtu muhimu katika uongozi wa chama.
Kundi la vijana wanaodaiwa kuwa wafuasi
wa Zitto jijini Mbeya nao wanadaiwa kurushiana makonde na viongozi wa
Chadema katika ofisi ya chama hicho Mbeya Mjini kwa madai ya
kutofautiana misimamo kuhusu uamuzi wa Kamati Kuu. Mwenyekiti wa Chadema
wa Wilaya ya Mbeya Mjini, David Mwambigija ‘Mzee wa Upako’,
alithibitisha kutokea kwa vurugu hizo juzi mchana.
Mjadala wafungwa Kudhihirisha kuwa
wajumbe wa Kamati Kuu wametii agizo la Dk Slaa la kufunga mjadala huo,
jana gazeti hili lilipotafuta namna ya kumpata Mwigamba, alikuwa akikata
simu zake.
Lilipomtafuta Profesa Baregu, alipokea
lakini alijibu kwa ufupi kwamba kwa sasa hawezi kuzungumzia mambo ya
Chadema. Wafuasi wa Mbowe Baada ya Zitto na Dk Mkumbo kuzungumza baada
kuvuliwa madaraka, Mnyika na Lissu waliitisha mkutano na waandishi wa
habari kukanusha yote yaliyozungumzwa.
Katika mkutano wao akina Mnyika, walidai
kuwa waraka uliochapishwa na magazeti kuwa ndio uliomponza Zitto kwa
kuwa si uliowasilishwa mbele ya Kamati Kuu.
Lakini mwandishi wa waraka huo, Mwigamba
alijibu haraka kuwa hakuna kilichohaririwa bali waraka huo ndio sahihi.
Kutokana na vurugu zilizotokea Kigoma, wafuasi wa Mbowe walisema ni za
kutengeneza na leo wamejipanga kufanya mkutano kutetea hoja kuwa Kigoma
anakotoka Zitto, wanaunga mkono uamuzi wa Kamati Kuu.
Mbali na kikao hicho cha Kigoma, pia
Mratibu Mkuu wa Umoja wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu (Chasso), Dar es
Salaam, Elihuruma Himida, alisema leo umoja huo utatoa kauli kupinga
matamko ya wanaojiita wanafunzi wa vyuo vikuu, waliosema watazunguka
nchi nzima kumwunga mkono Zitto.
Elihuruma pia alidai kuwa mkutano wa
Zitto kujibu hoja za kuvuliwa madaraka, uliandaliwa na wanachama wa
Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), akina Juliana Shonza, waliohudhuria
mkutano huo wa Zitto, huku viongozi wa Baraza la Vijana la Chadema
(Bavicha), wakizuiwa kumsikiliza kiongozi huyo.
CHANZO;HABARILEO
Blogger Comment
Facebook Comment