Profesa Mussa Juma Assad
RAIS Jakaya Kikwete amemteua Profesa Mussa Juma Assad kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue kwa vyombo vya habari jana, uteuzi wa Assad ulianza Novemba 5, mwaka huu na ataapishwa leo, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Kabla ya uteuzi huo, Assad alikuwa Profesa Mshiriki, Idara ya Uhasibu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na anachukua nafasi ya Ludovick Utouh, ambaye amestaafu kwa mujibu wa Sheria za Utumishi wa Umma.
Profesa Assad ni msomi, mwenye weledi, ujuzi na uzoefu mkubwa wa uhasibu na udhibiti wa fedha ambaye ana Shahada ya Uzamivu wa Uhasibu kutoka Chuo Kikuu cha Southampton, Uingereza mwaka 2001 na Shahada ya Uzamivu katika Udhibiti wa Fedha kutoka Chuo Kikuu cha Dublin City, Jamhuri ya Ireland mwaka 1991.
Pia ana Stashahada ya Kitaaluma ya Uhasibu kutoka Chuo Kikuu cha Dublin City mwaka 1990 na Shahada ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam mwaka 1988. Pamoja na uzoefu wa kitaaluma, Profesa Assad anao uzoefu mkubwa katika eneo la uhasibu na ukaguzi.
Alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi (NBAA) kwa miaka saba (2007 - 2014); ni Rais na Mjumbe wa Chama cha Wahasibu Afrika tangu mwaka 2012; na ni mjumbe wa Bodi kadhaa za Wakurugenzi nchini Tanzania.
Katika kumteua Profesa Assad kuwa CAG, Rais anayo imani kubwa kuwa elimu, weledi, ujuzi na uzoefu alionao utamwezesha kutekeleza vema majukumu ya nafasi hiyo muhimu sana katika utawala bora wa nchi yetu.HABARILEO
0 comments :
Post a Comment