yabainika HATUA ya Rais Jakaya Kikwete kuridhia kutengua uteuzi wa
mawaziri wanne, sasa ina kila dalili za kumpa nafasi ya kuchukua uamuzi
wenye mwelekeo mpya ndani ya muda mfupi ujao kuanzia sasa... Ni katika
mwelekeo huo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye naye alitakiwa na
wabunge kujiuzulu, licha ya juzi kutokuwa tayari kulizungumzia jambo
hilo wakati akitangaza uamuzi wa Rais kutengua uteuzi wa mawaziri hao
wanne, anaaminika kutangaza uamuzi huo huku hatma yake ya kuondoka
madarakani ikiwa imezungukwa na wingu la shaka. Ingawa hadi sasa Pinda
mwenyewe amekwishasema yuko tayari kung’oka na kwamba atafurahi kama
uamuzi huo utachukuliwa dhidi yake, lakini hatua iliyochukuliwa na Rais
Jakaya Kikwete sasa inadhihirisha kuwepo kwa dalili za kutaka kumnusuru
kiongozi huyo dhidi ya shinikizo la wabunge, ambao mara kwa mara
wamekuwa wakimtaka ang’oke, wakimtuhumu kwa uzembe. Baadhi ya wadadisi
na wafuatiliaji wa mambo waliochambua uamuzi huu wa sasa wa Rais
Kikwete, wanaeleza kuwa huenda kiongozi huyo akawa anatumia staili ile
ile aliyoitumia mwaka mmoja uliopita kumnusuru Pinda. Wanaeleza kuwa,
mwaka 2012, Kikwete alilazimika kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri
kwa kuwaweka kando mawaziri nane ambao wabunge walikuwa wakishinikiza
wang’olewe pamoja na Pinda, baada ya kukasirishwa na ripoti ya Mkaguzi
Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), iliyowatuhumu mawaziri hao
kwa ubadhirifu. Hata hivyo, baada ya kufanya mabadiliko hayo,
yaliyoshuhudia mawaziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, Maliasili
na Utalii, Ezekiel Maige, Afya Hadji Mponda, Viwanda na Biashara Cyril
Chami, Uchukuzi, Omari Nundu na wengine, Rais Kikwete hakumuondoa Pinda
na tishio la wabunge kutaka kumuondoa kwa kura ya kutokuwa na imani naye
nalo lilififishwa na hatua hiyo. Wakati wadadisi na wachambuzi wa mambo
wakiwa na mtizamo huo, zipo taarifa zinazoeleza kuwa ugumu wa Rais
Kikwete kuchukua hatua ya kumuondoa Pinda unatokana na hatua yake ya
kutaka kuinusuru serikali na mzigo wa gharama za kuwalea mawaziri wakuu
pindi wanapoondoka kwenye nyadhifa zao. Hatari hiyo ya serikali kubaki
na mzigo mkubwa wa viongozi wakuu wastaafu, ndiyo inayotajwa wakati
fulani mwaka 1994 kumlazimisha Rais Ali Hassan Mwinyi kumrudisha kwenye
nafasi ya uwaziri mkuu, Cleopa Msuya, aliyepata kuhudumu kwenye nafasi
kama hiyo wakati wa utawala wa Mwalimu Julius Nyerere. Hadi sasa
Tanzania ina mawaziri wakuu wastaafu watano, ambao ni John Malecela,
Cleopa Msuya, Jaji Joseph Warioba, Frederick Sumaye na Edward Lowassa.
Hata hivyo, taarifa ambazo RAI Jumapili limezipata zinaeleza kuwa, Pinda
binafsi yuko tayari kukabidhi madaraka, ingawa uamuzi huo haijulikani
utachukuliwa namna gani na Rais Kikwete pindi atakaporejea Alhamisi wiki
hii, akitokea Marekani, alikokuwa kwenye matibabu. Kwa mujibu wa
taarifa hizo zilizolifikia gazeti hili, tayari Pinda amemueleza Rais
Kikwete juu ya azma yake hiyo, huku nyingine zikieleza kuwa
amekwishamuandikia barua ya kujiuzulu. Ingawa si Pinda wala Ikulu
waliopatikana kuthibitisha taarifa hizo hadi tunakwenda mitamboni usiku
wa kuamkia leo, ni wazi kwamba, hatua ya sasa ya Rais Kikwete inakuja
kama mbinu ya serikali yake kutaka kujisafisha kupitia mabadiliko hayo
ya Baraza la Mawaziri, ili kukwepa lawama ambazo zimekuwa zikielekezwa
mara kwa mara na jamii dhidi ya serikali yake kuhusu vitendo mbalimbali
vya ubadhirifu na ukiukwaji wa haki za binadamu. Tayari mawaziri wawili
majina yao yameanza kutajwa kurithi nafasi ya Pinda, ikiwa ataondoka
katika nafasi hiyo. Mawaziri hao ni Waziri wa Miundombinu, Dk. John
Magufuli na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu, Stephen
Wassira. Aidha kitendo hicho cha Rais kuamua kutengua uteuzi wa mawaziri
wa aina ya Emanuel Nchimbi wa Mambo ya Ndani, Balozi Khamis Kagasheki
wa Maliasili na Utalii, na David Mathayo wa Kilimo kwa tuhuma
zilizotokana na Operesheni Tokomeza, inatajwa kuliweka njia panda Baraza
zima la Mawaziri, hususan wale wanaotajwa kuwa ni mawaziri mizigo.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kuwa uamuzi huo wa Rais
Kikwete umewashtua mawaziri karibu wote, huku baadhi yao wakipata shaka
kama wataendelea kubaki katika nyadhifa zao. Ni hatua hiyo pia inatajwa
kumpatia nafasi ya kuwaondoa au kuwahamisha wizara mawaziri wengine,
wakiwamo wale waliopachikwa jina la mawaziri mizigo pindi atakapofanya
mabadiliko ya Baraza la Mawaziri. Mawaziri wanaotajwa kuwa ni mizigo na
ambao tayari wamekwishahojiwa na Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
ni pamoja na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru
Kawambwa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia.
Wengine ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza,
Waziri wa Fedha, William Mgimwa, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk
Abdallah Kigoda, na Waziri wa Nchi Menejimenti na Utumishi wa Umma,
Celine Kombani. Katika mabadiliko hayo ya Baraza la Mawaziri
yanayotarajiwa kufanywa ndani ya muda mfupi, pia huenda yakatoa nafasi
kwa baadhi ya mawaziri ama kuondoka au kubaki, lakini pia kuwajumuisha
wapya. Miongoni mwa wanaotajwa kujumuishwa katika baraza jipya la
Mawaziri ni pamoja na Dk. Asha Rose Migiro, ambaye hivi karibuni Rais
Jakaya Kikwete alimteua kwenye nafasi ya ubunge. << RAI JUMAPILI
>>
-
Blogger Comment
-
Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments :
Post a Comment