Mwili wa Aliyekuwa Mwenyekiti CCM wa mkoa wa Mwanza na Diwani wa Kata ya Kisesa, Mhe. Clement Mabina baada ya kushambuliwa
Marehemu Clement Mabina enzi za uhai wake.
MWENYEKITI wa zamani wa chama cha mapinduzi(ccm)
mkoa wa Mwanza Clement Mabina ambaye pia ni diwani wa kata ya Kisesa wilayani
Magu mkoani Mwanza ameuawa na wananchi wenye hasira katika ugomvi wa mashamba.
Tukio la kuuawa kwa Mwenyekiti huyo wa Ccm Mkoa wa
Mwanza ambaye alishindwa katika uchaguzi wa nafasi ya Mwenyekiti wa ccm mkoa wa
Mwanza mwaka jana na Waziri wa zamani na Mbunge wa zamani wa Ilemela Dk Antony
Diallo lilitokea leo asubuhi katika eneo la kijiji cha Kanyama wilayani Magu.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana na kuthibitishwa
na Mkuu wa polisi wa wilaya(OCD) ya Magu ODC Mkapa pamoja na Mwenyekiti wa
Halmashauri ya wilaya ya Magu Desdery Kiswaga zimeeleza kuwa tukio limetokea
majira ya saa mbili asubuhi.
ODC Mkapa alikiri kutokea kwa tukio la kupigwa na
kuuawa kwa Mwenyekiti huyo wa zamani wa Ccm Mkoa na Mwenyekiti wa zamani wa
Halmashauri ya wilaya ya Magu baada ya kutokea kutokuelewana baina yake na
wananchi wa eneo la kijiji cha Kanyama alikokuwa na shamba lake alikokuwa
amekwenda kupanda miti.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Magu
Desdery Kiswaga alisema kuwa amepokea taarifa za kuuawa kwa kupigwa na wananchi
wenye hasira kutokana na ugomvi wa mashamba na kuelezwa kuwa amesikitishwa sana
na kuuawa kwa Mwenyekiti huyo wa zamani wa Halmashauri ya wilaya ya Magu.
Taarifa zaidi toka eneo la tukio la Kanyama
kulikotokea mauaji hayo zimeeleza kuwa Mwenyekiti huyo wa zamani wa Ccm alifika
katika eneo hilo majira ya asubuhi kwa ajili ya kupanda miti katika eneo la
milima ya Kanyama ambalo analimiliki ambavyo hata hivyo linadaiwa kuwa na
mgogoro baina yake na wananchi.
Baada ya kufika katika eneo hilo,wananchi nao walifika
katika eneo hilo na kumhoji sababu za kupanda miti katika eneo hilo ambalo bado
lina mgogoro wa umiliki na kutokea kutokuelewana baina yake na wananchi.
Baada ya majibishano ya muda mrefu na kuona wananchi
wameanza kumzingira Mabina aliamua kufyatua risasi hewani kuwatawanya wananchi
hao ambapo kwa bahati mbaya mojawapo ya risasi hizo zilimpiga mtoto aliyekuwa
katika eneo hilo na kupoteza maisha.
Taarifa hizo toka katika eneo hilo la tukio zimeeleza
kuwa kutokana na tukio hilo wananchi walimzingira Mabina na kuanza kumpiga kwa
silaha mbalimbali za jadi kama vile mapanga, fimbo, mawe, mikuki na kusababisha
kifo chake papo hapo.
Kabla ya kurejea chama cha mapinduzi(ccm) na
kufanikiwa kuwa diwani wa Kata ya Kisesa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya
ya Magu, Mabina aliwahi kuwa mwanachama wa chama cha NCCR-Mageuzi na aligombea
nafasi ya Ubunge katika jimbo hilo mwaka 1995 na kushindwa na aliyekuwa Mbunge
wa jimbo hilo Malaki Lupondije.Habari kwa hisani ya Gsengo Mwanza.
0 comments :
Post a Comment