Makumi ya watu wenye silaha nchini Libya, wamelizingira jengo la Benki ya Taifa ya nchi hiyo mjini Tripoli. Habari zinasema kuwa, watu wenye silaha wamefunga mlango wa kuingia na kutoka katika jengo hilo na kumtaka Waziri Mkuu wa nchi hiyo Ali Zeidan ajiuzulu mara moja. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, baada ya watu hao kuegesha gari lao aina ya lori mbele ya benki hiyo ya taifa ya Libya, waliwalazimisha wafanyakazi wake kutoka nje ya jengo. Hata hivyo habari zaidi kuhusiana na tukio hilo bado hazijatangazwa rasmi na serikali. Ni vyema kuashiria hapa kwamba, Libya imekuwa ikishuhudia hali ya mchafukoge katika maeneo tofauti ya nchi hiyo huku makundi yaliyoshiriki katika harakati za kumuondoa madarakani Kanali Muammar Gaddafi yakiwa yanaendelea kuchafua usalama wa nchi sanjari na kukataa kukabidhi silaha zao kwa serikali. Hayo yanajiri katika hali ambayo hivi karibuni watu wenye silaha walimuua mwanajeshi mmoja nchini humo na kupelekea jeshi la serikali kuingilia kati huku mwana wa kanali mmoja wa kikosi cha jeshi la baharini katika mji wa Benghazi, mashariki mwa Libya akijeruhiwa. Mbali na hapo siku chache zilizopita, kulitokea mripuko wa bomu la kutegwa ndani ya gari na kupelekea zaidi ya watu 22 kuuawa na kujeruhiwa katika mji huo wa Benghazi.
CHANZO:RADIO IRANI
CHANZO:RADIO IRANI
0 comments :
Post a Comment