Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage. |
Dar es Salaam.
Hatma ya Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage itajulikana leo wakati
kamati ya utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) chini ya
mwenyekiti wake Jamal Malinzi atakapokutana Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Kikao hicho mbali na kumjadili Rage pia kitapitia ajenda mbalimbali
ikiwemo uundwaji wa vyombo vya haki Kamati ya Nidhamu, Kamati ya Maadili
na Kamati ya Uchaguzi.
Kamati hizo zinaundwa upya baada ya zile za awali zilizoundwa na Rais
aliyemaliza muda wake Leodegar Tenga kuvunjwa na Rais Malinzi mara
alipotangazwa kuwa mshindi.
Tayari Malinzi ameshaunda kamati ndogondogo na kamati hizi atakazotangaza leo ndiyo kamati za mwisho katika ngazi za uamuzi.
Mbali na kamati hizo, kikao hicho pia kitatoa tamko la mwisho kuhusu
Rage ambaye alikaidi agizo la kamati hiyo ya utendaji iliyotoa Novemba
23 kwa kumtaka aitishe mkutano wa dharura wa wanachama ndani ya siku 14
ili kujadili matatizo yanayoendelea ndani ya klabu hiyo ikiwa ni pamoja
na kufanya marekebisho ya katiba.
Hata hivyo, Rage alikaidi agizo hilo kwa kile alichoeleza kuwa katiba ya
Simba haisemi hivyo na hamlazimishi kuitisha mkutano huo, pia tayari
Rage ameweka msimamo wake kuwa anasubiri tamko hilo la TFF ili atangaze
tarehe rasmi ya kuanza mchakato wa uchaguzi.
Wakati huohuo, TFF imetangaza kesho ndiyo siku ya mwisho ya kuweka
pingamizi kwa usajili wa dirisha dogo kwa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom
na Ligi Daraja la Kwanza.
Klabu za Kagera Sugar, Mtibwa Sugar na Coastal Union ndizo timu pekee
kati ya 14 za Ligi Kuu hiyo ambazo hazikuwasilisha maombi ya usajili
katika dirisha dogo.
Ashanti United imeweka rekodi ya kusajili wachezaji 15 katika usajili wake wa sasa.
Mwananchi
0 comments :
Post a Comment