Mohamed Omari Mkwawa (Tindo) mwanamapinduzi aliyesahauliwa, mwamasishaji, mpelelezi, mtekelezaji mipango ya upigaji kura Zanzibar 1963, mwanamapinduzi Zanzibar 1964, askari wa msituni wa Afro Shirazi Party, mvushaji askari mamluki wa Kimakonde na makabila mengineo kwenda Zanzibar kupiga kura na kushiriki katika mapinduzi akiwa amekishika kitabu Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru!
Mmoja wa washirika wa Mohamed Omari Mkwawa alikuwa Victor Mkello.
Utangulizi
Kwa
kipindi kirefu historia ya mapinduzi ya Zanzibar
ilikuwa ni ile historia rasmi ambayo imeathiri historia nyingi Afrika. Viongozi
wa Afrika wanapenda ile historia itakayowakweza na kuwaonyesha wao katika
mwanga wa kupendeza. Vinginevyo historia hiyo haitakiwi. Wazalendo wenyewe hawakuwa na hamu
ya kuandika historia hii na watu wa nje walioandika historia ya mapinduzi ya
Zanzibar hawakupata kuifanyia haki historia ya Zanzibar labda kwa ugeni wao na
kwa kuyaamini maelezo yaliyokuwa “wazi” kwa wakati ule, mfano mkubwa ukiwa ni
kule kuamini kuwa mapinduzi ya Zanzibar yalipangwa na makomredi wa Umma Party.
Hapajakuwapo udanganyifu mkubwa katika uandishi na
utafiti kama huu. Dkt Ghassany amekiweka chano
uwanjani bila kawa. Akizungumza na Abdushakur Aboud wa Sauti ya Amerika Dkt
Ghassany amesema kuwa historia ya Zanzibar ni historia ya kujijuwa maisha yake
akiwa mjukuu wa babu wa mababu Muomani na mabibi wa Kimanyema na Kimwera–
mchanganyiko wa damu ya Kiarabu na Kiafrika. Hii kwa hakika ndiyo historia ya
wananchi wa Zanzibar.
Ni tabu sana kumpata huyo Muarabu Zanzibar kila umuonae
Muarabu basi ana mjomba na shangazi Mwafrika. Maadui wa Zanzibar wakiweka mkazo katika ubaguzi wa
rangi na kuwafitinisha Wazanzibari. Ukweli huu ndiyo chanzo cha matatizo yote
yaliyoikumba Zanzibar
toka vyama vya siasa vilipoanza katika miaka 1950 na matatizo yaliyosababisha
mauaji ya mwisho yakiwa mwaka 2001.
Mohamed Omari Mkwawa
Mwaka
1995 wakati wa uchaguzi wa kwanza wa vyama vyingi Tanzania nilibahatika kufuatana na mgombea
urais wa CUF Prof. Ibrahim Haruna Lipumba katika kampeni za uchaguzi katika
mikoa ya Kilimanjaro na Tanga. Prof. Lipumba alifanya mkutano mkubwa sana Tangamano kiasi cha
kuishtua CCM. Baada ya mkutano ule Prof. Lipumba na ujumbe wake walialikwa
nyumbani kwa mama mmoja akijulikana kama Mama
Ummie (sasa ni marehemu) ambako walifanyiwa dhifa kubwa. Kote tukipita mitaa ya
Tanga msafara wetu ulikuwa ukishangiliwa kwa nguvu sana. CUF ilikuwa imeingia Tanga kwa kishindo
kikubwa.
Mimi
kazi yangu ilikuwa kuangalia niliyokuwanayaona na kupiga picha. Kwa hakika
nilikuwa nikishuhudia historia ikijiandika. Historia ambayo ilikuwa imeshahibiana
sana na ile ya wakati wa kudai uhuru wa Tanganyika
katika miaka 1950. Lakini ninalotaka kusema si hili bali ni picha ambayo
niliipiga ndani ya nyumba ya Mama Ummie. Picha hii ilikuwa inamuonyesha mzee
mmoja wa makamo aliyevaa fulana ya CUF mbele ikiwa na picha ya Prof. Lipumba.
Mzee huyu alikuwa amekaa nyuma ya Prof. Lipumba. Kwa wakati ule picha hii
haikuwa na maana yoyote kwangu na hata nilipokuwa naitazama mara kwa mara sura
yake si iliyokuwa inanivutia bali ile fulana ya CUF aliyovaa ambayo ilikuwa na
picha ya rafiki yangu Prof. Lipumba.
Mungu
ana mipango yake. Mihangaiko ya kutafuta riziki yakanihamishia Tanga na nikawa
karibu sana na
baadhi ya viongozi wa CUF na wanachama
wake. Sasa hapa ndipo nilipokujakuonana uso kwa uso na mzee yule kwenye picha
yangu niliyoipiga hata kwa wakati ule ilikuwa miaka mingi iliyopita. Jina la
huyu mzee wangu ni Mohamed Omar Mkwawa.
Ilikuwa katika barza yetu ya kawaida ya kunywa kahawa na kula pweza huku tukijadili
historia ya Tanzania
ambako siku moja Mzee Mkwawa alinambia, “Mohamed nataka nikuambie kitu. Unajua
mimi nimehusika sana katika mapinduzi ya Zanzibar?”
Nilimuangalia
Mzee Mkwawa kwa makini. Fikra yangu ya utafiti na uandishi ishashtuka haipo
tena usingizini. Mzee Mkwawa aliendelea, “Mimi ndiye niliyekuwa nikiwavusha
Wamakonde kutoka Kipumbwi kwenda Zanzibar
kuipigia kura ASP na wakati wa mapinduzi mie ndiye niliyewavusha Wamakonde
kwenda kuipindua serikali ya Jamshid.” Sasa moyo wangu ukaanza kudunda kwa
nguvu. Naisemesha nafsi yangu, “Huyu mzee anajua uzito wa maneno haya?” Tuishie
hapa. Kuanzia siku ile nikawa sasa namtazama Mzee Mkwawa kwa jicho jingine na
heshima yangu kwake ikawa imepanda maradufu. Nilikuwa nimeshatambua kuwa Mzee
Mohamed Omari Mkwawa alikuwa mmoja wa wanahistoria waliosahaulika katika
historia ya Tanganyika na Zanzibar. Juu ya hayo
nilishangazwa na kitu kimoja. Iweje leo huyu mwanamapinduzi wa ASP ambae Abeid
Amani Karume alimpa jina la “Tindo” kwa ujasiri wake amekuwa mstari wa mbele
CUF chama ambacho kinanasibishwa na Hizbu hasimu mkubwa wa ASP?
Dr Harith Ghassany
Nilikutana
na Dr Harith Ghassany mwaka 1999 nyumbani kwake Maskati, Oman. Naikumbuka siku
ile kama jana vile. Kanipeleka kwake mwenyeji wangu Farouk Abdulla lakini kabla
ya kunipeleka nilikuwa nimeshalisikia jina lake mara nyingi sana pale Maskati
kila nikikutana na jamaa wenye asili ya Tanzania jina lake litaibuka. Katika
fikra yangu ikanijia kuwa Dkt Ghassany atakuwa ni mtu mzima. Sielewe kwa nini
nilipata picha hii. Tulipopiga hodi na akatokea Dkt Ghassany kuja kutufungulia mlango
nikapata mshangao mkubwa.
Aliyekuwa
mbele yangu alikuwa ni kijana mdogo sana tofauti na nilivyodhani. Kwa njia ya
utani hata kabla sijatoa salamu. Nikamgeukia Farouk nikasema, ”Ah! Dkt
Ghassany, Dkt Ghassany, Dkt mwenyewe ndiye huyu?” Mila na tamaduni za watu wa
pwani wakikutana hazipishani. Maskhara ni dalili ya mapenzi. Dkt Ghassany pale
pale alipokea yale maskhara na akajibu, ”Bwana
wangu we wanakutisha bure kwani we ulidhani litakuwa jitu kubwa?” Urafiki
na udugu wetu umedumu hadi leo na ndipo katika mazungumzo aliponifahamisha kuwa
anataka kuandika historia ya kweli ya mapinduzi ya Zanzibar. Hapo ndipo
nilipomjuvya kuhusu Mzee Mkwawa na nikamuomba aje Tanga amuhoji.
Kitu
kimoja mashuhuri kwa mashujaa wa harakati za siasa katika Tanzania ni kuwa
takriban wote wana hali ngumu sana za maisha. Sikujua vyema hali ya Mzee Mkwawa
hadi nilipofika nyumbani kwake na Dkt Ghassany. Utu uzima na udhaifu wa maisha
ulikuwa umempiga barabara. Nilimjulisha Dkt Ghassany kwa Mzee Mkwawa na
kuwaacha waendelee na maongezi yao. Niliporudi mchana kumchukua Dkt Ghassany
rafiki yangu alinambia nimuache nije jioni kumfuata. Niliporudi jioni nilimkuta
Dkt Ghassany amechoka na uso umesawijika. Tukiwa ndani ya gari yangu tunaondoka nikamuuliza kulikoni.
Dkt Ghassany akanambia maneno ambayo hadi leo yamebaki kichwani mwangu,
”Mohamed ufunguo wa kitabu changu anao Mzee Mkwakwa na kama nisingeonana nae
utafiti wangu wote wa kabla ungelikuwa hauna maana yoyote.”
Dkt
Ghassany alikuwa amechukuliwa na Mzee Mkwawa katika safari ya zaidi ya nusu
karne. Mzee Mkwawa akimshika mkono kwanza kumpeleka Pemba ambako akiwa kijana
wa kiasi cha miaka 25 akifanya kazi ya uashi. Huo ndio ulikuwa wakati wa siasa
za ASP na Hizbu zimepamba moto. Mzee Mkwawa alikuwa mmoja wa wachezaji wa ngoma
ile hata kama alikuwa anatoka Tanganyika. Dkt Harith akavushwa na kuletwa pwani
ya Kipumbwi na Sakura ambako Mzee Mkwawa
alikuwa akisimamia kambi ya mafunzo iliyokuwa msituni ya wakata mkonge wengi
wao wakiwa Wamakonde, kambi ambayo ilitoa askari waliotumika kuipindua serikali
ya Mohamed Shamte 12 Aprili 1964.
Dkt
Ghassany hakuwa amejitayarisha kwa haya. Alishangwazwa na uwezo wa kumbukumbu
wa Mzee Mkwawa, akitaja majina na mahali na akirudia mazungumzo neno kwa neno
kati yake na maofisa wa serikali ya Tanganyika kutoka vyombo vya usalama
waliomtia katika operesheni maalum ya kuipindua Zanzibar kutoka Tanganyika.
Majina ya Abdulla Kassim Hanga, Jumanne Abdallah, Ali Mwinyi Tambwe, Victor
Mkello, Oscar Kambona na wengine yakawa yanadondoka moja baada ya lingine. Taarifa
hizi ndizo zilizommaliza Dkt Ghassany na kumsawajisha uso.
Mimi
binafsi nilipigwa na butwaa. Nilibaini kama alivyobaini Dkt Ghassany kuwa Mzee
Mkwawa alikuwa hazina na tulikuwa tumevumbua mgodi wa dhahabu. Kazi yetu sasa
ilikuwa kuchimba tu. Kumekuwa na uvumi kwa miaka mingi katika duru za wanasiasa
wapya na wa zamani na katika wanafunzi wa historia ya Tanzania na Mapinduzi ya
Zanzibar kuwa Ali Mwinyi Tambwe alihusika sana katika kupinduliwa kwa serikali
ya Zanzibar lakini hakuna aliyejuwa ni kwa kiwango gani na alihusika vipi.
Lakini zito ni kuwa yeye mwenyewe akiudhika sana mtu akimuuliza habari zile. Kwa
nini ilikuwa hivyo? Kitabu cha Kwaheri
Ukoloni, Kwaheri Uhuru cha Dkt Ghassany kilikuja kutoa majibu. Hakuna
binadamu apendae historia yake ihusishwe na mauaji na dhulma na kufutwa kwa
nchi yake.
Kwa
kipindi cha takriban miaka saba Dkt Ghassany alikuwa akija Tanga kwa mahojiano
na Mzee Mkwawa na katika kipindi hicho Mzee Mkwawa alitupeleka Kipumbwi na
Sakura na kutuonyesha sehemu zile ambazo walikuwa na kambi na wakifanya mazoezi
ya kivita na matumizi ya silaha. Mkahawa ambao wale wakata mkonge walikuwa
wakila chakula cha usiku kabla ya kuvushwa kwa vyombo vya bahari kwenda Unguja bado
upo hadi leo ingawa kwa sasa kijumba kile hakitumiki tena kama mkawaha. Endapo
itakuja siku serikali ya Zanzibar itataka kuhifadhi historia ya Mapinduzi ya
Zanzibar bila shaka moja ya vitu vitakavyokuwa katika makumbusho ni picha ya
hicho kibanda.
Victor Mkello
Kipumbwi
haijabadilika iko kama vilevile iliyokuwa miaka ya 1960. Kipumbwi imebaki vilevile kama kijiji cha
uvuvi. Mzee Mkwawa alitupeleka hadi sehemu ambapo bahari imeingia katika kijiji
lakini sehemu hiyo imefunikwa na mikoko mingi na vichaka. Tuliingia ndani na
kuangalia mandhari ya pale mahali. Hakika pale palikuwa sehemu nzuri ya
kujificha. Leo imekuwa sehemu hii ni maarufu kwa watu wa magendo. Mzee Mkwawa alitueleza kuwa hapo ndipo walipojificha
na ndipo walipopandia vyombo vyao kwa usiri mkubwa wakati wote wakiwa wamevaa
nguo matambara na kofia za makuti kama wavuvi. Tanga ilikuwa kituo muhimu cha kufanikisha
mapinduzi ya Zanzibar. Haikuwa bure kuwa Ali Mwinyi Tambwe, Jumanne Abdallah na
Victor Mkello walikuwa hapo na wala haistaajabishi kwa Dkt Ghassany kutueleza kuwa
vinara wa mapinduzi kwa upande wa bara, Mkello na wenzake, walisubiri taarifa
za mapinduzi katika mkesha ndani ya ofisi ya TANU Tanga.
Napenda
kukiri kuwa sikupata kushiriki kama msikilizaji wa mahojiano wakati wa utafiti
wa Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru. Kazi yangu kubwa sana ilikuwa kufungua
milango na kumwendesha daktari. Kwa ufupi kazi yangu ilikuwa kumwekea mwandishi
mazingira mazuri ili kazi yake iwe nyepesi. Kwa hakika ilikuwa kazi ambayo na
mimi vilevile nilisoma, kujifunza mengi na kupata faida kubwa. Katika haya
nakumbuka sakata la kumtafuta Victor Mkello. Leo si wengi wanaomjua Victor Mkello
au hata kupata kusikia jina lake likitajwa. Lakini kwa sisi tuliokuwa wadogo
tukiwa shule katika miaka ya 1960 Mkello alikuwa hapungia katika magazeti ya Ngurumo na Mwafrika. Mzee Mkwawa ndiye aliyetusaidia kumtafuta alipo. Victor
Mkello ndiyo aliyekuwa ”Amiri Jeshi Mkuu” wa lile jeshi la Wamakonde lililokuwa
na makao yake makuu katika mashamba ya mkonge ya Sakura na Kipumbwi. Bila ya
kupata kauli ya Mkello kitabu kisingeweza kuandikika.
Ilichukua
muda kuweza kumpata. Kwanza tulikwenda Muheza ambako ndiko kwao. Huko
tukaambiwa kuwa hakuwapo hapo bali kwa muda mrefu alikuwa Tanga. Mwishowe
tulimkuta nyumbani kwake Nguvu Mali. Mkello alikuwa katika kitanda cha mauti.
Kisukari kilikuwa kikimla kiwiliwili chake. Hakuwa anaweza kunyanyuka kitandani
wala kukaa. Kwa hakika alikuwa anasikitisha. Huyu hakuwa Victor Mkello
niliyekuwa namsoma katika magazeti wala yule ambae Mzee Mkwawa alikuwa
akituelezea. Mtu mjanja aliepambana na Magiriki wamiliki wa mashamba ya mkonge
akitetea haki za Waafrika katika miaka ya 1960. Huyu kwa kweli hakuwa yule
Victor Mkello aliyekuwa akisaidiana na TANU na Mwalimu Julius Nyerere kupigania
uhuru wa Tanganyika. Hiki mbele yetu kilikuwa kivuli chake. Hapakuwa na
wasiwasi wowote Victor Mkello alikuwa akisubiri malaika wa mauti amtembelee na yeye
hilo alikuwa akilijua fika.
Victor
Mkello na Mzee Mkwawa wanamapinduzi waliofutwa katika historia walitazamana na
wakasalimiana kama vile hakuwapata kujuana. Jicho la Mkello lilikwenda kwa Dkt
Ghassany kisha likaangukia kwangu kisha likarudi kwa mwanamapinduzi mwenzake
Mzee Mkwawa. Baada ya utambulisho uliofanywa na Mzee Mkwawa nilihisi woga na
wasiwasi kwenye sura ya Victor Mkello. Hakuwa anaamini kuwa Dkt Ghassany katoka
Maskati kwa ajili ya utafiti wa historia na hili lilijidhihirisha alipofunua
kinywa kuzungumza. Victor Mkello alikuwa na hisia kuwa alifuatwa kukamatwa kwa
vifo vya Waarabu vilivyotokea Zanzibar wakati wa mapinduzi ili apelekwe
Mahakama ya Kimataifa. Baadae Dkt Ghassany alinifahamisha kuwa jinsi Waingereza
walivyomueleza katika taarifa zao za siri ambazo yeye alizisoma London
zimeafikiana kabisa na jinsi alivyomuona pale. Waingereza walimsifia Mkello kwa
kusema kuwa alikuwa bingwa wa kuteleza kama samaki ndani ya maji.
Kufupisha
maelezo. Ilichukua karibu miaka mitatu kwa Victor Mkello kukubali kuzungumza kuhusu
mapinduzi ya Zanzibar. Dkt Ghassany akienda Maskati na kurudi Tanga na kila
akienda kwa Victor Mkello, Mkello hakuwa tayari kueleza kile alichokijua kuhusu
mapinduzi ya Zanzibar. Kila nilipokwenda na Dkt Ghassany kumuona Mkello hali
yake ilikuwa inazidi kudidimia. Sasa alikuwa kakatwa mguu mmoja kwa ajili ya
kisukari. Ilikuwa katika hali ile katika siku zake za mwisho ndipo siku moja
alipomwambia Dkt Ghassany aje siku ya pili na yeye atazungumza na angependa
azungumze mbele ya mkewe ili amkumbushe pale atakapokuwa kasahau kitu.
Hapa
ndipo ilipo moja ya sehemu tamu kabisa ya kitabu hiki Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru. Victor Mkello Amiri Jeshi Mkuu wa
Mamluki wa Kimakonde alizungumza. Mimi sikushiriki katika mazungumzo yale
nilijiweka pembeni ili Mkello azungumze na Dkt Ghassany kwa utulivu. Nilikuwa
nimeegesha gari yangu karibu ya msikiti jirani ya nyumba ya Mkello nikimsubiri
daktari akamilishe upasuaje mgonjwa apate nafuu. Mwendo wa Dkt Ghassany wa
kudunda alipokuwa ananijia pale nilipoegesha gari ulidhihirisha furaha yake.
Haukupita
muda mrefu baada ya mazungumzo yale na Dkt Ghassany, Victor Mkello akaaga dunia
kimya kimya. Hakuna mtu aliyejua kifo chake kama ilivyokuwa vifo vingi vya
mashujaa waliopigania uhuru wa Tanganyika. Hakuna hata gazeti moja lililotoa
taazia yake wala hotuba hazikusomwa kaburini kwake. Mkello aliondoka katika
historia ya Tanzania kimya kama jinsi mamluki wake walivyokuwa wakiingia
Zanzibar kimya kimya usiku mkuu na kwa
siri, mapanga yao makali ya kukata mkonge yakiwa chini ya nguo zao za ndani
yakisubiri kuivamia Zanzibar na kuua watu wasio na hatia. Kazi hii kwao
haikuhitaji mafunzo kwani mafunzo
walikuwanayo muda mrefu katika kazi yao ya kukata mkonge katika mashamba ya
mkonge ya Tanga. Pigo moja lilitosha kuangusha chini jani zito la mkonge seuze
kiungo cha binadamu.
Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru
ni kitabu kilichoandikwa kwa staili ya pekee wahusika wenyewe wa matokeo katika
mapinduzi kujitolea kueleza kile kilichotokea katika mapinduzi, kabla na baada
yake. Kuanzia mipango ya kuangusha serikali ya Zanzibar hadi katika kuwaua wale
waliokujakushukiwa kuwa ni maadui wa mapinduzi hadi kufikia hata kuweka wazi
jinsi walivyoshiriki katika mengi ya kusikitisha kupelekea hata msomaji
kujiuliza kwa nini hawa watu baada ya miaka yote hiyo kupita wameamua kueleza
yote hayo. Vipi Abdallah Kassim Hanga, Othman Shariff, Mdungi Ussi, Jaha Ubwa,
Abdulaziz Twala na wengineo walivyouliwa, nani alitoa amri ya mauaji, nani
aliwauwa na katika mazingira gani. Kifo cha Karume mwenyewe kwa mtutu wa
bunduki hakikuwekewa pazia na chanzo cha kuamuliwa kuwa auawe ni tofauti ya
kilichozoeleka kuelezwa. Karume hakuuawa na ”wapinga mapinduzi” kama ilivyozoeleka kuelezwa katika
historia rasmi.
Kwa kumaliza tusubiri mapitio ya kitabu hiki na ni wazi
kuwa wasomaji watapata mengi ya kuelimisha na kuhuisha. Tunategemea wasomi wa
somo la historia watakaopitia kitabu hiki watatufanyia hisani kubwa kwa
kuwaleta katika picha wahusika wakuu wa mapinduzi – Mwalimu Julius Nyerere –
fundi mkuu mwenye kishindo kikubwa lakini hakisikiki, mkono wake wa chuma hauonekani,
uso wake nyuma ya pazia, Abdallah Kassim Hanga – kiongozi hasa na mpangaji wa
mapinduzi, Victor Mkello – mtumishi wa Hanga na Nyerere bila ya yeye mwenyewe kujua kati ya hao
wawili nani aliyekuwa bingwa kumshinda mwenzake katika mchezo mchafu wa siasa ya
kuiuwa Zanzibar na Wazanzibari na wengineo.
Lakini juu ya hayo yote mipango hii ilikuwa ni ya akina
Nyerere, Hanga na Mkello pekee? Dkt Ghassany anaeleza nini kuhusu mkono wa Waingereza, Algeria,
Misri, Wachina, Warusi, Marekani na Mayahudi? Nini kilichowasukuma hao wote
katika mapinduzi ya Zanzibar?
Nini kilimsukuma Nyerere, kuwapindua Waislam walioupigania Uhuru wa Tanganyika na baadae kuwapinduwa Waislam
walioupigania Uhuru wa Zanzibar na kuendelea
kuwadhibiti hata baada ya kuipindua Zanzibar?
Nini kilichowasukuma Waingereza na Wamerekani kuachia mapinduzi yafanyike?
Lakini kubwa zaidi kipi kilichowasukuma Wayahudi kuingia na kusaidia mapinduzi,
ni ile chuki yao
ya asili dhidi ya Waarabu au kulikuwa na jengine ambalo liliwatia khofu? Na
kwanini kitabu kiitwe Kwaheri Ukoloni
Kwaheri Uhuru: Zanzibar
na Mapinduzi ya Afrabia? Kitabu kina majibu ya haya maswali mengine ambayo
bado hayajaulizwa na chemchemu mpya za utafiti.
Dkt Ghassany anastahili pongezi kubwa sana
kwa kuinusuru historia ya mapinduzi ya Zanzibar
na kuwaamsha Wazanzibari na Watanganyika toka lepe zito la usingizi ili
wajitambue na wamjue adui yao.
Anastahiki pongezi kubwa zaidi si kwa kukiandika kitabu cha Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru bali kwa
kutumia mrengo usiokuwa na mrengo. Huna pa kumuweka Dkt Ghassany na baada ya
kumaliza kukisoma kitabu ukaridhika napo. Kama
utafikiria kuwa kitabu ni cha CUF basi baada ya kusoma mpaka mwisho utavunjika
moyo. Kama utamtumbukiza ndani ya CCM basi
ataelea. La kama unataka upae nje ya masunduku na mapakacha basi utamuona
katulia ndani ya uhuisho wa umoja wa Zanzibar
na Tanganyika Mpya – Tanzania Mpya.
Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru ni ngoma nzito ambayo watu wameanza kuicheza hata
mdundo haujaanza kupigwa! Tayari imeshaingia katika rikodi za Hansard za Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Tayari imeshasikika katika Sauti ya Marekani. Tayari daktari anafuatilia kwa
karibu ukweli wa Maridhiano na kuwa kwa mara nyengine tena ukweli wake
umeshaanza kupotoshwa na waroho na tayari historia mpya na kubwa zaidi hata
kuliko ile ya Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964 imeshaanza kuvurugwa.
Watengenezaji wa filamu Hollywood
wana mtindo wa kumaliza senema zao za matokeo ya kweli kwa kueleza katika
maandishi yale yaliyowafika wahusika wa kisa kilichotengenezwa hiyo senema.
Huonyesha majina na mwisho wa hao wahusika, kama wahai, wako wapi, wamekufa na kama wamekufa ni kwa kuuliwa au kwa amri ya Mungu nk.
Katika Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru majina
ya wahusika machache ambayo yametajwa katika makala haya yako kama
hivi:
1.
Mohamed Omar Mkwawa: Yu hai
na anaishi Makorola Tanga
2.
Abeid Amani Karume: Ameuawa
1972
3.
Abdallah Kassim Hanga: Ameuawa 1967/68
4. Mustafa Songambele Yuhai
anaishi Songea.
5. Victor Mkello Amekufa
kifo cha kawaida
6. Ali Mwinyi Tambwe Baada
ya mapinduzi alikuja kuhusika katika mchakato wa kuunda muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Amekufa kifo cha kawaida.
7. Jumanne Abdallah Alitumikia
serikali kwa muda mrefu hadi alipofariki kifo cha kawaida
8. Oscar Kambona Aligombana
na Nyerere na akakimbia nchi mwaka 1967 na kwenda kuishi uhamishoni Uingereza
9. Kuna vigogo kadhaa ambavyo viko hai na kwa sasa
wameomba majina yao
yahifadhiwe.
17 Ramadhani 1431
0 comments :
Post a Comment