RAI YA MZEE ABOUD JUMBE
Ukiachilia mbali kitabu chake cha THE PARTNERSHIP, Mzee Abood Jumbe
aliyewahi kuwa Rais wa Zanzibar, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na
Makamu Wa Kwanza wa Rais wa Tanzania kabla ya kushinikizwa kujiuzulu na
chama mwaka 1984 kutokana na msimamo wake wa serikali tatu, ameandika
pia kitabu kingine kinachoitwa TUISHI BILA KUBAGUANA. Kwenye kitabu
hicho kilichochapishwa mwaka 2003 Mzee Jumbe anaeleza mengi kuhusu
kuvuliwa kwake nyazifa za uongozi kwenye chama na serikali. Fuatana nami
nikupe machache;
KIKAONI DODOMA
‘’…Siku tatu za kwanza za mkutano, Jumanne hadi Alhamis, ni wajumbe
wachache tu, wote wakiwa kutoka Tanzania visiwani, ndio waliosimama
mmoja baada ya mmoja kulalamika na kushambulia kule walikokuita
‘’kupenda kwangu na kunyima madaraka, kutosikiliza shauri wala maoni,
kujifanyia nitakavyo, kutoipenda CCM na Azimio la Arusha na madai
mengine kama hayo…’’ ( uk 15)
KUJIUZULU
‘’….Siku ya Jumamosi, baada ya kumuachia Ramadhani Haji (aliyekuwa
Waziri Kiongozi) kutoa maelezo yake, ndipo mimi nilipochambua tuhuma
zilizotolewa. Nilipomaliza nikashauri niruhusiwe kuacha shughuli zote za
chama na serikali’’
BAADA YA KIKAO
‘’….Nilipowasili nilikofikia, si muda walifika Mabwana Kawawa na Sokoine
wakifuatiwa muda mfupi na Mwalimu Nyerere. Niliambiwa kwa vile niliacha
madaraka kwa mdomo hakuna ushahidi, bora kufanya uthibitisho kwa
maandishi.
Kwa kutotaka ‘’kuchafua hali ya hewa’’ niliandika kuacha madaraka ya
Makamu Mwenyekiti wa chama na Makamu wa wa Rais wa Muungano, nikampa
aliyekuwa mpiga taipu wangu achape. Mwalimu aliponiuliza kuhusu Zanzibar
nilimwahidi kufanya hivyo nikifika Zanzibar.
HAIFAI KWENDA ZANZIBAR!
Hapo ndipo aliponiambia ingekuwa bora kwa ‘’sasa’’ kutokwenda Pemba
(Nilikotaka kumpeleka kwao mke wangu niliyekuwa nimefuatana naye ) wala
kwenda Unguja na kwa hiyo niandike na kuacha kwangu shughuli za
Zanzibar. Kwa kuona wazi wasiwasi uliojidhihirisha, nilikubali yote.
ULINZI MKALI
‘’Tulipofika uwanja wa ndege wa Dar es Salaam na kukuta ulinzi mkali wa
Jeshi na Polisi, wakiwepo mkuu wa jeshi na mkuu wa jeshi la polisi,
nilishindwa kabisa kuelewa sababu na maana ya yote hayo yalikuwa ni ya
nini au kwa nini? Mpaka leo hakuna aliyenielimisha nab ado niko
ujingani’’ (uk 17)
SIMU IMEKATWA!
‘’Nilipwerewa nilipofika nyumbani Mjimwema na kutaka kupiga simu Unguja.
Niliona , kabla ya kutangazwa yaliyotokea, niwatulize wake zangu na
wanangu Unguja angalau wajue tu nilikuwa salama Mjimwema. Niligundua
simu hazifanyi kazi! Hapo nilimshukuru Mwenyezi Mungu nikamwachia yeye
na kukaa kusubiri maajabu mengine huku nikiwaza ‘’Tunakwenda wapi’’?
SERIKALI TATU
‘’Mfumo wa serikali tatu ndio umekuwa msimamo wangu na ndio mtizamo
wangu uliopingwa vikali na chama..’’
MAHUBIRI YA KUUVUNJA MUUNGANO!
‘’Wenye kuhubiri kuuvunja muungano, watambue kuwa hawawezi kufanya hivyo
kienyeji…Huu ni muungano wa Watanzania, si wa chama hiki au kile. Wote
wenye umri wa miaka ishirini na tisa na chini ya hapo ambao naamini ndio
wengi, hawajawahi kuwa chochote isipokuwa Watanzania.
Kabla ya kuwanyang’anya au kuwafutia utanzania wao, wana haki ya
kushirikishwa kuamua nasaba yao. Hii inamaana itapaswa kufanyika kura ya
maoni ili Watanzania wenyewe ndio waamue kuvunja au kubadili mfumo wa
Muungano.
Kisheria na kwa mujibu wa katiba, si jambo dogo au jepesi kuvunja
Muungano, kama inavyoonekana baadhi ya viongozi kudhani. Lazima
Watanzania kuangalia, kutafakari kwa makini na kujuana kwa yakini
tunatoka wapi, kwa nini tuliungana, tumefika wapi na sasa tunataka au
hatutaki nini, au tunataka kwenda wapi.
RAI YAKE
Katika zoezi hili (kuhusu Muungano) wanasiasa na Watanzania kwa ujumla
wanapaswa wawe wakweli; wenye busara na zaidi kuliko yote ni uaminifu.
Miaka mia ijayo hapatakuwa, sio tu katika hili bali kote duniani, hata
mmoja miongoni mwa walio duniani leo na hata akiwepo hatakuwa na lake.
Bali, vizazi vyetu vitakuwepo. Mazao ya mbegu tunazoatika au kupanda leo
itabidi kuvunwa na vizazi vyetu kesho’’
……………………
Kwa uchambuzi/simulizi kuhusu vitabu na waandishi endelea kutembelea
ukurasa wetu wa ‘’Kitabu Nilichosoma’’. Kauli mbiu yetu ni KITABU NI
SILAHA.
Usisahau ku-like ukurasa wetu ili kukuza wigo wa watu wanaofikiwa na
taarifa zetu.
-
Blogger Comment
-
Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments :
Post a Comment