Dar es Salaam. Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda amesema kuwa, Serikali itaendelea kutengeneza mazingira mazuri ya kufanya biashara ili wawekezaji wa nje na ndani waweze kutekeleza majukumu yao bila kikwazo.
Dk Kigoda aliyasema hayo juzi usiku alipokuwa
kwenye hafla ya kuzitambua Kampuni 100 Bora zinazokua kwa kasi nchini
(Top 100 Mid–Sized Companies), ambapo Kampuni ya Kipipa Millers Limited
ya jijini Mwanza ilishika nafasi ya kwanza.
Kampuni hizo zilitambuliwa na kupewa tuzo kutokana
na shindano linaloendeshwa na Kampuni ya Mwananchi Communications (MCL)
na KPMG Tanzania na kudhaminiwa na Benki ya NBC pamoja na Soko la Hisa
la Dar es Salaam (DSE).
Dk Kigoda alisema shindano hilo linaimarika kila
mwaka na lina nafasi kubwa ya kuimarisha uchumi kwa Kampuni za Afrika
Mashariki.
Alisema ili kampuni hizo ziweze kufikia mafanikio,
Serikali itajitahidi kuweka mazingira yatakayoziwezesha kufanya
shughuli zake vizuri na kufanya uzalishaji kwa gharama nafuu.
Alizitaka kampuni zilizofanikiwa kuingia kwenye
kundi la kampuni 100 bora, kujitambua kuwa sasa wao ni washindi na hivyo
wajitahidi kufanya shughuli zao kitaalamu zaidi.
“Kwa kiwango hiki mlichofikia sasa ni washindi, mfanye kazi zenu kitaalamu zaidi,” alisema Dk Kigoda.
Alisema kwa sasa Tanzania imeshuka kwenye nchi
zenye viwango vizuri vya kufanya biashara duniani, hali inayofanya
baadhi ya wawekezaji kukimbia.
Alieleza suala hilo linaipa Serikali changamoto ya
kutengeneza mazingira bora na rafiki ili kuvutia wawekezaji kufanya
shughuli zao kwa faida.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Mwananchi
Communications Limited (MCL), Zuhura Muro alisema kwa kushirikiana na
KPMG, wanaendesha shindano hilo kwa sababu wanaelewa kuwa hiyo ni njia
muhimu ya kuhamasisha kampuni kufanya vizuri.
Alisema kuwa, kampuni hizo ni muhimu kwa uchumi wa
nchi na ustawi wake kwani kodi wanazolipa ndizo zinazotumika kwa
maendeleo ya nchi.
“Sasa ni wakati wetu wa kuinuka, lakini hatuwezi
kuinuka bila kuwa na watu muhimu kama ninyi (kampuni 100 bora) kwani
ndiyo mnaotengeneza ajira, nyie ni watu muhimu sana kwa uchumi wa nchi
hii,” alisema Muro.
CHANZO:MWANANCHI
CHANZO:MWANANCHI
Blogger Comment
Facebook Comment