Wanafunzi wa shule ya sekondari nchini wakiwa kwenye mahafali ya kuhitimu kidato cha sita.
Siku chache baada ya kufungwa kwa pazia la
udahili kwa wanafunzi wa kidato cha sita walioomba kujiunga na vyuo
vikuu nchini, imebainika kuwa zaidi ya wanafunzi 5,000 wameshindwa
kujiunga na vyuo hivyo kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo matumizi ya
mtandao wa kuomba udahili.
Pazia la udahili huo kwa wanafunzi waliomaliza
kidato cha sita mwaka huu, lilifungwa rasmi Julai 5, mwaka huu. Hadi
wakati unafika tarehe hiyo, wanafunzi waliokuwa wameomba nafasi hiyo ni
39,140.
Matokeo ya kidato cha sita mwaka huu, yanaonyesha
kuwa watahiniwa 50,611 walifanya mtihani huo na kati yao 44,366 sawa na
watahiniwa wa shule waliofaulu ni 40,242 sawa na asilimia 93.92 ya
waliofanya mtihani huo.
Watahiniwa wa kujitegemea waliofanya mtihani huo
walikuwa ni 7,659 na waliofaulu ni 4,124 sawa na asilimia 53.87.
Kutokana na matokeo hayo, watahiniwa wote waliofaulu ni 44,366, hivyo
kufanya wanafunzi walioshindwa kujiunga na vyuo vikuu kuwa 5,226.
Akizungumza na Mwananchi Jumamosi, Mkurugenzi wa
Ithibati na Ubora wa Elimu ya Juu wa Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU), Dk
Savinus Maronga alisema, wanafunzi waliomaliza kidato cha sita na
kuomba kujiunga na vyuo vikuu ni 39,140 na kwamba vyuo vikuu nchini vina
uwezo kwa kuchukua wanafunzi 60,000.
Dk Maronga alisema hali hiyo inatokana na baadhi
yao kutokuwa na sifa zinazotakiwa kuweza kuomba udahili wa kumwezesha
kusoma elimu ya juu.
“Kuna baadhi hawana sifa ‘Eligibility’ za kuweza
kuchaguliwa kuingia Chuo Kikuu. Hivyo ili uweze kudahiliwa kuendelea na
elimu ya juu ni lazima uwe na vigezo. Kuhusu mfumo sidhani kama ulikuwa
na matatizo yeyote,” alisema Dk Maronga
Kauli za Wanafunzi
Wanafunzi waliozungumza na gazeti hili kuhusu
mfumo huo wa udahili wa mtandao, walisema una usumbufu kutokana na wengi
kutokujua kuutumia.
Frank Mabagala aliyehitimu Shule ya Sekondari Pugu
Jijini Dar es Salaam, alisema wanafunzi walio wengi wameshindwa
kuutumia mfumo huo kwani una mambo mengi ya kufanya.
“Nilijaza fomu vizuri tu, lakini sikuwa najua kama
kuna wakati nilitakiwa kwenda kuangalia ‘Eligibility’ hadi nilipoambiwa
na rafiki yangu kwenda kuangalia ‘Eligibility’ na kukuta kuna nafasi
imeandikwa ‘NO’ hapana vyuo vyote nilivyochagua,” alisema Mabagala.
Alisema hata upatikanaji wa vocha za TCU bado
zilikuwa tatizo, kutokana na kupatikana sehemu moja tu ya Benki ya NBC.
Hivyo kwa watu wanaoishi pembezoni mwa benki hiyo kuwawia vigumu kupata
huduma hiyo kwa haraka.
0 comments :
Post a Comment