-->

HAYA NDIO MIONGONI MWA MADHARA YA PESA KUTOKANA NA TAFITI ZA KITAALAMU

clip_image001
Na Chande Abdallah
RIPOTI ya Wiki imegundua kuwa, fedha ni hatari kwa afya ya binadamu kwani huweza kusababisha madhara makubwa.
Katika uchunguzi, ilibainika kuwa fedha za noti na zile za sarafu huweza kukusanya na kusambaza vimelea vya magonjwa hatari kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine.


Kuhakikisha ukweli wa jambo hilo, Ripoti ya Wiki ilifanya mahojiano na mtaalam wa magonjwa mbalimbali, Dk. Richard Marise na kusema kuwa tafiti mbalimbali duniani zimeripoti kuhusu vimelea vinavyoweza kusafirishwa kupitia fedha ambavyo ni Staphylococcus Aureus, Escherichiacoli,Fecal Bacteria na sumu nyingine.
“Tafiti nyingi zilizofanywa katika nchi zilizoendelea, zimegundua kuwa vimelea hatarishi kwenye fedha hasa za noti ambapo vingi hutokana na uchafu utokao kwa mwanadamu mwenyewe kwa mfano; kinyesi, mkojo na jasho.
“Vimelea hivyo kwa pamoja husababisha magonjwa kama boils (magonjwa ya ngozi) pneumonia, toxic shock syndrome (homa za sumu mwilini), diarrhea (kuharisha), gum diseases (magonjwa ya fizi), homa za vipindi na meningitis (uvumbi wa bongo) ambao kama hakuna matibabu huweza kusababisha kifo,” alisema Dk. Richard.
Akifafanua jinsi fedha zinavyoweza kusafirisha magonjwa, daktari huyo alisema fedha huweza kushikwa na mtu asiyeosha mikono yake kwa maji safi na sabuni baada ya kutoka kujisaidia, kisha hela hiyo huweza kutua mikononi mwa mtu mwingine ambaye huacha jasho lake na kuongeza vimelea vya magonjwa mengine juu yake.
Mzunguko huo unaweza ukawa mkubwa kufikia hatua ya vimelea kusambaa kwa mamilioni ya watu hivyo kuifanya jamii kuwa katika hatari zaidi ya maambukizi ya ugonjwa husika.
Dk. Richard alikazia kuwa, maambukizi hutokea kama mtu aliyeshika hela hizo atagusa sehemu zenye unyevunyevu kwenye mwili wake kwa mfano jicho, mdomo na pua ambapo vimelea hivyo vitapata nafasi ya kuingia ndani ya mwili.
Katika mazingira ya kawaida, fedha zenyewe huhifadhiwa katika mazingira hatarishi ambapo kuna mifano ya watu kuhifadhi fedha ndani ya nguo za ndani au kwenye matiti (akina mama zaidi).
Fedha pia huweza kudondoka kwenye uchafu wa aina mbalimbali na kuokotwa kisha ikatumika tena.
Imeelezwa kuwa, ukiachilia mbali kubeba vimelea vya magonjwa, fedha zinaweza kubeba sumu na madawa ya kulevya juu yake ikiwa itapitia kwenye mikono ya mtu aliyeshika vitu hivyo.

“Ni vyema ukatumia fedha kwa uangalifu,  usiweke hela mdomoni na ukumbuke kuosha mikono yako kila mara kwa maji na sabuni ili kujikinga na maambukizi,” alitahadharisha Dk. Richard.
CREDIT TO GPL
Share on Google Plus

About Omari Makoo

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment