Mkuu wa JWTZ, Meja Jenerali Davis Mwamunyange
*Adaiwa kutoweka na nyaraka nyeti
OFISA
wa cheo cha juu katika Jeshi la Wananchi (JWTZ), anayeaminika kuwa na
asili ya Rwanda, ametoweka katika mazingira ya kutatanisha, huku akiacha
wingu la mashaka kwamba, hatua yake hiyo inaweza ikawa imeambatana na
kupotea pia kwa baadhi ya taarifa muhimu za kijeshi.
Taarifa
za kutoweka kwa ofisa huyo mwenye cheo cha luteni kanali, zinalihusisha
tukio hilo na hatua za makachero wa JWTZ kufuatilia nyendo zake na
zililifikia gazeti la MTANZANIA Jumapili kwa mara ya kwanza katikati ya
wiki hii.
Vyanzo vya habari vya kuaminika vinaeleza
kuwa, tayari maofisa wa JWTZ wameshaanza kufuatilia kwa karibu tukio la
kutoweka kwa ofisa huyo, ambalo pia limezusha hali ya sintofahamu
kwamba, huenda akawa ameondoka na nyaraka nyeti za kijeshi.
Kabla
ya kutoweka ofisa huyo, ambaye nyendo zake zimekuwa katika darubini
kali za makachero wa JWTZ, alikuwa akifanya kazi katika kitengo cha
teknolojia ya mawasiliano ya kijeshi (IT).
Hatua ya
kutoweka kwa ofisa huyo wa juu wa JWTZ anayetajwa kwa jina moja la
Selumbo, imekuja siku chache tu baada ya kuibuka kwa msuguano wa kauli
baina ya Ikulu ya Dar es Salaam na ile ya Kigali.
Chanzo
cha msigano huo wa maneno uliogeuka na kuwa mzozo wa kidiplomasia, ni
ushauri uliotolewa na Rais Jakaya Kikwete kwa Rais Paul Kagame wa
kumtaka awe tayari kukaa meza moja na waasi wa kundi la FDLR wanaopigana
Rwanda, kutoka mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Tayari
msigano huo wa Kikwete na Kagame umeanza kutajwa na baadhi ya wadadisi
wa mambo kuwa tishio kubwa la kwanza la ustawi, uimara na misingi ya
mshikamano ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambayo mataifa hayo
mawili ni wanachama wake.
Siku chache baada ya
ushauri huo, Kagame alinukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari nchini
Rwanda akimkejeli Kikwete, hata kufikia hatua ya kutoa kauli zenye
mwelekeo wa vitisho dhidi yake.
Kauli hizo za Kagame
zilisababisha Rais Kikwete, kupitia katika hotuba yake ya mwishoni mwa
Julai, kujibu mashambulizi, huku akieleza bayana kushangazwa na
kushtushwa na kejeli na matusi yaliyokuwa yakielekezwa kwake.
Akitumia
maneno ya kidiplomasia ambayo yametafsiriwa na baadhi wa wachambuzi wa
masuala ya diplomasia na sayansi ya siasa kuwa yanabeba ujumbe mzito,
Rais Kikwete alisema alikuwa amesikia yote yanayosemwa kutoka Rwanda na
alikuwa hakusudii kuyapuuza.
Kauli hiyo ya Kikwete
ambayo ilitanguliwa na ile aliyoitoa siku chache mkoani Kagera ya
kuwataka wahamiaji haramu kuondoka nchini, ilifuatiwa na matukio ya
kuondoka nchini kwa Wanyarwanda wanaokadiriwa kuzidi 5,000.
Wakati
hali ikiendelea kuwa ni ya mashaka na kutoaminiana kati ya Tanzania na
Rwanda, katikati ya wiki hii, gazeti dada la MTANZANIA Jumatano,
lilikuwa na habari kubwa yenye kichwa cha habari kisemacho; ‘Nini
kinamtia Jeuri Kagame?’ ambayo pamoja na mambo mengine, ilieleza namna
watu wenye asili ya Rwanda walivyojipenyeza katika taasisi mbalimbali
nyeti za umma.
Kuvuja kwa taarifa za kurejea Rwanda
kwa maelfu ya wahamiaji haramu sambamba na hizi za sasa za kutoweka kwa
ofisa wa juu wa JWTZ kunathibitisha kuhusu kuwapo kwa mwelekeo huo wa
mambo.
Vyanzo vya habari vya gazeti hili, vinamtaja
ofisa huyo kuwa ni mmoja wa makachero wenye asili ya Rwanda waliokuwa
wakifanya kazi ndani ya JWTZ na ambao wanahofiwa kuwa watu wenye
mawasiliano ya karibu na serikali ya Rwanda, kwa malengo ambayo bado
hayajawekwa bayana.
“Ni kweli, huyo ofisa ametoweka
jeshini na sijui sababu zilizo nyuma yake…hili suala la kuwa anakusanya
taarifa za siri za jeshi letu na kuzipeleka Rwanda nadhani
ziligunduliwa na watu wetu ambao wapo kwenye mfumo wa kijeshi,”
alidokeza mmoja wa watoa taarifa wa MTANZANIA Jumapili.
Msemaji
wa JWTZ, Meja Erick Komba, alipoulizwa na gazeti hili kupitia simu yake
ya kiganjani kuhusu ukweli wa taarifa hizo, alishindwa kukubali au
kukataa, kwa kile alichoeleza kuwa suala hilo ni zito hivyo alikuwa
akipaswa kuzungumza kwanza na viongozi wake kabla ya kulitolea taarifa.
Meja Komba alieleza kuwa, wanajeshi wanaotoroka ni wengi na wapo waliofungwa kwa kosa hilo la utoro.
“Jamani
suala hili ni zito, naliogopa, nyinyi hamlioni kama ni zito? Sio kwamba
sipendi wananchi wapate habari, suala hili tupeni muda kwanza
tulifanyie ‘analysis’, mbona wanajeshi wengi wanatoroka na hamripoti!
Waliotoroka ni wengi, wangine wametorokea Rwanda na kwingine na
wamefungwa.
“Ni lazima kwanza niongee na mabosi wangu ndiyo nizungumzie vizuri hili… njoo ofisini Jumatatu (Kesho),” alisema Meja Komba.
Sanjari
na tukio hilo, taarifa zaidi zilizonaswa na gazeti hili zimedai kuwa
sasa imebainika pasipo shaka kuhusu kuwapo kwa makachero wa Serikali ya
Kigali wanaodaiwa kupandikizwa katika taasisi na idara nyeti za serikali
kwa ajili ya kufanya ushushu kwa maslahi ya Rwanda.
Inadaiwa
kuwa intelijensia ya JWTZ iliyo na mizizi ndani na nje ya nchi ilibaini
mapema kuwapo kwa majasusi wa Kinyarwanda ndani ya mfumo wa dola na
nyendo zao zimekuwa zikichunguzwa kwa muda mrefu na zilibainisha hali
hiyo.
- Source: Mtanzania
0 comments :
Post a Comment