-->

NDEGE YA RAISI YATUMIKA KUBEBEA MKAA,MIHOGO NA NDIZI



WABUNGE wa CCM Zanzibar wameibua zengwe jipya dhidi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad kwamba anatumia ndege ya Rais kubebea mkaa, mihogo na ndizi kutoka Pemba kwenda Unguja.

Habari zilizopatikana kutoka ndani ya serikali ya Mapinduzi Zanzibar zinaeleza kuwa, tuh
uma hizo zilitolewa na wabunge hao wakati wa kikao chao na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein mwezi uliopita.

Kitendo hicho kinachodaiwa kufanyika mwezi uliopita kimeonekena kuwakera baadhi ya viongozi wa Serikali wakiwamo wabunge wa CCM Zanzibar, ambao wakati wa kikao hicho na Rais Dk Shein mwezi uliopita mjini Zanzibar, walilizungumza kwa uchungu na kuomba Rais amuonye Maalim Seif kwa kuigeuza ndege ya Rais kuwa ya mizigo.

Anayedaiwa kuibua hoja hiyo ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Taifa (UVCCM), Sadifa Juma Khamis, ambaye alisema kuwa kitendo hicho cha Makamu wa Kwanza wa Rais kutumia ndege hiyo kubebea mkaa, mihogo na mikungu ya ndizi kinadhalilisha Ofisi ya Rais.

Katibu wa Wabunge wa CCM Zanzibar, Mbunge wa Magomeni, Mohammed Chombo alipoulizwa na gazeti hili kuhusiana na suala hilo alikiri wabunge hao kulifikisha suala hilo kwa Rais Shein.

“Tulimweleza Rais matatizo mengi likiwamo na hilo la Makamu wa Kwanza wa Rais kutumia ndege ya Serikali kubebea mihogo na mkaa,” alisema.

Alisema kuwa Rais aliwaambia kuwa ameyapokea malalamiko hayo na kwamba atayafanyia kazi.

Chombo alisema kuwa kwa sasa wanamsubiri Rais Shein awaite kuwapa majibu ya matatizo yao.

Baadhi ya wabunge wa CCM Zanzibar ambao walizungumza na gazeti hili, walisema kuwa kitendo hicho ni matumizi mabaya ya mali za umma kwa sababu kuna vyombo vingi vya usafiri vinavyoweza kutumika kusafirishia mizigo hiyo.

Ofisa mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina lake kutoka Mamlaka ya Ndege za Serikali, akizungumzia utaratibu wa viongozi wa Serikali kutumia ndege hizo, alisema viongozi wa juu wa Serikali ya Muungano na Zanzibar hukodi ndege zao.

Alisema hajawahi kuona ndege kubebea mkaa, hata ndege ya jeshi hajawahi kuona ikibeba mkaa.

Hata hivyo, Katibu wa Wabunge wa CUF, Mohammed Habibu Mnyaa, alisema madai hayo ya wabunge wa CCM ni siasa chafu dhidi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na kwamba wao wanaamini hawezi kufanya jambo hilo. MWANANCHI
Share on Google Plus

About Omari Makoo

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment