Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, ameeleza
kushangazwa na hatua ya Serikali kuwapatia kazi ya ujenzi wa Bandari ya
Mwambani mkoani Tanga watuhumiwa wa sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow.
Amesema watuhumiwa hao wamepewa kazi hiyo kupitia Mradi wa Mwambani
Economic Corridor (MWAPORC), ambao utagharimu Sh trilioni 54, huku
kukiwa hakuna taratibu za utangazaji wa zabuni zilizofuatwa na Serikali.
Kauli hiyo aliitoa jana alipokuwa akihutubia mikutano ya hadhara
iliyofanyika katika miji ya Mafinga na Iringa mkoani hapa ambapo alisema
Serikali imeipa kazi ya ujenzi Kampuni ya VIP Engineering and
Management inayomilikiwa na James Rugemalira ambaye anahusika katika
sakata la Escrow.
Zitto alisema ACT-Wazalendo wanamtaka Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta
afanye uchunguzi kuhusu mradi huo wa Mwambani na achukue hatua kwa kile
alichodai kuwa utapeli wa watu wa Escrow.
“Mwambani Economic Corridor Project hapakuwa na zabuni yoyote
iliyotangazwa, na huu mradi umekuwa ukiandaliwa na Serikali. Sheria ya
Private Public Partnership (PPP) imeweka utaratibu wa zabuni kwa miradi
ya ubia na Serikali.
“Taratibu hazijafuatwa, hakuna zabuni iliyotangazwa kuhusu Bandari ya
Mwambani, miradi mikubwa kama hii Serikali hutakiwa kutoa ‘guarantee’
kwa mikopo ambayo inachukuliwa.
“Hivyo kuhusika kwa Rugemalira wa Escrow na mwanasheria Cathbert Tenga
wa Richmond kwenye mradi huu ni mwendelezo wa miradi ya kitapeli,”
alisema Zitto.
Zitto ambaye pia alikuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), alisema uzito wa mradi huo
wa bandari unakwenda sambamba na reli ambayo itafika hadi Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Kongo (DRC).
Alimtaka Waziri Sitta kutoa taarifa kwa umma kwa kuwa taifa limechoshwa na miradi ya kitapeli.
MWANASHERIA ATOA UTETEZI
Akitoa taarifa kuhusu mradi huo hivi karibuni, msimamizi wa mradi huo
ambaye pia ni Mwanasheria mashuhuri nchini, Cathbert Tenga, alisema
utamilikiwa na Watanzania wenyewe na si watu kutoka nje ya nchi kama
ilivyo katika miradi mingine.
“Sisi hivi sasa tunahangaika kuhakikisha nchi hii inasonga mbele kwani
mradi huu hivi sasa upo katika hatua za awali za upembuzi yakinifu kwa
kuwa na timu ya wataalamu, na ili jambo hili liweze kusonga mbele ni
lazima siasa ziepukwe,” alisema Wakili Tenga.
Alisema kutokana na juhudi wanazoendelea nazo hadi sasa wamefanikiwa
kupata benki ya Afrika Kusini, DBSA, ambayo itafanya kazi katika mradi
huo mkubwa nchini.
Tenga alisema mradi huo wa MWAPORC utakuwa ni moja ya nguzo kwa uchumi
wa taifa ikiwa Serikali itaamua ufanyike kwa kuwaunga mkono Watanzania
wazalendo badala ya kujali wageni pekee.
MWIGAMBA NA UMASKINI
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Samson Mwigamba, alisema
hali ya umaskini nchini imezidi kuongezeka huku viongozi wakiendelea
kuponda maisha.
“Wakati Rais Jakaya Kikwete anaingia madarakani mwaka 2005 hali ilikuwa
mbaya, lakini bado watu walikuwa na matumaini ya kurekebishiwa hali zao,
leo anakaribia kumaliza kipindi chake cha uongozi, uchumi bado
unamilikiwa na watu wachache.
“Tanzania ni nchi pekee inayochimba madini ya tanzanite, mazao yao
Mirerani ni madini, lakini bado Serikali ilichukua ule mgodi na kuwapa
makaburu kutoka Afrika Kusini huku Watanzania wakibaki watazamaji. Pia
walikuwa wakichimba huku wakiweka maji yenye sumu huku Watanzania
wakiendelea kufa kwa Ukimwi na njaa,” alisema
Mwigamba.
Alisema pamoja na tanzanite kuchimbwa nchini, lakini nchi ya Afrika
Kusini imekuwa ya kwanza katika soko la dunia kwa kuuza madini hayo
ikifuatiwa na Kenya huku Tanzania ikishika nafasi ya tisa.
Source: Gazeti la Mtanzania
-
Blogger Comment
-
Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments :
Post a Comment