Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
ASKOFU
Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Muadhama Polycarp
Kardinali Pengo amesema msimamo wake kuhusu Katiba Inayopendekezwa uko
pale pale na ametaka wanaoamini alichosema, wasambaze ujumbe wake kwa
wengine.
Akizungumza na
Chama cha Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) hivi karibuni, Askofu
Pengo alitoa wito kwa waumini kuachwa huru wafanye maamuzi yao wenyewe
juu ya kuipigia kura ya ndiyo au hapana Katiba Inayopendekezwa badala la
kushinikizwa na viongozi wa dini kuipigia kura ya ‘hapana’ katiba hiyo.
Aidha, amesema kamwe hawezi kubadili kile alichosema kwani ni ukweli anaouamini na alishaweka hilo wazi.
Askofu
Pengo alisema hayo jana wakati wa ibada Maalumu ya Shirikisho la Kwaya
Katoliki (Shikwaka ) iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Kipawa, jijini
Dar es Salaam ambako kwaya zaidi ya 100 zilishiriki.
“Jana
(juzi) baada ya ibada kule Kurasini walikuja waandishi wa habari na
tukaanza kujadiliana na baadaye nilipomaliza wengine kisirisiri
walijadili kwa nini sikusema chochote kuhusu Katiba Inayopendekezwa;
Sasa ndugu zangu niseme mara ngapi,” alihoji.
“ Hivi ni nani
anaweza kufikiria naweza kubadili maneno niliyosema, leo niseme kweli na
kesho hapana. Nitakuwa mtu wa aina gani wa kubadili maneno na
misimamo,”alisema.
Alifafanua kuwa alishasema ukweli anaoujua
hivyo hana sababu ya kuurudia na kwamba kufanya hivyo ni kutafuta
ugomvi. ‘’Yale niliyosema kuhusu suala hilo nimesema mara moja na ni
mara moja tu basi,’’ alisisitiza.
Askofu Pengo aliwataka waamini
na wasio waamini waliomsikia na kukubaliana na aliyosema, kuwa ni
wakati wao kuendeleza taarifa hiyo kwa kusambaza katika sehemu
mbalimbali.
Akirejea habari za kufufuka kwa Yesu, alisema
kusambaza msimamo wake kutaenea kwa watu wengi zaidi kwani ndivyo injili
ya ufufuko wa Bwana Yesu ilivyoenea kwa Petro ambaye awali wakati wa
mateso ya Yesu, alimkana lakini mara baada ya kufufuka alisambaza
taarifa hizo.
Askofu Pengo alisema mashemasi kama
Filipo,Stephano na wengine hawakumwachia Petro kusambaza ufufuko wa
Bwana Yesu ila kila walipokwenda walitamka kuhusu ufufuko na hakukuwa na
haja ya kumuita Petro kuelezea ufufuko huo.
Alisema wasingefanya hivyo injili isingefika duniani kote .
“Hivyo
hivyo wale walioamini niliyosema kuhusu msimamo wangu wa Katiba
Inayopendekezwa, waendelee kusambaza kila wanapokwenda kwa manufaa ya
nchi,” alisisitiza.
Alisema ndivyo inayofundishwa na fumbo la
ufufuko wake Yesu kwa jambo jema halitegemei mtu mmoja kurudia rudia
kwani atakera watu kutokana na kuwapo wanaosikia jambo moja mara kwa
mara.
Askofu Pengo alisema anapoongelea tamko lake kuhusu Katiba
si kwamba anataka kugeuza nafasi ya ibada kuwa mahali pa kutangaza
siasa au shughuli za kijamii, bali neno lolote analofanya ni ukweli wake
na hatobadili.
Alitaka waumini kusimama na kusema potelea mbali
katika kusimamia ukweli wa kile wanachoamini kwa kuwa jasiri bila
kuogopa chochote na kuwa sawa na mtu anayesema liwalo liwe.
Pengo
alisema katika ulimwengu wa sasa, umuhimu wa kutamka ukweli na liwalo
liwe, unazidi kudhihirika kutokana na madai ya nyakati kwani ni muhimu
kwa maaskofu, mapadre na hata viongozi wa serikali kila mmoja ana nafasi
ya kutamka ukweli.
Ugaidi
Aidha, Pengo alizungumzia
tukio la ugaidi nchini Kenya lililosababisha vifo vya watu zaidi ya 147
na kusema hakuna aliyefikiria kuwa Kenya inaweza siku moja kuzingirwa na
watu na kufanyika mauaji yenye msimamo wa imani za dini.
Alisema
ingawa nchi hiyo ilikuwa na malumbano kadhaa, lakini si dini. Alisema
tukio hilo halipendezi si kwa Waislamu wala Wakristo.
“Tumuombe
Kristo atuponye na kutuepusha na balaa hilo, na yasiendelee kutokea kwa
jirani zetu huku kila mmoja akihakikisha kuwa na ujasiri wa kubaki na
msimamo wetu,’’ alisema.
Waraka wa maaskofu Mwezi uliopita
Askofu Pengo wakati akifungua Mafungo ya WAWATA, yaliyofanyika Kanisa
Kuu la Mtakatifu Joseph, Dar es Salaam alikosoa waraka wa maaskofu
kupitia Jukwaa la Kikristo, uliotaka waumini kupiga kura ya hapana kwa
Katiba Inayopendekezwa.
Alisema kuwaamulia ni kuwadharau kuwa hawana uwezo wa kufanya maamuzi sahihi wao wenyewe na kuingilia uamuzi wao.
Awali,
Jukwaa la Wakristo Tanzania liliwataka waumini wake kujiandikisha kwa
wingi katika Daftari la Kudumu la Wapigakura, kuisoma Katiba
Inayopendekezwa na kujitokeza kuikataa kwa kupiga kura ya “hapana”.
Taarifa
hiyo ilisainiwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT),
Askofu Dk Alex Malasusa, Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Katoliki
Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa na Mwenyekiti wa Kanisa
la Pentekoste Tanzania (CPCT), Askofu Daniel Awet.
Waliompinga Pengo
Baada
ya Askofu Pengo kutoa msimamo wake, Askofu wa Kanisa la Ufufuo na
Uzima, Josephat Gwajima alimkashifu na kumtuhumu kusaliti viongozi
wenzake wa Kikristo, kitendo kilichosababisha kukamatwa na kuhojiwa na
polisi.
HABARILEO
-
Blogger Comment
-
Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments :
Post a Comment