Kesi ya wizi wa wanyama hai: Mashahidi waeleza namna Twiga hai walivyotoroshewa nje
Mashahidi
wawili wa upande wa mashtaka, wameieleza mahakama namna wanyamahai,
wakiwamo twiga wanne, walivyosafirishwa kwenda Doha nchini Qatar kwa
kutumia ndege ya jeshi.
Mashahidi hao,
akiwamo mmoja wa madereva wa lori, walitoa ushahidi wao juzi wakiongozwa
na jopo la mawakili watatu wa Serikali, Evetha Mushi, Pius Hilla na
Stella Majaliwa.
Shahidi wa sita,
Davis Kimei aliyekuwa dereva wa lori aina ya Mitsubish Fusso, alieleza
namna alivyosafirisha wanyama hao toka Arusha hadi Uwanja wa Ndege wa
Kilimanjaro (Kia).
Mbele ya Hakimu
Mkazi Mfawidhi, Simon Kobelo shahidi huyo alidai Novemba 25, 2010
alikodishwa kubeba wanyama hao na watu watatu, wakiwemo wawili wenye
asili ya kiasia hadi uwanja wa Kia kwa ujira wa Sh150,000.
“Baada ya
kuelewana tulikwenda hadi kwenye nyumba moja eneo la Kwamrefu, Arusha na
humo ndani nilikuta vijana wengi ambao walikuwa wakitengeneza mabox
yaliyokuwa na Twiga na Swala,” alisema.
Shahidi huyo
alidai baada ya kuwapakia wanyama hao, msafara wa malori manne ulielekea
Kia na kufika saa 8:00 usiku na kuelekea moja kwa moja uwanjani ambapo
walikuta ndege kubwa ya jeshi imeegeshwa.
“Maboksi yale yalishushwa na kupakiwa katika ndege hiyo usiku ule wa manane,” alisema.
Shahidi wa saba,
alidai siku ya tukio saa 4:00 usiku aliwasikia wafanyakazi wawili
uwanjani hapo, wakisema kuna wanyama wangesafirishwa usiku huo.
“Nilimdokeza mkuu
wa upelelezi… Nilipokuwa nyumbani bosi wangu alinipigia simu na
kuniambia ile taarifa niliyompa ilikuwa ni ya kweli kuna ndege ya
Serikali inasafirisha wanyamapori,” alisema.
Shahidi huyo
alidai kuwa saa 6:00 usiku alirudi kazini na ilipofika saa 8:30 usiku
lilikuja basi aina ya Toyota Coaster ambapo walishuka watu wenye sare za
jeshi wenye asili ya kiarabu.
Washtakiwa katika
kesi hiyo inayovuta hisia za Watanzania wengi ni Kamran Ahmed, Hawa
Mang’unyuka, Michael Mrutu na Patrick Paul na kesi hiyo itaendelea
kusikilizwa Agosti 13 na 14.
Kwa hisani ya Mwananchi....kupitia jamii forum
Baadhi ya picha za Doha zoo nchini Qatar.
0 comments :
Post a Comment