-->

BASI LINALOTUMIA KINYESI CHA BINAADAMU LAONEKANA MTAANI NCHINI UINGERZA

Basi linalotumia kinyesi badala ya mafutaUINGEREZA yashuhudia kwa mara ya kwanza katika miji ya Bath na Bristol basi linaloendeshwa kwa nguvu ya gesi inayotokana na kinyesi cha binaadamu pamoja na masalia ya chakula.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, ‘basi kinyesi’ kama lilivyoitwa na wakazi wa Uingereza, lilionekana kwenye mitaa ya miji ya Bath na Bristol.
Basi hilo lina uwezo wa kubeba abiria 40 na linatumia gesi iitwayo biomethane inayozalishwa baada ya kuchakatwa kwenye mabwawa ya majitaka.
Basi hilo lina uwezo wa kutembea mpaka umbali wa kilometa 299 kwa kutumia tenki moja la gesi hiyo, na kiwango hicho cha gesi kinaweza kuzalishwa na watu watano kwa mwaka.
Wahandisi wamesema basi hilo litasaidia kuwa na uwezo endelevu wa kupata nguvu itakayoliendesha kwa ajili ya kusafirisha umma na pia litakuza uimara wa hewa safi.
Gesi hiyo inayosifika kwa kuwa rafiki wa mazingira, kwa kuwa inazalisha kiwango kidogo cha hewa ukaa, inatengenezwa na mabwawa ya maji yanayoangaliwa na kampuni ya GENeco mjini Bristol.
Kiwango chake gesi inayozalishwa, hakichafui hewa tofauti na inavyokuwa kwa aina nyingine ya gesi zinazotengenezwa viwandani kwa kutumia dizeli.
Pia kampuni hiyo imekuwa ya kwanza nchini Uingereza kwa kuzalisha gesi kwa kutumia kinyesi cha binaadamu na mabaki ya chakula, gesi iliyounganishwa kwenye gridi ya taifa ya gesi.
Mohammed Saddiq, Meneja Mkuu wa GENeco, anasema “Kutokana na mabaki ya kinyesi, tumetengeneza gesi ya kutosha ya biomethane na kufanikiwa kuunganisha gesi hiyo kwenye mfumo wa gridi ya taifa kiasi kinachotosha kutumika nyumba 8,500 na kujazwa kwenye mabasi yanayotumia gesi hiyo.
Uchakataji wa majitaka mjini Bristol unachakata mita milioni 75 za ujazo na tani 35,000 za mabaki ya chakula kwa mwaka.
Baada ya uchakataji huo, mita milioni 17 za ujazo za gesi ya biomethane huzalishwa kwa mwaka kiasi ambacho kinatosheleza mahitaji ya takriban nyumba 8,500.
Faida kwa mazingira
Matumizi ya magari yanayotumia gesi yana nafasi kubwa ya kupunguza uchafuzi wa hewa hasa maeneo ya mijini kuliko ilivyo kwa dizeli.
Gesi ya biomethane inapunguza kwa zaidi ya asilimia 97 utoaji wa hewa zenye kemikali hatari ambazo huweza kupenya kirahisi kwenye mapafu ya binaadamu na kuingia kwenye mishipa ya damu.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa wiki za hivi karibuni na mamlaka inayoshughulikia Afya ya Jamii nchini Uingereza, mtu mmoja katika kila watu 20 wanaoishi mijini watapoteza maisha mapema kutokana na kuvuta hewa yenye kemikali hatari.
Matumizi ya gesi hupunguza kati ya asilimia 80-90 ya gesi ya Nitrogen Oxides (NOx) inayosababisha utengenezaji wa mvua yenye asidi na miji yenye ukungu, ambayo ina madhara kwenye ukuaji wa uoto.
Katika kuonyesha matumizi ya gesi asilia ya kinyesi na mabaki ya chakula ni rafiki wa mazingira, utafiti uliofanywa na GENeco unaonyesha hewa ya mkaa (CO2) inayozalishwa hupungua kwa asilimia 95 ukilinganisha na inayozalishwa kwa dizeli.
Kiwango hicho pungufu ya asilimia 95 ya hewa ya mkaa kinazalishwa wakati wa mchakato wa utengenezaji wa gesi hiyo kabla ya kutumiwa kwenye magari yanayotumia gesi na kitaalamu inaitwa well-to-wheels (WTW).
Utafiti huo pia unaonyesha kiwango cha COkinachozalishwa pale gari au mashine inapotumia gesi hiyo ni chini ya asilimia kati ya 20 na 30 chini ya kiwango kinachozalishwa na magari yanayotumia dizeli.
Basi linalotumia hewa ya Haidrojeni
Kabla ya matumizi ya gesi ya kinyesi (au imezoelea zaidi kama biogesi) Uingereza katika jijni la London ilianza kutumia gesi ya Haidrojeni (Hydrogen) kama nishati mbadala na rafiki kwa mazingira.
Mji wa London umekuwa ukitumia teknolojia za kupunguza hewa mkaa kwa kutumia mabasi yanayotumia Haidrojeni (zero emission Hydrogen fuel cell buses) tangu mwaka 2011.
Huu ni mpango wa nchi za Ulaya wa kuwa na usafiri rafiki kwa mazingira (Cleaner Urban Transport for Europe – CUTE).
Kubuniwa kwa teknolojia hiyo mpya Uingereza, kumesababisha mamlaka kutenga barabara mahsusi kwa mabasi hayo; ambayo ni kati ya Covent Garden mpaka Tower Gateway.
Kwa mujibu wa utafiti, zaidi ya vifo 4,300 hutokea kwenye jiji la London kila mwaka kwa sababu ya hewa chafu. Kubuniwa kwa mabasi hayo yatumiayo haidrojeni, ni hatua moja ya suluhisho la tatizo hilo.
Kwa kutumia teknolojia hiyo kinachozalishwa siyo moshi bali ni mvuke wa maji usioweza hata kidogo kuchafua mazingira.
Teknolojia hiyo pia itaepusha uzalishaji wa hewa za Salfa, Nitrojeni na hewa nyinginezo chafu zinazozalishwa na magari yanayotumia dizeli na petroli.
Nguvu ya kuendesha mabasi hayo inatokana na betri kadhaa zinazohifadhi nguvu za umeme uliozalishwa kwa Seli Umeme kama kifaa kinachotumia gesi ya haidrojeni na gesi ya Oksijeni kuzalisha umeme unaohifadhiwa kwenye betri na hatimaye kuweza kutoa nguvu ya kuendesha basi.
Haidrojeni inayozalishwa inahifadhiwa kwenye mitungi minane iliyopo kwenye paa la basi kwa juu na kwa ujumla wake mitungi hiyo ina uwezo wa kuhifadhi kilo 60 za haidrojeni.
Kiwango hiki kinaweza kulifanya basi liweze kutembea umbali wa kilomita 500 bila ya kuongezewa haidrojeni ya ziada.
Mchakato huo wa kuunganisha gesi za Haidrojeni na Oksijeni unazalisha majimaji na hivyo mabasi hayo kumwaga maji badala ya moshi ambao ungeweza kuchafua mazingira kama inavyoonekana kwenye magari ya kawaida yanayotumia dizeli au petroli.
Mabasi hayo pia yanauwezo wa kutengeneza nguvu za ziada zinazohifadhiwa kwenye betri kila basi linapofunga.
Pamoja na uzuri wa mabasi hayo, kuna changamoto kubwa, mojawapo ikiwa ni gharama kubwa ya kununua mabasi hayo, uendeshaji na utunzaji wake. Nchini Canada, gharama za kununua Haidrojeni ni kubwa mara tatu ukilinganisha na dizeli.
Gharama za basi moja kwa sasa, kwa mujibu wa BPS kampuni ya Canada inayojihusisha na utengenezaji wa nishati mbadala miaka mitano iliyopita basi hilo liliuzwa kwa Dola 2.1 milioni , sawa na Sh. 3.3 bilioni.
Gharama hizo ni mara nne ya gharama ya basi la dizeli kwa mujibu wa taarifa hiyo. Hata hivyo gharama zimeshuka kwani kwa sasa katika nchi za Ulaya zimefikia Dola 1.5 milioni, sawa na Sh. 2.4 bilioni.
London ni moja ya miji kadhaa duniani iliyoamua kutumia teknolojia hiyo, baada ya jiji la Madrid, nchini Hispania kuwa la kwanza duniani kwa matumizi hayo mwaka 2003. Jiji la Hamburg nchini Ujerumani, Peth na Reykjavik nchini Iceland yalifuatia.
Kuna miradi mingine mingi katika utengenezaji wa vifaa vinavyotumia teknolojia hiyo kama Haidrojeni iliyopo California, nchini Marekani inayoaminika kuwa kubwa zaidi duniani kwa kuwa na mradi wa utengenezaji wa mashine zinazotumia haidrojeni.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment