Zitto Kabwe akisema jambo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira siku za hivi karibuni. Picha na Maktaba
Dar es Salaam. Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imeiagiza Bodi ya Sukari Tanzania (SBT) kumwondoa katika nyumba ya bodi hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira kutokana na kuishi katika nyumba hiyo kinyume na taratibu.
Wasira akiwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika
alikuwa akiishi katika nyumba hiyo inayomilikiwa na SBT iliyopo Masaki
jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa SBT, Henry Semwaza
aliieleza Kamati ya PAC jana katika kikao kilichofanyika kwenye ofisi
ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam, kuwa wamekuwa wakifanya jitihada za
kuwasiliana na Wasira kuhusu kuirejesha nyumba hiyo, lakini hakuna
utekelezaji wowote unaofanyika.
“Mara ya mwisho tulimwandikia barua mwaka 2012
kuhusu kuirejesha nyumba hiyo, lakini bado hajairejesha na anaendelea
kuishi katika nyumba hiyo,” alisema Semwaza.
Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe akitoa azimio la
Kamati hiyo alisema, “Hapa hakuna msukumo mnaoufanya yaani tangu mwaka
2012 mlipomwandikia barua mpaka sasa kimya. Tunaiagiza SBT kumwandikia
barua Wasira mkimtaka arejeshe nyumba na nakala ya barua hiyo tuipate
Jumatatu (Januari 19 mwaka huu).”
Alisema kutokana na kuwapo kwa harakati za kutaka
kubadili hati ya umiliki ya nyumba hiyo, Zitto alisema, “Msajili wa
Hazina kamati inakuagiza uhakikishe umiliki wa nyumba hiyo unabaki kwa
bodi ya sukari na si vinginevyo.”
Zitto pia alimwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya
Kilimo, Chakula na Ushirika, Sophia Kaduma amwandikie barua Katibu Mkuu
Kiongozi kuhusu uamuzi huo wa Kamati.
Pia, PAC imeishauri Wizara ya Kilimo kuandaa
sheria itakayounda Bodi ya Sukari isiyokuwa na mgongano wa kimaslahi ili
kutoa fursa ya kufanya uamuzi tofauti na ilivyo sasa.
SOURCE:MWANANCHI
0 comments :
Post a Comment