Aliyekuwa mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Kingunge Ngombale Mwiru akiwasilisha mada kuhusu Umuhimu wa Wananchi Kuielewa na Kushiriki katika zoezi la upigaji kura Katiba inayopendekezwa.
Mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale Mwiru, amesema ndoto zake zinaashiria ukoloni unarudi iwapo viongozi watategemea wawekezaji na wataalamu kutoka mataifa ya kigeni kuendeleza sekta ya mafuta na gesi.
Kingunge alisema hayo Dar es Salaam jana, wakati akizungumza kwenye mkutano uliowakutanisha viongozi wa serikali na Jukwaa la Wahariri (TEF), kujadili namna ya kuelimisha wananchi kuhusu katiba inayopendekezwa.
“Hii siyo ndoto yangu Kingunge, kama hakuna tahadhari ipo siku mtashuhudia tena wakoloni wanarudi. Viongozi wasiweke fikra zao kwa wawekezaji na wataalamu wa kigeni katika gesi na mafuta, sisi hatustahili kuwa katika hali hiyo tena ,” alisema Kingunge.
Baadhi ya watetezi wa sera za kutumia wageni kuendeleza gesi na mafuta ni viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini, wanaodai kuwa Watanzania hawana mitaji wala teknolojia ya kuchoronga miamba ya gesi na mafuta ardhini na baharini.
Akielezea suala la uchumi katika mifumo ya katiba za nchi, mwanasiasa huyo ambaye alikuwa mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, alisema tatizo hilo halipo nchini pekee bali Afrika nzima ambako maendeleo na ustawi wa watu
ni duni.
Alisema tabia iliyojengeka ya kutosheka nchi za Afrika ikiwamo Tanzania kwa kuamini wawekezaji na wataalamu wa nje wana uwezo wa kuwainua kiuchumi ni hatari.
Alisema imejengeka dhana kwamba bidhaa bora na wataalamu wanaoweza kubuni na kuunda vitu wanatoka katika nchi za Ulaya na Marekani, huku wataalamu wazawa kazi yao ni ukarabati pekee.
“Bahati mbaya viongozi wetu wamechelewa kutambua na kujiuliza kwa nini tumezidiwa nguvu, imefika wakati misingi ya waasisi wa taifa hili tuifuate kwa kujenga mwelekeo wa nchi unaoleta kujitegemea,” alisisitiza.
Alihimiza kizazi cha sasa kufanya mabadiliko ya kifikra kwa kujikita katika mapinduzi ya sayansi na teknolojia pamoja na kujifunza nchi za Asia ambazo zimekua kwa kasi kiuchumi baada ya kupambana na hatimaye zimeanza kuchuana na baadhi ya nchi za Magharibi kiuchumi.
Aliongeza kwamba kwa mara ya kwanza katiba inayopendekezwa imetoa njia ya kuelekea katika maisha bora kwa kutambua uwapo wa uchumi na kuhakikisha wazawa wanaendeleza nchi yao.
HAMAD NA MUUNGANO
Kwa upande wake, Mbunge wa Wawi (CUF) Hamad Rashid Mohamed, aliwataka wahariri kuwa waangalifu na watu wanaotaka kuuvunja Muungano kwa kutumia mgongo wa katiba inayopendekezwa.
Alisema kuwapo kwa utulivu wa kiutawala katika Visiwa vya Zanzibar ni kwa ajili ya Muungano, vinginevyo hakutakuwa na serikali madhubuti kutokana na vyama vyote kuwa na wajumbe sawa katika Baraza la Wawakilishi.
“Msimamo wangu unabaki kuwa mmoja kwamba anayetaka kuvunjika Muungano ni adui yetu, Zanzibar haina mwenyewe asilia na yote mnayejitokeza na kusema eti imeuzwa na mimi ni dalali ni upuuzi,” alisema hamad.
TUJENGE TANZANIA MPYA
Awali wakati akifungua mkutano huo, Waziri Mukangara alivitaka vyombo vya habari kuelimisha wananchi kwa weledi na usahihi ili kuwasaidia kupiga kura ya maoni wakiwa na ufahamu mpana.
Alisema kura ya maoni inatarajiwa kufanyika Aprili 30 mwaka huu, ambapo inahitajika elimu kwa umma kuwafikia wananchi wengi.
Waziri Mukangara alisema kutumia vyombo vya habari watu wataelewa mambo yaliyokuwamo kwenye katiba hiyo na hatimaye kupiga kura.
Mkutano huo uliandaliwa kwa pamoja na Waziri ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki, na wageni waalikwa walikuwa Kingunge, Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed na aliyekuwa mbunge wa Bunge Maalum la Katiba, akiwasilisha taasisi za elimu ya juu, Dk. Francis Michael.
SOURCE:PAPARAZIHURU
0 comments :
Post a Comment