-->

PATA HABARI NA TUKIO KATIKA PICHA JINSI VURUGU ZILIVYOTOKEA KWENYE MDAHALO WA KATIBA PENDEKEZWA

Katika mazingira ya kutatanisha, siku ya Jumapili vurugu zimekatisha mdahalo uliokuwa ukiendelea kujadili mchakato wa katiba mpya ya Tanzania huku baadhi ya watu wakipigwa na kujeruhiwa.


Mdahalo huo uliokuwa ukitangazwa moja kwa moja kupitia redio na televisheni ulivurugika kutokana na kundi la vijana wapatao 20 kuanza kumzomea aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, alipokuwa akiwasilisha mada yake.
Vijana hao ambao haijajulikana walitokea wapi au walikuwa na ajenda gani waliinua mabango ya kupinga msimamo wa waliokuwa wakiendesha mdahalo na kusema rasimu ya katiba iliyopendekezwa inakidhi mahitaji yote na kusema hakuna haja ya mdahalo.
Jaji Warioba ambaye ni Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania alifanikiwa kutoka nje ya ukumbi ulipokuwa ukifanyika mdahalo huo mjini Dar Es Salaam, lakini wapo watu waliojeruhiwa kutokana na kurushwa viti na vitu vingine.
BBC iliwasiliana na Jaji Warioba apate kueleza yaliyotokea na kama yuko salama baada ya vurugu hizo, lakini aliomba radhi kwa kusema hayupo tayari kulizungumzia swala hilo.
Kiongozi wa kitengo cha hamasa umoja wa vijana CCM (UVCCM), Paul Makonda, aliyekuwepo ukumbini alidaiwa kuhusika na vurugu. Lakini alipoulizwa na BBC kujibu tuhuma hizo Bw Makonda amekanusha kuhusika nazo huku akisema kwamba alihudhuria mdahalo kwasababu ulikuwa wazi kwa kila mtu.
Wakati wa vikao vya Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma, Makonda aliwahi kutoa kauli za kumkebehi Jaji Warioba ambaye tume yake iliandaa rasimu ya iliyokuwa ikijadiliwa na bunge hilo.
Hata hivyo Kamanda wa Polisi mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, aliieleza BBC kuwa hana maelezo ya kutosha na kwamba atalizungumzia akipata taarifa rasmi ya kiofisi.
Tanzania ipo katika mchakato wa kupata katiba mpya. Rasimu iliyodaliwa na kupitishwa na bunge lililosusiwa na vyama vya upinzani inatarajiwa kupigiwa kura na wananchi mwezi Aprili, 2015.
Wachambuzi wa maswala ya kisiasa wameeleza wasi wasi kuwa endapo hakutakuwa na kuvumiliana hali ya kisiasa nchini humo inaweza kubadilika na kuleta ghasia ambazo zinaweza kuepukika.
BBC SWAHILI
Share on Google Plus

About Omari Makoo

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment