Mmoja wa watumiaji wa dawa hizo ambaye hakutaka
kutajwa gazetini kwa kuhofia usalama wake, alisema mtambo huo
umerahisisha upatikanaji wa heroine nchini maarufu ‘white sugar’ kama
inavyojulikana mitaani.
“Zamani ‘white sugar’ ikitoka shamba (nchi
inakotengenezwa yaani Pakistan na nchi nyingine) ilikuwa inapelekwa
Mombasa, Kenya, ambako kuna mtambo wa kuchanganya na dawa nyingine ili
iongezeke wingi wake, lakini kazi hiyo inafanyika hapa hapa nchini kwa
sasa,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu uwepo wa mtambo huo hapa
nchini, Mkuu wa Kitengo cha Kuzuia Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa
alisema kuwa kuna taarifa alizonazo ambazo bado anazifanyia kazi.
“Hata kama nikiwa nazo nazifanyia kazi, za kwangu mimi nazifanyia kazi na hata za kwako nazifanyia kazi,” alisema Nzowa.
Hata hivyo, Nzowa akizungumza katika kipindi cha
Malumbano ya Hoja kilichorushwa na Televisheni ya ITV juzi, alisema kuwa
katika siku za hivi karibuni wafanyabiashara wa heroine wamekuwa
wakiingiza nchini malighafi za dawa hizo, tofauti na awali ambapo
walikuwa wakiingiza dawa hizo zikiwa tayari kwa matumizi.
Akitoa mfano alisema kuna raia wa kigeni
alikamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es
Salaam, akiwa na malighafi hizo zilizokuwa zikifanana na sukari na
kwamba Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Mkemia Mkuu wa Serikali,
ndiyo waliobaini kuwa haikuwa sukari kama ilivyodhaniwa.
Alisema kutokana na uhaba wa dawa hizo bei ya kete
imepanda ambapo hivi sasa hakuna kete ya gramu 0.11 inayouzwa chini ya
Sh 3,000.
Hii ni mara ya pili kubainika kuwepo kwa mtambo wa
kutengenezea dawa za kulevya nchini. Miaka ya hivi karibuni jeshi la
polisi lilikamata mtambo wa kutengenezea dawa za kulevya katika nyumba
moja iliyopo eneo la Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.
Uchunguzi uliofanywa unaonyesha kuwa mbali ya
kuwepo mtambo huo kuna nyumba tano katika eneo la Tandika jijini Dar es
Salaam karibu na soko, ambazo zinatumika kuuza dawa za kulevya huku
baadhi ya polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, wakiwalinda wauzaji wake
kwa kuwapa taarifa ya mipango inayopangwa na jeshi la kuwatia mbaroni.
HABARI NA MWANANCHI
HABARI NA MWANANCHI
0 comments :
Post a Comment