-->

KESI YA SHEKH PONDA YAIGHALIMU SERIKALI SHILINGI MILLIONI 1O

NewsImages/6955262.jpgUsafiri wa helikopta waitafuna dola mara 71 ya gharama ya gari
ULINZI wa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda, akiwa gerezani na anapopelekwa mahakamani, umeanza kuvitesa vyombo vya Dola. Habari zilizolifikia gazeti hili na kuthibitishwa na Kamanda wa Kikosi cha Anga wa Jeshi la Polisi, zinaeleza kuwa serikali juzi ilitumia kiasi cha shilingi 10,682,031 kama gharama za usafiri wa helikopta za kumpeleka na kumrudisha kiongozi huyo mahakamani mkoani Morogoro.

MTANZANIA Jumatano kupitia vyanzo vyake vilivyoko ndani na nje ya Jeshi la Polisi, limedokezwa kuwa gharama za kurusha helikopta kwa dakika 45 hadi saa moja ni dola za Marekani 3,000 hadi 3,300 ambazo ni sawa na shilingi 5,341,032.85 .

Hivyo gharama za kwenda na kurudi kwa saa jumla yake ni dola za Marekani 6,600 ambazo ni sawa na shilingi 10,682,031.

Akithibitisha hilo, Kamanda wa Kikosi cha Anga wa Jeshi la Polisi, Antony Mwami alisema gharama za kurusha helikopta kwa dakika 45 ni dola 3,000 ambazo ni sawa na shilingi milioni tano.

Katika uchunguzi wake gazeti hili limebaini kuwa gharama hizo zilizotumika kwa siku moja tu, zingetosha kumsafirisha Ponda kwenda Morogoro na kurudi mara 71, endapo ungetumika usafiri wa gari wa kawaida.

Gazeti hili limebaini kuwa kwa usafiri wa kawaida wa gari, gharama za kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro hazizidi shilingi 150,000.

Juzi Jeshi la Polisi kwa kutumia helikopta yake inayodaiwa kuwa na uwezo wa kubeba watu wanane, lilimsafirisha Sheikh Ponda hadi mkoani Morogoro ambako alipandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi na kusomewa mashtaka ya uchochezi yanayomkabili.

Sheikh Ponda aliwasili kwa helikopta hiyo na kutua kwenye uwanja wa gofu, Morogoro akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi na alipakiwa tena kwenye gari maalumu ambalo liliongozana na mengine matatu ya polisi kuelekea eneo la mahakamani.

Baada ya kumalizika kusomwa kwa kesi hiyo, msafara ule ule ulimrejesha uwanja wa gofu saa sita mchana na kupandishwa tena kwenye helikopta kurejea jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, gharama hizo zinazozidi shilingi milioni 10 ni zile za helikopta tu, mbali na nyingine zikiwemo posho pamoja na magari yaliyotumika kumsafirisha wakati alipotua na kurudi katika uwanja wa gofu.

MTANZANIA Jumatano limedokezwa kuwa ndani ya Jeshi la Polisi, rubani anayerusha helikopta kwa muda wa saa moja, hulipwa kuanzia shilingi 100,000.

Kwamba helikopta iliyotumika kumbeba Ponda, hubeba watu wanane kwa maana ya marubani wawili na abiria wengine sita.

Hata hivyo gazeti hili limedokezwa kuwa, kwa askari ambao wanasindikiza mahabusu kama watalala wanakokwenda, hulipwa posho na kama hawalali hawalipwi.

Katika tukio la kumsindikiza Ponda hawakulala, hivyo hawakulipwa chochote.

Wakati hayo yakijitokeza, Gazeti hili kupitia vyanzo vyake vya habari vilivyoko ndani ya Jeshi la Polisi, limedokezwa kuwa hatua ya Ponda kusafirishwa kwa helikopta ilitokana na uamuzi wa baadhi ya viongozi wa juu wa Jeshi hilo walioko Dar es Salaam na wale wa Morogoro.

Inaelezwa kuwa viongozi hao walifikia uamuzi huo, baada ya kudai kuwapo kwa taarifa za kiintelijensia za kuwapo kwa tishio la usalama wa nchi endapo Ponda angesafirishwa kwa njia ya kawaida.

Juzi Ponda alianza kwa kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam na kufutiwa mashtaka ya uchochezi yaliyokuwa yakimkabili, baada ya kusomewa mara ya kwanza Agosti 14 mwaka huu akiwa kitandani katika Taasisi ya Mifupa ya Hospitali ya Muhimbili, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kumshitaki.

Alidaiwa kutenda makosa hayo katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano kati ya Juni 2 na Agosti 11 mwaka huu.

Ponda alifikishwa mahakamani hapo saa 12 asubuhi na baadaye alipandishwa kizimbani na kufutiwa kesi hiyo baada ya Wakili Kweka kuwasilisha hati hiyo ya DPP chini ya kifungu cha 91 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

Baada ya kufutiwa mashtaka hayo, alichukuliwa na kupelekwa Morogoro ambako pia alisomewa mashtaka ya uchochezi.
SOURCE:MTANZANIA
Share on Google Plus

About Omari Makoo

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment