Na Mwandishi Wetu
WATANZANIA
ambao idadi yao inaweza kupita mamia, wameshanyongwa nchini China
kutokana na kupatikana na hatia ya kujihusisha na biashara ya madawa ya
kulevya.
Ripoti
maalum ya madawa ya kulevya, iliyofanyiwa kazi na gazeti hili kwa
kukusanya taarifa ndani ya nchi, Afrika Kusini na China kwenyewe,
inaweka hadharani siri ya mamia ya Watanzania kunyongwa.
Katika
ripoti hiyo, inaonesha kwamba mataifa ya Afrika Kusini na Uganda, yapo
mstari wa mbele kuripoti taarifa za raia wao kunyongwa China lakini
Tanzania imekuwa ikisuasua.
“Huu
ukimya wa serikali yetu, unafanya wengi kukosa taarifa sahihi, matokeo
yake wanajiingiza kwenye biashara hiyo haramu ambayo mtu akikamatwa tu
China na akikutwa na hatia lazima anyongwe,” alisema Joel Mabruki,
mfanyabiashara wa nguo na simu kati ya Tanzania na China.
Mabruki
aliongeza: “Kama serikali yetu ingekuwa na utaratibu wa kutangaza kila
Mtanzania anayenyongwa China, pengine vijana wengine wangeogopa na
baadhi yao wangeacha kabisa. Hivi sasa idadi inaongezeka kwa sababu
hawaambiwi ukweli.”NA GLOBAL PUBLISHER
KITENGO CHA MADAWA YA KULEVYA KINAJUA
Kwa
mujibu wa Mkuu wa Jeshi la Polisi, Kitengo cha Kuzuia na Kudhibiti
Madawa ya Kulevya, Godfrey Nzowa, ofisi yake inazo taarifa kuhusu
Watanzania kunyongwa China lakini akatupa mpira kwa Mkurugenzi wa Kuzuia
na Kudhibiti Madawa ya Kulevya, Christopher Shekiondo.
“Kuhusu
idadi na majina, hilo suala aulizwe mkurugenzi. Ila ukweli ni kwamba
Watanzania wengi wanakamatwa China na wananyongwa,” alisema Nzowa.
MAAFA PAKISTAN
Kwa
upande mwingine, Nzowa alisema kuwa watu wanaizungumzia sana China
lakini ukweli ni kwamba nchi nyingine ambayo inanyonga Watanzania wengi
ni Pakistan.
Nzowa
alisema kuwa pengine taarifa za Pakistan hazipatikani sana kutokana na
mwingiliano wa Tanzania na nchi hiyo, tofauti na China ambayo Watanzania
wanakwenda na kurudi kila siku iendayo kwa Mungu.
“Tunaposema
madawa ya kulevya ni janga kubwa inafaa ieleweke hivyo. Watanzania
wanaonyongwa China na Pakistan ni wengi sana. Tuwe makini juu ya hili na
tuzingatie kwelikweli,” alisema Nzowa.
TAARIFA ZA MITANDAO YA KIJAMII
Tofauti
na mataifa mengine ambayo ripoti za raia wao kukamatwa na kunyongwa
China hutolewa rasmi na balozi zao, hapa Tanzania, habari huenezwa na
mitandao ya kijamii.
Mfano;
mitandao ya kijamii ndiyo pekee iliyoripoti kuhusu kunyongwa kwa mrembo
mwanamitindo (jina tunalo) aliyeshiriki video ya wimbo Twende Zetu wa
mwanamuziki Saidi Juma ‘Chegge’, aliyewashirikisha Amani James Temba
‘Mheshimiwa Temba’, Feruzi Mrisho Rehani ‘Ferouz’ na Yessaya Ambilikile
‘YP’.
Vilevile,
alipokamatwa aliyewahi kushika nyadhifa za makamu mwenyekiti na katibu
msaidizi kwenye Klabu ya Simba (jina tunalo), mitandao ya kijamii
iliandika bila serikali kutoa tamko rasmi.
Hata
hivyo, kutokana na kukosekana na taarifa rasmi kutoka serikalini,
mitandao ya kijamii ilitoa habari zenye kushitua, nyingine ikidai mtu
huyo aliyewahi kuwa kiongozi wa Simba alifungwa miaka 70 jela, nyingine
ikieleza kwamba tayari alishanyongwa.
MWAKALEBELA ATOA USHUHUDA WAKE
Katibu
Mkuu Mstaafu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Frederick
Mwakalebela, alipozungumza na gazeti hili, alisema kuwa kati ya mwishoni
mwa mwaka 2009 na mwanzoni mwa 2010, alikwenda China katika safari ya
kikazi.
“Nikiwa
kule, niliambiwa taarifa za Watanzania wengi ambao walinyongwa baada ya
kukutwa na hatia ya kujishughulisha na biashara ya madawa ya kulevya,”
alisema Mwakalebela.
Alipoulizwa
kuhusu kiongozi huyo wa Simba, Mwakalebela alijibu: “Nikiwa China
niliambiwa amenyongwa. Niliporudi hapa nchini ndiyo nikasikia amefungwa
miaka 70.”
Mwakalebela
aliongeza: “Ukweli ni kwamba kwa taarifa nilizopata nikiwa China,
Watanzania wengi sana wananyongwa kwa sababu ya madawa ya kulevya.
Naweza kusema ni mamia. Ikiwa kwa muda mfupi niliokuwepo pale nimeambiwa
karibu watu 10, je mwaka mzima inakuwaje?”
WENGINE WANAPONZWA NA WANIGERIA
Mfanyabiashara
Mtanzania, Hashim Rau, ambaye hufanya biashara zake kati ya Tanzania,
Afrika Kusini na China, alisema kuwa kuna Watanzania walinyongwa baada
ya kuponzwa na Wanigeria.
Rau
alisema, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa O. R. Tambo, uliopo nje kidogo
ya Jiji la Johannesburg, umewasababisha matatizo Watanzania wengi
kutokana na tabia yao ya ukarimu.
Alisema:
“Mtanzania anaweza kutoka na biashara yake kuja kuuza Afrika Kusini,
baada ya hapo anapanda ndege ya moja kwa moja kwenda China. Akiwa uwanja
wa ndege anakutana na Mnigeria muuza madawa ya kulevya.
“Mtanzania
anakuwa hana mizigo mingi, kwa hiyo yule Mnigeria anamwomba Mtanzania
amsaidie kupitisha begi lake moja kwenye mzani, akidai kuwa yeye mizigo
yake ni mingi, anaogopa atatozwa fedha nyingi.
“Kumbe
lile begi linakuwa na unga. Sasa Mtanzania kwa kutojua, atakubali, baada
ya hapo lile begi litaandikwa jina la Mtanzania. Mbele ya safari kama
litavuka salama, Mnigeria atamshukuru Mtanzania na kuchukua begi lake
lakini likikamatwa, Mnigeria atakimbia, Mtanzania atabaki na mashtaka
ambayo mwisho wake ni kunyogwa China.”
Akisimulia
ushuhuda wake, Rau alisema kuwa aliwahi kuombwa msaada wa aina hiyo na
Mnigeria mmoja lakini alipotaka kukagua begi lina nini ndani alikataa.
“Alipokataa
nikague ndani ya begi kuna nini nami nikamkatalia kumsaidia kwa sababu
naujua mchezo wao. Sasa pale uwanjani alikuwepo Mtanzania mwingine
mwenye asili ya Tanga (jina tunalo), alipoombwa na yule Mnigeria
alikubali.
“Nilijitahidi
kumwonesha ishara hakunielewa, mwisho nikamwambia asikubali lakini
hakunielewa. Tulipofika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Guangzhou
Baiyun, China, yule Mtanga alikamatwa baada ya lile begi kukutwa na
madawa ya kulevya mchanganyiko wa heroine, cocaine na methamphetamine.
“Kama
kawaida, yule Mnigeria alitoweka. Mimi niliujua ule mchezo lakini
nilijiweka pembeni kwa sababu ningejionesha najua chochote au namtambua
yule Mtanga ningeshikiliwa. Tena pengine na mimi ningekuwa
nimeshanyongwa siku nyingi zilizopita kwa sababu hiyo ni kesi ya mwaka
2008.
“Watanzania
wajue kwamba China hakuna mchezo, hawana muda wa kufuatilia ushahidi,
ukikutwa na unga, ikithibitika hivyo, kwao huo ni ushahidi tosha kwamba
wewe ndiye mmiliki na unanyongwa,” alisema Rau.
PEMBE TATU HATARI
Uchunguzi
wa gazeti hili kwa kufanyia kazi matukio ya Watanzania kukamatwa na
madawa ya kulevya, umebaini kuwa pembe tatu hatari imetengenezwa na
wauza unga katika nchi za Tanzania, Afrika Kusini na China.
Imebainika
kwamba wafanyabiashara wa madawa ya kulevya, wamekuwa wakisafirisha
idadi kubwa ya madawa hayo kwenda Afrika Kusini ambako husafirishwa kwa
mafungu kwenda China.
Ripoti za
hivi karibuni, zinaongeza nguvu katika madai kwamba Tanzania na Afrika
Kusini, kuna udhaifu mkubwa wa udhibiti wa madawa ya kulevya ndiyo maana
wafanyabiashara huingiza na kusafirisha mizigo mikubwa kwa urahisi.
Kutokana
na hali hiyo, wafanyabiashara hao husafirisha madawa ya kulevya yenye
uzani mkubwa tena kupitia katika viwanja vya ndege kisha kuziweka katika
mafungu madogomadogo kwenda China na kwingineko ambako mahitaji ni
makubwa na bei ni nzuri.
Uchunguzi
umebaini kuwa sheria kali za China za kudhibiti madawa ya kulevya,
zinasababisha uhaba mkubwa wa mihadarati ndani ya nchi hiyo, kwa hiyo
anayefanikiwa kupitisha, huuza kwa bei kubwa sana.
WATUMWA WENGI NI WANAWAKE
Mwanamke,
Janice Bronwyn Linden, 38, raia wa Afrika Kusini, alinyongwa China
mwaka 2011, baada ya kukutwa na hatia ya kusafirisha madawa ya kulevya
aina ya methamphetamine yenye uzito wa kilogramu tatu.
Nobanda
Nolubabalo, 23, raia wa Afrika Kusini, alikamatwa Uwanja wa Ndege wa
Suvarnabhumi, Bangkok, Thailand, akiwa ameficha cocaine zenye uzani wa
kg 1.5.
Watanzania,
Agnes Gerald na Melisa Edward, hivi karibuni walikamatwa Afrika Kusini,
wakiwa na mzigo wa madawa ya kulevya aina ya methamphetamine, yenye
thamani ya shilingi bilioni 6.8.
Mtanzania
mwingine, Sharifa Mahmoud, yupo nchini Misri akisubiri adhabu ya
kunyogwa, baada ya kukutwa na hatia ya kuingiza nchini humo, madawa ya
kulevya aina ya heroine.
Saada
Ally Kilongo, ni mwanamke mwingine wa Kitanzania ambaye hivi karibuni
alikamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, Dar es
Salaam, akiwa na madawa ya kulevya aina ya methamphetamine yenye thamani
ya zaidi ya shilingi milioni 170.
Zahra
Thomas, kutoka Visiwa vya Sao Tome, alikamatwa mwaka jana, Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Hong Kong, akiwa na mzigo wa heroine wenye uzito
wa kilogramu 12.
Mnigeria, Helen Okechukwu, alinaswa Falme za Kiarabu akiwa na madawa ya kulevya aina ya cocaine, uzani wa kg 20.
Mifano
hiyo, inatosha kuonesha jinsi wanawake wanavyotumiwa na wauza unga
kusafirisha mizigo yao kwa imani kwamba mwanamke ni rahisi kupita sehemu
za ukaguzi bila kushtukiwa, vilevile kukwepa dhuluma.
MSEMAJI WA POLISI
Msemaji
wa polisi nchini, Advera Senso, aliliambia gazeti hili wiki iliyopita
kuwa Watanzania wengi wananyongwa China kwa sababu ya hatia ya
kujihusisha na biashara ya madawa ya kulevya.
“Majina ya wahusika kwangu hayapo. Ila nafahamu kuwa wengi wananyongwa,” alisema Senso.
NI SIRI KUBWA
Habari zinasema kuwa mara nyingi utekelezaji wa adhabu ya kifo China ni siri lakini ubalozi wa Tanzania hujulishwa.
“Ila mara
nyingi wauza madawa ya kulevya husababisha mkanganyiko wa uraia
kutokana na kuwa na hati hata tatu, hii husababisha ubalozi wa Tanzania
China ubaki na siri ya mtu aliyenyongwa bila kujulishwa ndugu zake,”
kilisema chanzo chetu na kuongeza:
“Ikitokea
ndugu wanaulizia hapo hupewa taarifa kamili kuhusu taarifa za ndugu yao
kama ameshanyongwa au bado anatumikia kifungo.”
Chanzo
chetu kilibainisha kuwa mbali na kunyongwa, vilevile hutokea vifo vya
kimafia, kwani wauza unga huuana wao kwa wao ili kudhulumiana.
“Ikitokea mtu ameuawa, taarifa zikifika ubalozini, zinafuatiliwa lakini kama hazieleweki hubaki siri,” kilisema chanzo.
STORI YA MKUMBUKWA
Aprili
mwaka jana, kijana wa Kitanzania, Mkumbukwa John Shayo, aliuawa China na
maiti yake ilikaa mochwari mwaka mzima, kabla ya kuletwa nchini mwaka
huu na kuzikwa mkoani Mwanza.
Mkumbukwa, anasadikiwa kuuawa na mtandao wa wauza madawa ya kulevya, ingawa haijulikani sababu yake ni nini.
TUNACHUNGUZA
Gazeti
hili linaahidi kupita kila panapotakiwa ili kukamilisha orodha kamili ya
Watanzania walionyongwa China kisha ripoti hiyo, tutaichapisha katika
matoleo yajayo.
CHINA YAONGOZA KWA KUNYONGA
Chati
iliyopo ukurasa wa kwanza ni takwimu za Shirika la Kimataifa la Haki za
Binadamu, Amnesty International mwaka jana ambayo inaonesha kwamba China
ndiyo kinara wa kunyonga watu duniani ambapo inanyonga maelfu kila
mwaka kwa makosa mbalimbali ikiwemo kusafirisha madawa ya kulevya,
ikifuatiwa na Pakistan na Falme za Kiarabu.
About Omari Makoo
0 comments :
Post a Comment