Kufuatia
kauli za Serikali magazetini kuhusu mimi na kodi ya umiliki wa kadi za
simu; nijibu tu kwa ujumla kwamba SITAACHA. Badala yake naomba kuwapatia
namba zao: Makamba 0767783996 na Mgimwa 0754/0684765644, tunachohitaji
ni kauli ya Serikali kuwa kodi imesitishwa na itaondolewa na sio siasa
chafu.
Kwa mliotaka msimamo wangu juu ya kauli ilinukuliwa
jana tarehe 18 Julai 2013 na Gazeti la Majira kwamba Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Januari Makamba kwamba “Mnyika
anaangalia upepo unakoelekea, akiona watu wanalalamika ndipo anaongea
namsihi aache kufanya siasa katika jambo hili”, naomba kutumia mtandao
huu kutoa majibu ya ujumla kwa maswali na masuala yote kama ifuatavyo:
Nieleze kwamba sitaacha kufanya siasa kwenye jambo hili mpaka kodi hiyo
itakapofutwa kuwawezesha wananchi wa kipato cha chini kubaki na fedha
walau kidogo kwa maendeleo.
Sitaacha kufanya siasa kwa sababu ndio
kazi yangu ambayo wananchi walinichagua kuifanya ya kuwawakilisha na
kuisimamia Serikali ambayo yeye Makamba ni sehemu yake. Sitaacha kufanya
siasa kwa sababu Mwalimu Nyerere alisema ili nchi yetu iendelee
inahitaji watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.
Ambacho
sitafanya ni siasa chafu kama hizo ambazo Makamba amefanya za kusema
uongo, kwa kuwa naamini anafahamu kabisa kwamba sijaanza kuongea kuhusu
suala hili baada ya malalamiko ya wananchi bali jambo hili nilianza
kulishughulikia bungeni mara baada ya Waziri wa Fedha kuwasilisha
jedwali la marekebisho la kuanzisha kodi lukuki za simu ikiwemo hii.
Katika mchango wangu bungeni, nieleza kwamba muswada huo wa sheria ya
fedha kwa kupandisha kodi kwenye mafuta na simu ni ‘muswada wa majanga
ya kuwaongezea mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi.
Aidha,
sikuishia kusema tu kwa niaba ya wananchi bali nilichukua hatua kwa
mujibu wa kanuni za Bunge nami kuwasilisha jedwali la marekebisho ya
kupinga kodi ya umiliki wa kadi za simu pamoja na kodi nyingine zote
zenye kuongeza mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi sio kwenye sekta
ya mawasiliano bali pia kwenye sekta zingine ikiwemo sekta ndogo (sub
sector) nyeti ya mafuta.
Mlioniuliza kwa SMS katika simu na
kwenye mitandao ya kijamii sasa ni wakati wa Makamba kuhojiwa kwa njia
hizo hizo (Simu yake ya Mkononi ni 0767783996) kwa kuwa yeye ni sehemu
ya Serikali na Serikali ndiyo ambayo iliingiza suala hili kwa mara ya
kwanza ndani ya ukumbi wa Bunge kupitia hotuba ya Bajeti Serikali na
ikalirudia kuliingiza kupitia jedwali la marekebisho ya Sheria ya
Serikali; ni wakina nani hasa kwa majina ndani ya Serikali na Bunge
walioingiza kodi hii? Na ni wakina nani hasa waliopigia kura ya ndio
kuipitisha?
Aidha, amenukuliwa na gazeti la Mwananchi la leo
tarehe 19 Julai 2013 akieleza kwamba hakubaliani na suala hili na kupita
kwake ilikuwa na kuzidiwa nguvu. Hivyo, ataje kwa majina hayo waliozidi
nguvu serikali kinyume na matakwa yake. Amenukuliwa akisema pia kwamba
anajua kuwa suala hili haliwezi kutekelezwa na kwamba ni lazima
litabadilishwa kwa kuangalia eneo lingine la kutoza kodi. Ni vizuri
akahojiwa, ikiwa huo ni msimamo wa Serikali; mwenye mamlaka ya kusitisha
kodi hiyo ni nani na kwanini hajitokezi kutoa agizo la kusitisha wakati
maandalizi yakiendelea ya kupeleka muswada bungeni wa kuifuta kabisa
kodi hiyo katika mkutano ujao?
Wakati Naibu Waziri akisema
hayo, Waziri wa Fedha Dk William Mgimwa katika Serikali hiyo hiyo yeye
ametoa kauli tofauti siku hii hii ya leo ambapo kwa mujibu wa gazeti la
Mtanzania amewataka watumiaji wa mitandao ya simu nchini na watanzania
kwa ujumla kuwa na subira kuhusu tozo ya sh 1000 kwa mwezi kwa kila
laini ya simu za kiganjani.
Na kwa kuwa amesema kwamba Serikali
inaendelea kupokea maoni kutoka kwa wadau, natoa mwito kwa wananchi
kumtumia maoni kupitia namba zake za simu za mkononi 0754/0684-765644.
Aidha, ni vizuri aeleze subira hiyo ivutwe mpaka lini? Na ni wakina nani
hasa kwa majina waliomfanya akaingiza kodi hiyo katika kitabu cha
Hotuba yake aliyosoma bungeni kuhusu bajeti ya Serikali na wakina na
hasa kwa majina waliomfanya arejeshe kodi hiyo ya kadi za simu kwenye
jedwali la marekebisho ya muswada wa sheria ya fedha alilowasilisha
bungeni.
Nasisiza kuwa kauli za ujumla za Serikali bila
kuwataja kwa majina wahusika ni za kujivua mzigo wa lawama baada ya
malalamiko ya wananchi kuhusu kodi hii na nyinginezo kwa kuhamisha mzigo
huo kwa wabunge. Ni muhimu badala ya kutoa kauli za ujumla za kulaumu
wabunge, Rais ama kiongozi mwingine mwenye mamlaka ajitokeze kusitisha
kutozwa kwa kodi hiyo na kuanzisha mchakato wa muswada wa kufuta kodi
hiyo kuwasilishwa katika mkutano wa Bunge unaotarajiwa kuanza tarehe 27
Agosti 2013.
Majina ya wahusika yasipotajwa au mamlaka
zinazohusika zisipotoa kauli katika mkutano wa hadhara nitakaoshiriki
jumapili tarehe 21 Julai 2013 katika Uwanja wa Sahara kata ya Mabibo
kuanzia saa 8 Mchana mpaka saa 11 Jioni nitatoa mrejesho kuhusu
yaliyojiri katika mkutano uliopita wa Bunge na kueleza hatua zaidi
zinazopaswa kuchukuliwa kuwezesha majina ya wabunge hao kutajwa
hadharani na hatua za kuondoa kodi hiyo kuchukuliwa.
Uongozi
bora na uraia mwema wenye uwajibikaji ni chimbuko na chachu ya ukuaji
endelevu wa uchumi wa nchi na ustawi wa maisha ya wananchi. Twende kazi.
John Mnyika (Mb)
19 Julai 2013
About Omari Makoo
0 comments :
Post a Comment