-->

MILA HII MILA GANI?????????



                  
   MILA HII MILA GANI?
1.      Bismilahi jaliyani, kwa jinale la kuwata,
            Katumbasi hakiyani, kwa shairi najikita,
             La ndoa nawahojini, majibu nayatafuta,
             Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
2.       Tunaishi minazini,  kwa umoja bila vita,
              Kwa zetu mila za dini, ni zetu ndizo sifata,
              Ila sasa shangazwani,  majibu bila kupata,
             Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
3.      Barobaro mefikani,  kijana ndoa kufata,
            Binti naye yu radhini, tuanze yetu maisha,
            Pingamizi subiani,  nimebaki mebuhita,
           Mila hii milagani?  Namtata nauliza.
4.      ’Kijana wafanya nini,  binti yetu kumfata,
             Kwenu kwako waishini,  au la nyumba matata,
             Utabaki minazini, magomeni kutofata”,
             Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
5.      ”Kijana wamilikini,  kwa maswali wakung’ata,
              pikipiki ama gani ,  chako kipato kuteta,
             Tueleze kwa makini, wetu binta takamata”,
             Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
6.      ‘Bara au  pembezoni,  kijana wapi mekita,
              Kama  ni unyamwezini,  hutopata wetu binta,
              Hatutaki pelekani,  kwa golo kijana pita,’
              Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
  
7.     Mila hii mila gani ,  mbona kwani mwatukata,
           Kwa ukubwa atharini , vijanenu twashimita,
          Kapata jiko chogoni ,  mwanikata na manyota,
          Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
8.      Shemegi wa ukatani , na thamani hutopata,
         Kuingia qabulini , kwa mahali hutopita,
       Tunataka milioni,au samani taleta,’
          Mila hii mila gani? Namtata nauliza.
9.      Wenu wingi maharini, siyo Baraka kupata,
          Kuishi kwenu ziwani, sifasiriwe ni tata,
          Muogopeni manani, kuziniwa wenu binta,
         Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
10.    Siwatii lawamani, kwa nasaba kujisuta,
         N’tokako mahameni, ili mujue kupata,
         Unasaba arabuni, sasa acheni lanata
        Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
11.   Kijana nazeekani ,barazani mejikita,
        Ishirini thalathini , arobaini napita,
       Si mvivu si muhuni, kiniponzacho ukata,
       Mila hii mila gani, Namtata nauliza.
12.  Binti nae lalamani, na utawa  kishapata,
     Ami yako subirini, wa Dubai hatosita,
      Olewa sikubalini, na mtu aso wa bata,”
      Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
13.  Rasuli tumuigeni, mtumetu masumita,
      Hakujali arabuni, ambao si twajiita,
      Kwa rangie kujubuni, kiburini kujiita,
      Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
14.  Mitendeni pembezoni, haweshani kujiteta,
        Kwa ubora nasabani, vote hivi vinanata,
        Ni mimi wa magomeni,  na sitokei tegeta,
        Mila hii mila gani?  Namtata nuliza.
15.   Upotevu tuacheni, ujingani biringita,
        Vijanenu tazameni, miji mambo wanofata,
        Wanenu haribiwani, nao pia wajikita,
        Mila hii mila gani? Namtata nauliza.
16.   Mambo yao fanyiwani,  tazimia kwa kujuta,
        Hii yote kutunzani, heshimae sijepita,
        Na janga waokoeni, jinamizi linapita,
        Mila hii mila gani, Namtata nauliza.
17.   Fedheha tatawalani, iwapo mato fumbata,
        Mashariti punguzeni, na vikwazo kuvifuta,
        Ya msingi yawekeni, na vijana kuyapata,
        Mila hii mila gani? Namtata nauliza.
18.   Sidhalilishetu dini, kwa machafu mwaitita,
         Mwajitia lawamani, jiandaeni kujuta,
         Ozesheni oaneni, na vizazi vije peta,
         Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
19.   Ni hakika linichusha, hata mkanitapisha,
         Kwa mahali ya kutisha, kwayo sitawasafisha,
         Kwa hili mulo jivisha, ni kipi mwatufundisha,
         Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
20.     Lipofika liniteta, na mshenga nilileta,
          Ni wa bara  si mvita, ni kule kwa bwana pita,
           Linena bila kusita, qabulini hitapita,
           Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
21.    Samani sitazikidhi, ni sana naja waudhi,
         Saba ulufi naridhi, tusemeni si maradhi,
          Ngetaka ngenda kwa kadhi, kini meola sokidhi,
          Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
22.    Na chini linikalisha, seluni na kunivisha,
         Maombi kuwasilisha, kwa hoja mulinitisha,
         Lengo kutofanikisha, la ndoa kulikwamisha,
         Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
23. ” Mwerevu moja akaja, na kutoa ushauri,
      “Tumozesheni mseja, kuepusha na ushari,
       Tukizingatia mkaja, ni mambo yaso mazuri,
      Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
24. ‘Anapokuja kapela, muradhini kwa diniye,
     Muozesheni msela, na dini yake timiye,
      Ondoeni nayo mila, na mola aje ridhiye,’
      Mila hii mila gani, Namtata nauliza.
25.  ‘Ndo mtume katufunza, juu ya dini kutenda,
        Tusiwe kama mafunza, kwa miguu kuipenda,
        Tulienzi letu chenza, lisije kwetu kuvunda,’
         Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
26. ‘Na machungwa yalochungwa, chongalinji hakuchonga,
       Tusichunge yaso chungwa, sije tukala mchunga,
       Tukasema yalipangwa, kumbe twajipiga panga,’
        Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.       
27.   ‘Nawasia ndugi zangu, tuondoe matabaka,
         Radhi nayo yake mungu, pate nasi kutufika,
         Vijana wache uzungu, na vigingi kutoweka,’
         Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
28.    Kwa busara lika chini, kwayo mengi alonena,
         Ni kikao cha chukwani, kilifika  kwa mchina,
          Bada  hoja za mneni, lifuata za wanena,
          Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
29.    Pingamizi za wajomba, kwa kugomba zilifata,
         Walisema kwa kugomba, na kule kwao kunata,
     Ami yake “kwa kasumba,”ndilo jikole kupata,
       Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
30.    Shangazi nae simama, kuiunga hoja yake,
      Kwahiyo yako hekima, tatufanya tuondoke,
        Tumekuja kulisema, kijana wetu sondoke,’
         Mila hii mila gani? Namtata nauliza.
31.   ‘Nikiwa kama shangazi, nahitaji haki yangu,
         Na mkaja no ni kazi, ridhie mtimaangu,
         Kukulea ndio kazi, ni jukumu lilo langu,’
        Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
                                                                   
32.    Mama yako kanituma, Asumini nisikie,
         Ahitaji ilo nema, na si mradi ufike,
        Utatupa na lawama, na kwetu sifikirike,
        Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
33.  Yatilie akilini, kwa haya nayokwambia,
        Sijitose baharini, sababu unakimbia,
        Kumpenda Muhidini, wa bara nakuambia,’
        Milahii mila gani?  Namtata nauliza.
34.    Kikao kilinisuta, tena mbele ya hadhira,
         Muhidini lijikuta, nimeipoteza dira,
        Sikupakwa ta mafuta, angalau iwe nura,
        Mila hii mila gani? Namtata nauliza.
35.  ‘Asumini jina langu, ninahitaji olewa,
       Ni sitara ilo kwangu, nawahitaji elewa,
       Ni chaguzi lilo langu,  silazimishwi olewa,’
       Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
36.   Sihitaji ubaguzi, nilisema ninasema,
        Nitasema kichaguzi, bila hata ya kuhema,
         Nimepata ufunguzi, kuolewa kulo nema,’
         Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
37.  ‘ Nimeola tangu tangu, Muhidini ninapenda,
         Naomba awe mewangu, nahitaji mziwanda,
         Hili ndilo semo langu, na ndo kwake nishapenda,’
         Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
38.  ‘ Na kwangu munasegana, ama kweli tahizika,
        Nimekita nimebuna, kwa hili tasiwijika,
        Hamkani  nafusina, mtimau watirika,’
        Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
39.  ‘ Wangu wazazi mnani, kuzuwia Yasimini,
         Dini ni wake simini, kedikedi ni za nini,
         Seleleya nafusini, taingia na simani,’
         Mila hii mila gani? Namtata nauliza.
40.   ‘ Niko radhi natamka, kwa zenu hila tapinga,
         Nihurumeni tawika, kwa siku nyingi napinga,
         Ni mwaka wangu mefika, kufika huko Mafinga,’
         Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.      
41.   ‘ Ufiriti munolea, tahiliki nawambia,
         Asimini jisemea, kwa Dini mejichimbia,
         Kwakeye nimezowea, kwake hunisabilia,’
         Mila hii mila gani ? Namtata nauliza.
42.    Jamani nipeni jiko, acheni kunibagua,
         Msinipige  kiwiko, kijiweni nasugua,
         Yasimini langu jiko, na wenyewe mwatambua,
         Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
43.   Hivi sasa natambua, ile kauli ya Juma,
        Alivo kwisha tambua, kwa kule kwake kulema,
        Alinyimwa kuchukua, jiko lisilo kilema,
       Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
44.   Kiembe mbuzi n’kwao, hadi sasa hana hamu,
        Thalathini na mitano, arobaini sawamu,
        Kazikosa na nderemo, kwa mashariti magumu,
        Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
45.    Leta vitanda viwili, na kabati taijaza,
         Magodoroyo mawali, kulipamba lako chenza,
         Sisahau tasiwili, jitazama wako mwenza,
         Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
46.   Alishindwa nawambia, mpaka sasa atota,
        Kwa shakawa takimbia, lakini kwao asita,
        Ni wapi sasa dandia, kijana sasa kadata,
        Mila hii mila gani? Namtata nauliza.
47.   Na sasa lanitandama, sembuse mie wa bara,
        Haweshi kuniandama, kwa vigezo vya ukora,
        Na mashariti pindama, na kujikweza ubora,
        Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
48.   Na sasa tafanyanini, sihitaji kalimani,
        Simini aniamini, Simini kwangu amani,
        Ni wazazi lawamani, ndio yetu mitihani,
        Mila hii mila gani? Namtata nauliza.
49.   Ni kikao hakijesha, na wazee wajadili,
        Pingamizi zilikesha, ili tusiwe wawili,
        Takikisha najivesha, kivyovyote mesawili,
        Mila hii mila gani? Namtata nauliza.
50.  Baba mwana lisimama, na kukata na shauri,
       Mwanangu katu kiama, kwa bara piga zumari,
       Nitakupiga nakama, kiniletea kiburi,’
       Mila hii mila gani? Namtata nauliza.
51.  Takuja vipi olewa, na jitu liso mbolea,
       Tahizika kitolewa, kwa chogo kutembelea,
       Varuvaru ashakuwa, ni goro tazomelea,’
       Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
52. ‘ Tanakamishwa kipinga, usiole nazo raha,
       Kiendelea ka manga, Takoma kwazo karaha,
       Kibweteka  ko Mafinga, tandoka kwa majeraha,’
      Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
53. ‘ Jaribu tena uone, ndio kikao ukomo,
      Rasimi nisikione, nimekifunga mikono,
       Na goro huyu simone, taondoka kwa mishono,’
       Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
54.  ‘ Yasimini subiria, ame yako kungojeya,
        Tena haraka rejea, aghalabu tanogeya,
        Kwa  goro hutosifia, kwa uzuri wa amiya,’
        Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
55.  Mali yake yakutosha, pia na sisi tafika,
        Na tena tabu  tavisha, joho isije oneka,
        Sikini takurupusha, na kwetu utazomeka,’
        Mila hii mila gani? Namtata nauliza.
56. ‘Pamoja baba wanena, haki yangu wakaliya,’
       “Yasimini siwe lana, baba yako meongeya,”
       “Pamoja baba wanuna, Dini ndo kanichumbiya’
        Mila hii mila gani?  Namtata nauliza. 
57. ‘Simini kiendelea, na mimi kujibizana,
       Ni moto unakolea, tahiliki kwazo lana,
       Kwanza mbali potelea, takulani ewe mwana,’
       Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
58.  Tawanyikeni mesema, sihitaji kuwaona,
        Jambo hili limelema, wa mana sijamuona,
        Ni kauli nimesema, na wala sipaki hina,’
        Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
59.  Ndugu zangu isilamu, muogopeni qudusi,
       Kwa moto wa jahanamu, mufanyayo ni maasi,
       Meishikwa na naumu, kwa kubagua unasi,
       Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
60.   Wachunguzeni vijana, waishivo kwenye lana,
        Watoto wachafiana, libasi wavuliana,
        Mapenzi ya kupendana, wamekosa hawa wana,
       Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
61.  Nishaurini ndu zangu, kwa msiba lonipata,
      Nahitaji na mwenzangu, mitendeni sikupata,
      Hawabali hali yangu, jenda heka mesifata,
      Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
62.  Pakalini baguana, na wazawa wenguana,
      Wenyewe mwabezuana, wenye mali chaguana,
      Sikini wakaliana, wangojea buruzana,
      Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
63.  Mwenzangu mlo mtenga, kwa kisa hana jihenga,
       Na nyumba kutokujenga, bodaboda si kitunga,
       Si yeye ana ujinga,  elimu kwake mzinga,
       Mila hii mila gani?   Namtata naulizia.
64  .Muogopeni rabana, rasuli amemtuma,
       Kwa diniye lo bayana, ni kwa nini mwachutama,
       La nikahi twasutana, na pia kunisakama,
       Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
65.  Tafadhali walo wangu, tazama wanoyafanya,
       Metoka tangu na tangu, vijana tokwa na haya,
       Wapate kulinda tangu, nyumbani silete haya,
        Mila hii mila gani?  Namtata naulizia.
66.   Tavumilia kipindi, vijana sasa twachoka,
        Bila kujali makundi, tajilinda kwa mashoka,
         Twataji wetu ushindi, ulomezwa na mahoka,
         Mila hii mila gani ?  Namtata naulizia.
67.   Rijali pia banati, wote mefika wakati,
        Kudai zetu chapati, noliwa kihayawati,
        Na watu wenye mashati, wakilindwa  na manati,
        Mila hii mila gani?  Namtata naulizia.
68.   Thubutu sasa jaribu, kuzuwia ombwe kazi,
        Twakomboe so adhabu, na sitara zizozizi,
        Sitirike sio tabu, washirati kumaizi,
        Mila hii mila gani?  Namtata naulizia.
69.   Waso yale wazuzuri, tayazuru makaburi,
        Zajirani meshamiri, mukomboke na kiburi,
        Punguzeni na mahari, ni mahari so uturi,
        Mila hii miola gani?  Namtata naulizia.
70.   Naufunga mjadala, haki fike maisara,
        Vijana chushwa kulala, kwa vigezo vya kafara,
        Mefika sasa pahala, nani basi huuchwara,
        Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
71.    Kaditama ya tamati, kabula yangu  mauti,
          Nauasa huumati, tusifuge mabanati,
          Zingatieni jamati, wasia hu ndio hati,
          Mila hii mila gani?  Namtata nauliza.
72  . Mashattani wa haramu, tashabbahu shubuhani
        Mithilisha ya shattamu, tashakkamu shakuwani
        Watanassabu masumu, wahumu majuhalani
         Mila hii mila gani? Namtata enda keti
                                SHUKURANI.
         PEKE ALLAH SHUKURIWE,  KWA YAKE YALO MAPANA
         KISHA KWA KILULUWALE, KWA MSADA ULOFANA
         NATAJA MKANALILE, PAMOJA NA MWAKUMUNA
         RAFIKI ANGU MAKOE, NI OMARI LAKE JINA
          KWA KUKATA NA UTEPE, KUFANIKISHA KUBUNA
          NI KWAO KILA LA KHERE, ATULIPE NA FAUNA
          WAZAZI NIWAOMBEE, KWA YAO YALO YA KINA
           KWA KUNIENGA BEBEBE, TANGU NIKIWA USHINA
                                                        Aaamin
                                                   Namtata I.A.Y
                                                       07-05-2013
                                            MUM/T/BAED/11/3236
                                    +255717545353/+255688255913
                                      namtatatheschooler@gmail.com
                                     Muslim University of Morogoro.
Share on Google Plus

About Omari Makoo

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment