-->

KWA MARA YA KWANZA LOWASA ASHAMBULIWA NA POLISI NCHINI TANZANIA


Kwa mara ya kwanza mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA na Umoja wa Katiba ya Wananchi UKAWA, Edward Lowassa jana alikumbana na joto la upinzani baada ya msafara wake kushambuliwa na mabomu ya polisi huko mkoani Arusha, kaskazini mwa Tanzania. Tukio hilo, lililotokea mbele ya msafara wa mgombea huyo wa urais, lilijiri eneo la Daraja la Nduruma katika Jiji la Arusha na kusababisha umati wa watu kutawanyika na wengine kutelekeza magari yao. Lowassa alikumbwa na kadhia hiyo, wakati akiwa njiani na mgombea mwenza, Juma Duni Haji na viongozi wengine wa Ukawa, wakitokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), huku wakiwa wamesindikizwa na umati mkubwa wa watu na magari. Tayari kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas amethibitisha kujiri kwa tukio hilo na kuongeza kuwa, polisi walilazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi ili kuwatawanya watu waliokuwa wakifanya vurugu na wengine kufunga barabara. Katika tukio hilo, idadi kubwa ya polisi walikuwa kwenye magari na silaha mbalimbali ambapo baadaye walianza kurusha mabomu ya machozi kutawanya watu na magari katika eneo la daraja hilo. Lowassa aliwasili uwanja wa ndege KIA saa tatu asubuhi akiwa ameongozana na viongozi wa Ukawa, Mbowe, Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia na Mwenyekiti wa NLD, Emmanuel Makaidi, Kaimu Mwenyekiti wa CUF taifa, Twaha Taslima na viongozi wengine kadhaa.
SOURCE:SAUTI YA TEHRAN
Share on Google Plus

About Omari Makoo

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment