Itakumbukwa
tarehe 16/06/2013 ilikuwa ni siku ya uchaguzi mdogo wa madiwani kwa
baadhi ya kata nchini. Uchaguzi huo umefanyika kwenye kata ishirini na
mbili (22) kati ya kata ishirini na sita (26) zilizotangazwa kufanya
uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi wazi.
Matokeo tuliyoyapata toka
kwenye maeneo yaliyofanya uchaguzi yanaonyesha kuwa kati ya kata 22
zilizofanya uchaguzi CCM tumeshinda kata 16 sawa na asilimia 72.72% na
wenzetu wamechukua kata 6 zilizobaki sawa na asilimia 27.28%.
Tunawashukuru
sana kote walikoonyesha imani yao kubwa kwa Chama chetu kwa kutupa
dhamana ya kuendelea kuwatumikia. CCM inawaahidi utumishi uliotukuka.
Hata wale 27.28% walioamua kuwajaribu wenzetu, tunawatakia kila lakheri,
kwani wametumia haki yao ya kidemokrasia kuchagua wanaodhani
watawasaidia kufikia malengo yao ya kimaendeleo. Uchaguzi kwenye kata
hizi zote umeisha sasa tuwatumikie wananchi.
Kata nne za jiji la
Arusha hazikufanya uchaguzi baada ya kuahirishwa kufuatia tukio la
kusikitisha la kulipuka kwa bomu kwenye mkutano wa kampeni wa Chadema
mjini Arusha tarehe 15/06/2013.
CCM
tunalaani tukio hilo la mlipuko wa bomu na matukio yanayofanana na hayo
katika nchi yetu. Tunawapa pole wale wote walioathirika na tukio hilo.
Ni vizuri serikali ikalichunguza swala hili kwa kutumia muda mfupi na
kuhakikisha waliohusika wanapatikana na kuchukuliwa hatua zinazostahili.
Pamoja
na kulaani na kuitaka serikali kukomesha vitendo hivi nchini, ni wakati
muafaka kwa vyama vya siasa nchini kujitazama upya kwani kuna kila
dalili kuwa tukio hili kama alivyonukuliwa na baadhi ya vyombo vya
habari mhe. Mbowe Mwenyekiti wa Chadema Taifa kuwa ni la kupangwa,
inawezekana limepangwa na Chadema wenyewe.
Hali ya kisiasa jijini
Arusha kuelekea uchaguzi huo ilikuwa wazi kuwa wana Arusha walishaamua
kuzirudisha kata hizo nne kwa CCM, hasa baada ya kuchoshwa na maandamano
na vurugu za kila siku jijini Arusha. Aidha kauli za kukata tamaa za
viongozi wa Chadema na vitendo vyao ni dalili tosha kuwa tukio hili
lilipangwa na Chadema wenyewe.
CCM
tunaendelea kusisitiza na kulaani juhudi za wenzetu kujaribu kujenga
umaarufu wa chama chao juu ya damu za Watanzania. Juhudi hizi zinapaswa
kulaaniwa na wazalendo wote ndani na nje ya nchi. Tukumbuke asiyekubali
kushindwa, si mshindani. Si busara wala uungwana na ni kinyume na utu
kutumia majanga ya kutengeneza kama mtaji wa kisiasa.
Lakini CCM
tunalaani pia kitendo cha viongozi wa Chadema kujaribu kutumia baadhi ya
misiba na majeruhi wa tukio hili kisiasa na mwisho wa siku kwenda
kuwatelekeza hospitali baadhi yao baada ya kuwaahidi kubeba gharama zote
za matibabu na mazishi.Tunaipongeza serikali kwa kuingilia kati na
kuwasaidia waathirika hawa na kuhakikisha wanapata huduma inayostahili.
CCM
inarudia kueleza masikitiko yake kwa waathirika wa tukio hili la
kinyama na kikatili lisilostahili kuvumiliwa hata kidogo. Kama Chama
tumeguswa sana na tukio hili pamoja na kulilaani, tunawasihi watanzania
tushindane na kutofautiana bila kupigana na kuvunja tunu ya nchi yetu ya
amani na utulivu. Katika demokrasia ya vyama vingi swala la kuvumiliana
ni swala la msingi sana katika kufikia ukomavu wa demokrasia hiyo.
Imetolewa;
Nape Moses Nnauye
Katibu wa CCM Itikadi na Uenezi.
17/06/2013
Nape Moses Nnauye
Chama Cha Mapinduzi
Ideology and Publicity Secretary
SOURCE:CCM CHAMA BLOG
-
Blogger Comment
-
Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments :
Post a Comment