ANNE SEMAMBA MAKINDA: NANI NI NANI URAIS CCM?
HISTORIA YAKE
Anne Semamba Makinda alizaliwa Julai 26, 1949 mkoani Njombe, zamani sehemu ya Iringa (atafikisha miaka 66, Julai mwaka huu).
Baba yake alikuwa mkuu wa mkoa aliyefanya kazi katika utawala wa Mwalimu Julius Nyerere kwa hiyo Makinda alikulia katika malezi ya watu wa daraja la kati au juu tofauti na Watanzania wengi wa wakati huo.
Alianza masomo yake katika Shule ya Msingi Uwemba iliyoko Njombe na kisha akaenda Shule ya Wasichana Peramiho kwa masomo ya kati “middle school” ambayo yalikuwa ya shule ya msingi. Hii ilikuwa mwaka 1957 - 1964.
Makinda alijiunga kidato cha kwanza mpaka cha nne katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Masasi iliyoko mkoani Mtwara mwaka 1965 - 1968, kisha kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Kilakala mkoani Morogoro mwaka 1969 - 1970. Shule hii wakati huo ikiendeshwa na masista wa kigeni kutoka shirika la Kikatoliki la Salvatory.
Wakati alipokuwa shule ya msingi, alikuwa mwanachama wa Umoja wa Vijana wa Tanu na alipokuwa akisoma sekondari wilayani Masasi, alikuwa mwenyekiti wa tawi la vijana la Tanu na pia kiongozi wa wanafunzi kwa ujumla. Makinda amekuwa kiongozi tangu akiwa mtoto. Baada ya masomo yake ya Sekondari, Makinda alijiunga na Taasisi ya Maendeleo na Usimamizi ya Mzumbe (IDM) ambacho siku hiki ni Chuo Kikuu cha Mzumbe ambako alihitimu Stashahada ya juu ya Uhasibu mwaka 1971 – 1975.
Alipohitimu Mzumbe, Makinda aliajiriwa na Shirika la Ukaguzi Tanzania (TAC) na alikuwa kwenye uangalizi kabla ya kupewa mkataba wa muda mrefu ndipo alipoamua kujiunga katika siasa za kitaifa.
Pamoja na kuanza harakati za siasa, Makinda bado alijiunga katika Taasisi ya Usimamizi wa Fedha ya Dar Es Salaam (IFM) na kuchukua kozi ya awali ya CPA mwaka 1975 – 1976 na hadi leo yeye ni mhasibu aliyeidhinishwa na kusajiliwa kisheria.
MBIO ZA UBUNGE
Makinda ana rekodi nzito ya kisiasa nchini, huenda kuzidi wanawake wengine wengi tu. Alianza ubunge akiwa na miaka 26 tu, hii ilikuwa mwaka 1975 na alipata fursa hii kupitia kundi la vijana wa CCM na ilikuwa ni lile bunge ambalo pia kina Samwel Sitta waliingia. Makinda ndiye aliyekuwa mbunge mdogo kuliko wote.
Wakati Makinda anajiunga na siasa za kitaifa, ilimpasa kuacha kazi katika Shirika la Ukaguzi Tanzania (TAC). Aliacha mshahara ambao ulikuwa mkubwa mara kadhaa kuliko wa mbunge na kuamua kujiunga na Bunge.
Alikuwa mbunge wa kawaida kwa miaka minane kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, akiwa anasimamia masuala ya Sera na Udhibiti wa Majanga mwaka 1983 akiwa na miaka 31.
Makinda alikuwa Waziri wa Nchi huku akibadilishiwa majukumu mara kwa mara ikiwamo kushughulikia masuala ya Muungano, Uratibu wa Serikali Kuu hadi mwaka 1990.
Alipewa tena nafasi ya ubunge ndani ya CCM baada ya uchaguzi wa mwaka 1990 na Rais Ali Hassan Mwinyi kwa mara nyingine, akamteua kuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto. Aliongoza wizara hiyo hadi mwaka 1995 alipoamua kuchukua fomu ya ubunge wa jukwaani, “kupambana na wanaume” ambao wamezoea kuwa “wanawake ni watu wa kupewa”, Makinda alisema hatasubiri kupewa tena.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, Makinda alipambana na mgombea wa NCCR, Dk Herman Ndembelwa Ngunangwa (PhD) – sasa marehemu.
Dk Ngunangwa huyu ni yuleyule aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo la Njombe Kusini mwaka 1990 – 1995 kupitia CCM na alikuwa mmoja wa wabunge maarufu wa “G55” walioongozwa na kina Njelu Kasaka.
Makinda alipata asilimia 49.6 ya kura zote dhidi ya 48.5 za Ngunangwa. Wakati anaendelea na ubunge, pia aliteuliwa na Rais Mkapa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma mwaka 1995 – 2000 na Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 alishinda ubunge wa Njombe Kusini kwa mara ya pili na ndani ya Bunge, akapewa jukumu la kuongoza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maliasili, Mazingira na Kupambana na Umasikini.
Mwaka 2005 alishinda kwa mara ya tatu akipata asilimia 83.3 dhidi ya Martin Juju Danda wa Chadema (sasa kada wa NCCR) aliyepata asilimia 15.6. Makinda alichaguliwa kuwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri la Muungano wa Tanzania, akadumu kwenye nafasi yake hadi mwaka 2010.
Mwaka 2010 aligombea tena ubunge Njombe Kusini na kupita bila kupingwa na alipotua Dodoma ndipo akachaguliwa kuwa Spika wa Bunge la Muungano.
Kwenye uchaguzi wa Spika, Makinda alipata kura 265 dhidi ya kura 53 za Mabere Marando wa Chadema (kura tisa ziliharibika).
MBIO ZA URAIS
Makinda hajautangazia umma wa Watanzania rasmi kuwa atagombea urais, lakini yeye ni miongoni mwa wanawake walioko ndani ya CCM ambao wanatajwa. Pia ni miongoni mwa makada wanawake wanaohofiwa ikiwa chama hicho kitaamua kumpa mwanamke nafasi ya kupeperusha bendera ya CCM.
Wakati huohuo, minong’ono ya Makinda kutaka kugombea urais inachagizwa na uamuzi wake wa kustaafu ubunge. Makinda ameachana na siasa za jimboni bila kueleza anaelekea wapi na kwa sababu ya ombwe la taarifa hizo, ndiyo anawekwa kwenye orodha ya wanaohisiwa au kupigiwa chapuo na chama chake.
NGUVU YAKE
Makinda ana rekodi nyingi ambazo zinamtofautisha na wanawake wengi. Ni mwanamke pekee (au mmoja wa wanawake wachache sana) ambaye amekuwa mbunge kwa rekodi ya umri mdogo wa miaka 26 tu hapa nchini.
Ndiye mwanamke wa kwanza kuwa Naibu Spika wa Bunge la Tanzania mwaka 2005 na pia mwanamke pekee wa Tanzania ambaye amevunja rekodi ya kuwa Spika wa Bunge la Tanzania. Wanawake wengine hawajavunja rekodi hizi.
Jambo la pili linalompa nguvu ni uwezo wa kujisimamia. Tangu alipokuwa anasoma shule ya msingi na baadaye Sekondari, Makinda amekuwa ni mtu wa kujisimamia na kufuata taratibu na miiko ya kazi yake.
Nidhamu hii ndiyo imemfanya apite safari ndefu mno ya uongozi tangu akiwa na umri mdogo hadi amekuwa mtu mzima.
Makinda ni mtulivu na ana uwezo mkubwa wa kiuongozi. Katika safari yake ya miaka zaidi ya 35 katika uongozi wa nchi, amesimamia kila jambo alilopewa na hakuwahi kuhusika na mambo yenye madhara kiuongozi, yeye ni mtu wa kujikita katika aliloelekezwa na kulisimamia.
Mara kadhaa amewahi kusikika akisema kuwa ‘anapenda kuchapa kazi na anaamini anaweza kutenda kama wanavyofanya wanaume’.
Kwa asili yake, Makinda yuko karibu na watu na ni mtu wa kujichanganya, hajali nani aliyeko mbele yake. Wakati tuko kwenye Bunge Maalumu la Katiba (BMK) angeweza kutembea mita 30 kwenda kuwasalimu wajumbe ambao hawajui kabisa.
Mawaziri wengi katika Baraza la Rais Jakaya Kikwete hawawezi kufanya kama mama huyu, kusalimiana nao ilikuwa hadi wewe uwafuate ukawasalimu, lakini “bosi” huyu wa Bunge la Muungano yeye kwake haikuwa shida, ni mtu wa kujishusha na anajua maana ya uongozi.
UDHAIFU WAKE
Moja ya udhaifu wa Makinda ni kupoteza muda mwingi akitekeleza matakwa ya walio juu yake bila wakati mwingine kuyapa changamoto ili wakubwa watoe mawazo sahihi au maelekezo yanayoeleweka.
Katika uongozi wake wa Bunge, amekuwa mtu mwepesi kwa CCM, mara nyingi Serikali inapata ahueni kubwa katika mijadala yake kwa sababu Makinda hachukui hatua na analiongoza Bunge kama vile ni sehemu ya Serikali. Kuna mahali anapaswa kuchukua hatua akiwa Spika lakini anaishia kusaidiana na Serikali na au kuilinda.
Wakati wa sakata la Tegeta Escrow, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alipaswa kuwa mmoja kati ya watu ambao wangewajibishwa maana madhambi yaliyotendeka yaliihusu Serikali ambayo yeye anaisimamia hata kama hakuhusika moja kwa moja.
Makinda alikuja juu pale alipoona jambo lile linamgusa Waziri Mkuu, alikataa mapendekezo ya PAC yasiwe maazimio ya Bunge hadi yafanyike maridhiano na mjadala. Chelewesha hiyo ndiyo baadaye iliunda kamati iliyokuja na maazimio ya kumuokoa Pinda na kuwatosa mawaziri wake.
Kutokana na utendaji wa namna hiyo, ndipo taswira ya woga na kuogopa mamlaka pia inaweza kujengeka, kwamba mwanamama huyu ana kiwango fulani cha woga unaopaswa kutokuwapo kiuongozi, amekuwa Spika wa Bunge la watu, amechaguliwa na wabunge kwa niaba ya wananchi wa Tanzania.
Alipaswa kutumia ule utaratibu wake wa kuzingatia taratibu, kanuni na misingi bila kuzubaishwa na matakwa ya chama chake. Unapokuwa Spika wa Bunge halafu ukawa unawasaidia mawaziri wanapozidiwa na wabunge, hautoi mfano mzuri wa uongozi.
NINI KINAWEZA KUMFANYA APITISHWE
Makinda ni mwanamke aliyekulia ndani ya mfumo wa uongozi wa nchi na anakijua chama chake vizuri. Kama CCM inahitaji mwanamke anayeitambua mifumo ya uongozi wa nchi na matatizo yake na labda ambaye atathubutu kuziba pale wenzake walipotoboa, huenda yeye ni chaguo sahihi hata kama inaweza kuhojiwa kiwango cha ushiriki wake katika ‘kutoboa’.
Jambo jingine kubwa linalombeba ni “uadilifu”. Makinda ana taswira nzuri kwa jamii na anatoa mfano wa wanawake wa Kitanzania wenye asili ya maadili ya nchi.
Wanawake wa Taifa hili wana taswira ya uadilifu. Makinda tangu enzi na enzi amekuwa akiishi maisha ya kawaida yasiyotumia ofisi za umma vibaya. Jambo hili litambeba sana.
Uzoefu wake serikalini ni kitu kingine kinachomsaidia. Kama nilivyoeleza, amekuwa mkuu wa mkoa kwa miaka zaidi ya mitano, amekuwa waziri kwa miaka takribani 20, amekuwa katika Ofisi ya Spika wa Bunge la Tanzania kwa miaka 10, ameongoza pia umoja wa mabunge ya Afrika na taasisi nyingine za kibunge duniani. Uzoefu wake ni turufu tosha inayombeba.
Kama CCM itaikwepa taswira ya watu au wagombea wenye makundi, Makinda atafaulu mtihani. Hata uingiaji wake kwenye Ofisi ya Spika mwaka 2010 kuwa kiongozi wa Bunge ilitokana na CCM kumkwepa Samwel Sitta.
Makinda hakupewa uspika kama fadhila, bali alionekana ndiye suluhisho pekee na muda wote ambao amekuwa Spika, hajajitambulisha kwenye kambi za urais ndani ya CCM. Hili linamfanya awe mtu muhimu kwenye mbio hizi.
Pamoja na kuwa Makinda ni mwanamama, kuna nyakati nyingi tu anaweza kuwa mkali kupita kiasi na hata mbishi hadi afahamishwe jambo vizuri, lakini pia huwa tayari kushuka chini haraka pale anapoona kuna haja ya kufanya hivyo ili pande zinazosigana zielewane tena. CCM inahitaji mtu wa namna hii ikiwa itahitaji kurudisha nidhamu kama itabahatika kuchaguliwa tena mwaka huu.
NINI KINAWEZA KUMWANGUSHA?
Mambo mawili makubwa yanayoweza kumwangusha Makinda, kwanza ni kuwa na mtandao mdogo ndani ya chama chake.
Ikiwa mteule wa CCM atapimwa na vikao vya chama hicho kwa kigezo cha nani ana watu wengi na kwamba akiachwa chama kitayumba, basi hapa Makinda ataanguka.
Kama nilivyosisitiza awali, Makinda hajafanya harakati za wazi za kusaka urais na hivyo anaweza kuwa mtu ambaye hana kundi kubwa la wafuasi, labda hadi apitishwe na chama.
Dhana ya kuwaogopa wanawake au kuwahofia pia inaweza kumtafuna.
Vikao vya uamuzi vya CCM kama vilivyo vya vyama vingine, vimejaa wanaume kuliko wanawake na mara nyingi hata uamuzi hufanyika kwa wahusika kujisahau ikiwa wanawake ni sehemu yao pia.
Kasumba hii inaweza kuwa mwiba kwa Makinda ukizingatia hofu ileile ya CCM, kuwa vyama vya Ukawa vinaweza kusimamisha mwanamume ambaye anatizamwa na jamii pana ya Watanzania kama kiongozi anayeweza kuliko mwanamke (dhana mbaya).
ASIPOPITISHWA (MPANGO B)
Makinda anahitajika bado kulisaidia Taifa katika nafasi za juu. Mara kadhaa nimemuona akipatanisha wabunge ilipotokea wanagombana kwa kutumia njia rahisi tu. Uanadiplomasia huu unaweza kulisaidia Taifa katika nyanja nyingi ambazo zinahitaji kushughulikiwa.
Wakati huohuo Makinda anaweza kusaidia kukuza sekta ya uhasibu na ukaguzi. Ifahamike kuwa yeye ni mhasibu na mkaguzi kitaaluma na tayari amepata mafanikio makubwa ya kuwa mtu muhimu katika nchi.
Tunafahamu kuwa kati ya maeneo ambayo bado nchi ina matatizo ni kwenye ngazi hizo za uhasibu na ukaguzi.
Fedha nyingi za Taifa zinaibwa kwa sababu ya mianya kwenye sekta hizo, kama anapenda, anaweza kuhamia huko na akatumia ushawishi wake kuanza kuleta mabadiliko chanya kwa vijana.
HITIMISHO
Makinda ni mmoja wa wanawake wachache wenye bahati na bidii kubwa kazini. Historia yake inamhukumu kuwa ni Mtanzania aliyetoa mchango mkubwa kwa Taifa katikati ya mfumo ambao hauwapi wanawake nafasi.
Pia, utumishi wake katika Bunge umelipeleka katika ngazi nyingine kabisa. Bunge analoliacha mwaka 2015 ni tofauti na lile lililoboreshwa na Sitta kisha akaachiwa.
Naamini kuwa atautumia vizuri uzee wake kukamilisha kazi kubwa aliyoifanya hapa Tanzania, lakini yote kwa yote namtakia kila la heri katika hatua nyingine za kiuongozi au ujenzi wa nchi kwa kadri atakavyojiamulia.
KUHUSU MCHAMBUZI:
Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa na Kijamii, ana uzoefu mkubwa wa uongozi wa kisiasa hapa Tanzania. Ana Cheti cha Juu cha Sarufi na Lugha, Shahada ya Sanaa “B.A” katika Elimu (Lugha, Siasa na Utawala), Shahada ya Uzamili ya Utawala na Uongozi (M.A) na ni mwanafunzi wa fani ya sheria (L LB) – Anapatikana kupitia +255787536759,(juliusmtatiro@yahoo.com) Uchambuzi na huu unatokana na utafiti na maoni binafsi ya mwandishi). (Uchambuzi huu umechapishwa na Gazeti la Mwanchi la Jumapili, 26 Aprili 2015).

0 comments :
Post a Comment